Wednesday, July 2, 2025

JUMBE AREJESHA FOMU YA UBUNGE SHINYANGA MJINI... "ZOEZI LIMEENDA VIZURI, CCM IMEWEKA MAZINGIRA BORA KWA WATIA NIA"

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi James Jumbe Wiswa leo Julai 2, 2025 amerejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu katika ofisi za CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi Wiswa amesema zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu limeenda vizuri na kwa utulivu mkubwa bila changamoto yoyote.


"Leo nimekuja kwa mara ya pili, hatua ya kwanza ilikuwa ni uchukuaji wa fomu, nimejaza fomu, na leo ni siku ya urejeshaji. Tumekamilisha hatua ya awali ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu. Zoezi limeenda vizuri. Kimsingi, mimi binafsi na wala sijasikia kwa mtu mwingine kama kulikuwa na changamoto yoyote katika hatua hii," amesema Mhandisi Jumbe.

Mhandisi Jumbe amepongeza uongozi wa CCM Wilaya kwa kuweka mazingira rafiki kwa watia nia na wagombea, akieleza kuwa taratibu zimekuwa rahisi na hazichukui muda mrefu.


"Unapofika kuchukua fomu unapewa control number, unalipia, unakabidhiwa fomu na kuendelea na ujazaji na uwasilishaji. Niwapongeze Mwenyekiti wa Chama, Katibu, Sekretarieti na watumishi wengine kwa maandalizi bora," ameongeza.

FAHAD AJITOSA UBUNGE SHINYANGA MJINI KUPITIA CCM: AVUNJA UKIMYA TETESI ZA ACT-WAZALENDO

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Fahad Gulamhafiz Mukadam akionesha fomu kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

 Mtoto wa mwanasiasa mkongwe na Meya mstaafu wa Manispaa ya Shinyanga, Mzee Gulamhafiz Mukadam, bwana Fahad Gulamhafiz Mukadam, ameibuka hadharani na kutangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza leo Julai 2, 2025 mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho, katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Fahad amesema ameamua kutumia haki yake ya kikatiba na ya msingi kama mwanachama wa CCM mwenye sifa stahiki, ili kuchangia maendeleo ya wananchi wa Shinyanga kupitia nafasi ya ubunge.

"Mimi ni mtoto wa Shinyanga. Nimechukua fomu kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi kugombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini. Kama ilivyo taratibu za chama chetu, kila mwenye sifa ana haki ya kugombea. Nimetumia haki yangu ya kikatiba na natamani kushirikiana na wana Shinyanga kuleta maendeleo," amesema Fahad.

Aidha, Fahad ameweka wazi kuwa amechukua hatua hiyo kama sehemu ya kutekeleza dhamira yake ya kweli ya kuwatumikia wananchi, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira ya wazi ya kisiasa nchini.
"Kupitia uongozi wa Rais Samia, kila mmoja ameruhusiwa kusema. Mengi yamesemwa kuhusu mimi, lakini leo nimeamua kuzungumza kwa vitendo. Nipo katika ofisi za CCM, chama chenye misingi, imani na miundo imara ya kuleta maendeleo kwa Watanzania," ameongeza.

Avunja Ukimya Kuhusu Tuhuma za ACT-Wazalendo

Fahad pia ametumia nafasi hiyo kukanusha vikali taarifa zilizoenea kwenye mitandao na midomo ya watu kwamba anapanga kugombea ubunge kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

"Wapo wanaosema nagombea kupitia ACT-Wazalendo. Pamoja na heshima kubwa niliyonayo kwa vyama vya upinzani, sijawahi kutamka wala kufikiria jambo hilo. Ni minong'ono tu ya watu, nami leo nimejibu kwa vitendo kwa kuchukua fomu kupitia CCM," amesema.

Tetesi hizo zilianza kusambaa kwenye duru za kisiasa zikidai kuwa maandalizi ya Fahad kugombea kupitia ACT-Wazalendo . 
Hata hivyo, kwa hatua ya kuchukua fomu ya CCM, mambo yamewekwa wazi.

Kwa kufanya uamuzi huo, Fahad Gulamhafiz Mukadam amejiunga na orodha ya makada kadhaa wa CCM waliokwisha tangaza nia ya kuwania ubunge Shinyanga Mjini, huku ushindani ukiendelea kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.


Tuesday, July 1, 2025

Naibu waziri Sillo awajulia hali majeruhi ajali ya Same.


Na John Walter -Kilimanjaro 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, amefika katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Hospitali ya Mawenzi, na Hospitali ya Wilaya ya Same leo Juni 29, 2025, kwa ajili ya kuwapa pole na kuwajulia hali majeruhi wa ajali iliyotokea jana Juni 28, 2025, Wilayani  Same, mkoani Kilimanjaro.

Ajali hiyo iliyohusisha basi la Kampuni ya Chanel One na gari dogo aina ya Coaster (Rosa) imesababisha vifo vya watu 38 na kujeruhi watu wengine 30. Mhe. Sillo ameeleza masikitiko yake kutokana na tukio hilo na kutoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, huku akiwatakia majeruhi uponaji wa haraka.

Katika ziara hiyo, Mhe. Sillo ameambatana na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, SACP William Mkonda, pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Awadhi Juma ambapo wametembelea pia eneo la tukio iliyotokea ajali hiyo

Aidha, Naibu Waziri Sillo ametoa wito kwa Madereva wote kuzingatia Sheria za usalama barabarani na kuwa waangalifu wakati wote ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Mhe. Sillo ameongeza kuwa Serikali kupitia Vyombo vya Usalama itaendelea kuchukua hatua kali kwa wote watakaokiuka Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari ya abiria pamoja na kutoa elimu kwa Madereva.


Picha mbalimbali wakati alipowatembelea majeruhi na eneo la tukio.










Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...