Wednesday, September 30, 2020

Benki ya CRDB yaboresha huduma kwa Wastaafu Wastaafu sasa kuhudumiwa kidijitali

 


Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts (watatu kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mpango wa uwezeshaji kwa wastaafu uliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam, leo. 


Wengine pichani ni kutoka kulia ni Mwenyekiti wa makatibu Wakuu Wastaafu, Michael Mwanda, Balozi Mstaafu Salome Sijaona, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, Mwenyekiti wa Umoja wa Polisi Wastaafu, Kamishna wa Polisi Mstaafu Suleiman Kova na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi Benki ya CRDB, Adili Stephen.


Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts (watatu kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mpango wa uwezeshaji kwa wastaafu uliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam, leo.  Kulia ni Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa na kushoto ni Mwenyekiti wa Umoja wa Polisi Wastaafu, Kamishna wa Polisi Mstaafu Suleiman Kova.


Benki ya CRDB imezindua mpango maalum wa uwezeshaji kwa wastaafu ambao unatoa fursa mbalimbali zinazolenga katika kuboresha maisha yao. Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo wenye kauli mbiu ya "Ndoto zako hazistaafu", Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts amesema mpango huo anajumuisha fursa za kujiwekea akiba, uwekezaji, pamoja na uwezeshaji wa kifedha kwa wastaafu.


Dkt. Witts alisema pamoja na uzinduzi wa mpango huo Benki ya CRDB pia imezindua huduma za akaunti maalum ya wastaafu "Pension Account" na huduma ya uwezeshaji kifedha kwa wastaafu kidijitali "Pension Advance" kupitia huduma ya SimBanking App.


Akielezea kuhusu akaunti ya wastaafu, Dkt. Witts alisema akaunti hiyo inawawezesha wastaafu kupokea pensheni zao kwa urahisi na usalama na kujiwekea akiba kutokana na vipato vinavyotokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazozifanya. Dkt. Witts alisema ili kutoa nafuu kwa wastaafu akaunti hiyo hufunguliwa bure, haina makato yoyote yale na hutoa fursa kwa wastaafu kuunganishwa bure na mifumo ya utoaji huduma kidijitalli ikiwamo SimBanking na Internet Banking. 

"Ninajivunia kuwajulisha kuwa hadi leo hii tukiwa tunazindua mpango huu wa uwezeshaji wastafu, tayari wastaafu zaidi ya 19,000 wameshafungua akaunti hii na wanafurahia huduma zetu," alisema Dkt. Witts huku akibainisha kuwa kupitia akaunti hiyo wastaafu wanapewa TemboCard inayowawezesha kupata huduma kwa CRDB Wakala na ATM zote nchi nzima.


Kwa upande wa huduma ya uwezeshaji wa kifedha kupitia "Pension Advance", Dkt. Witts alisema sasa hivi wastaafu wanaweza kupata uwezeshaji wa fedha za kujikimu na kuendesha maisha yao kuanzia shilingi 50,000 hadi shilingi milioni 1 popote pale walipo kidijitali kupitia SimBanking App, huku akibainisha kuwa mkopo huo wa Pension Advance unatolewa bila riba yoyote.


Akizungumzia kuhusu fursa za uwekezaji zinazotolewa na Benki ya CRDB kupitia mpango huo, Dkt. Witts alisema benki hiyo pia imeanzisha akaunti maalum ya uwekezaji ijulikanayo kama "Akaunti ya Thamani" ambayo inawawezesha wastaafu kujipatia kipato kila mwezi. "Akaunti hii ya Thamani inatoa fursa kwa wastaafu kuwekeza kwa kipindi cha miaka mitatu kwa riba ya hadi asilimia 8," alisema Dkt. Witts.


Naye Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Rabala alisema kupitia mpango huo wa uwezeshaji kwa wastaafu benki hiyo pia imejipanga kuendelea kutoa mikopo kwa wastaafu ili kuwawezesha kuendeleza biashara na miradi yao ya maendeleo na hivyo kupunguza ukali wa maisha ya kila siku. Kupitia mkopo huo Wastaafu wanaweza kukopa kuanzia shilingi milioni 1 hadi shilingi milioni 100 kwa kipindi cha mwaka 1 hadi 7.

Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu Wastaafu, Michael Mwanda aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwakumbuka wastaafu kupitia huduma na bidhaa zinazotolewa na benki hiyo. Mwanda alitoa rai kwa wastaafu wote kuchangamkia fursa hizo kuboresha maisha yao huku akiitaka Benki ya CRDB kutoa semina juu ya huduma hizo kwa wastaafu wote nchi nzima.


Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Polisi Wastaafu, Kamishna wa Polisi Mstaafu, Suleiman Kova aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuja na mpango huo wa uwezeshaji kwa wastaafu huku akibainisha kuwa zitasaidia kuleta chachu ya maendeleo na kufanya kustaafu kusiogopwe. "Na sisi wastaafu sasa tunajidai tuna benki yetu ambayo sio tu inausikiliza bali pia inatambua mchango wa wastaafu katika taifa letu, Asanteni sana Benki ya CRDB," alisema Kova huku akimuomba Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts kumsaidia kufungua akaunti ya Wastaafu ili aweze kufurahia huduma zote zinazotolewa katika mpango huo wa uwezeshaji wastaafu.

Waliomuua Kada wa CCM Njombe Wakiri Kutekeleza Mauaji Hayo



Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Hamis Issa amesema gari namba T 457 DAB, Toyota Gaiya, mali ya George Sanga ambaye ni mgombea Udiwani Kata ya Ramadhani kwa tiketi ya CHADEMA ilitumika wakati wa utekelezaji wa mauaji ya kada wa CCM Emmanuel Mlelwa.





Sheria mpya kuhusiana na maandamano dhidi ya Netanyahu Israel

Bunge la Israeli limepitisha rasimu ya sheria iliyoandaliwa kupunguza maandamano wakati wa karantini, ambayo imechukuliwa katika mfumo wa kupambana na janga la corona.

Pamoja na muswada uliopitishwa asubuhi na mapema, wakati wa karantini, umma utaweza kushiriki katika maandamano sio zaidi ya kilomita 1 kutoka nyumbani kwao.

Uamuzi huu umefungua njia ya kuzuia waandamanaji kutoka nje ya jiji na kutoka maeneo ya mbali ya jiji kushiriki katika maandamano ya kila wiki ya kumpinga Netanyahu mbele ya makazi ya Waziri Mkuu huko West Jerusalem kwa zaidi ya miezi minne.

Wapinzani wa Israeli wameitikia uamuzi huo, wakisema kwamba kuzuia maandamano hayo kumeumiza demokrasia ya nchi hiyo na kwamba sheria hiyo imetumikia masilahi ya kisiasa ya Netanyahu kwa kutumia Covid-19 kama kisingizio.

Serikali ya Netanyahu iliamua kuzuia maandamano hayo wiki iliyopita, lakini jaribio hili lilishindwa kwa sababu ya bunge kukataa.

Kwa zaidi ya miezi 4 maandamano yamekuwa yakifanyika nchini Israel  yakimtaka Netanyahu kujiuzulu kwa sababu ya usimamizi mbaya wa janga la Covid-19 na kesi ya ufisadi dhidi yake.

 

Ubabe, Matusi Vyatawala Mdahalo wa Trump, Biden



ZIKIWA zimesalia siku 35 kuelekea  uchaguzi mkuu wa urais nchini Marekani utakaofanyika Novemba 3 mwaka huu, wagombea urais,  Donald John Trump wa chama cha Republican na mpinzani wake Joe Biden wa Chama cha Democratic, wamekabana koo kwa mara ya kwanza kwenye mdahalo uliowakutanisha katika jiji la Cleveland, Ohio, nchini humo.

Mdahalo huo ulioongozwa na mtangazaji wa Fox News, Chris Wallace, ulichukua dakika 90 hadi kumalizika.


Wagombea walikabiliana kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uchumi, uongozi, afya na janga la Corona huku kauli zisizo za kiungwana na za kibabe zikitawala wakati wa kujibu maswali

Aidha, kabla ya kuanza kwa mdahalo huo taarifa zilisambaa  zikieleza kuwa Rais Trump alipanga kutompa mwanya mpinzani wake kuzungumza na kumkatisha kila atakapokuwa anaongea jambo ambalo kweli amelifanya.


Katika suala la afya, Biden ambaye ni makamu wa rais mstaafu  wa Marekani amelaumu uongozi wa Trump kwa kudai idadi kubwa ya Wamarekani wanaugua magonjwa hatari kiafya

"Watu milioni 100 (Marekani) wanaugua magonjwa yanayowaweka katika hatari," alisema Biden.


Katika kujibu hoja hiyo Rais Trump alikanusha na kueleza idadi hiyo ilikuwa ni uongo huku akiwa hana jibu sahihi kuhusu idadi ya Wamarekani wenye matatizo ya afya.

Kwa mujibu wa idara ya afya nchini Marekani, kati ya watu milioni 50 na 129 ambao sio wazee tayari wamepata matatizo ya kiafya.


Mdahalo huo ulichukua sura mpya mara baada ya Trump anayesaka muhula wa pili kumwambia Biden "Watu wanaelewa kuwa miaka yako 47 ndani ya siasa hujafanya chochote wanaelewa," Trump alisema huku Biden akijibu na kusema " endelea kupiga kelele, utanyamaza tu" alisema mgombea huyo wa Democratic.


Katika kujadili suala la ugonjwa wa Corona ambao umesababisha vifo 205,942 nchini humo, Biden alimlaumu Trump kwa kusema "Watu wengi walikufa na wengine zaidi watakufa usipopata akili ya haraka kushughulikia," alisema Biden.

Trump aliyeongoza kwa kumkaripia mshindani wake pamoja na mwendeshaji wa mdahalo huo, Chris Wallace, alijibu na kusema, " watu wachache zaidi wanakufa sasa hivi, vilevile maambukizi yamepungua. Wewe kamwe usingeweza kufanya kazi ambayo sisi tumeifanya. Hicho kitu huna kwenye damu yako," hili lilikuwa jibu ya Trump kwa Biden.


Wagombea wote walionyesha kutofautiana takribani kwenye kila swali waliloulizwa na mwenyekiti wa mdahalo huo, kuanzia masuala ya afya, usalama, hadi ya kifamilia.


Sehemu kubwa ya mdahalo ilitawaliwa na Trump, ambaye wachambuzi wanasema alifanikiwa kuuendesha kwa njia yake mwenyewe, yaani badala ya kujadili masuala muhimu alikuwa anarusha maneno kama vile "Nyamaza kimya…hebu nyamaza wewe!!"


Kura za maoni zinamuonesha Biden akiongoza lakini Trump amesisitiza kauli yake ya kutokuwa na imani na mfumo wa upigaji kura kwa njia ya posta.


Pia amekataa kutamka kama atayakubali matokeo ya uchaguzi huo licha ya mshindani wake kusema yuko tayari kwa matokeo yoyote.

HESLB Yatoa Siku Tano (05) Kwa Wahitimu Mafunzo Jkt Kuomba Mikopo


Na Mwandishi Wetu, HESLB
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa muda wa siku 5 kuanzia Oktoba mosi hadi 5 mwaka huu ili kuwawezesha wanafunzi waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hivi karibuni kuingia katika mfumo wa kuomba mkopo kwa njia ya mtandao na kukamilisha maombi yao.

Katika taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari leo Jumatano (Septemba 30, 2020) Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru alisema uamuzi huo unatokana na maombi ya wanafunzi, wazazi na walezi ambao hawakuweza kuomba au kukamilisha maombi yao kutokana na sababu ya kujiunga na mafunzo hayo.

Kwa mujibu wa Badru alisema katika muda huo wa siku tano, mfumo pia utakuwa wazi ili kuwawezesha waombaji ambao maombi yao yana upungufu kurekebisha kwa kuweka nyaraka sahihi ili kuiwezesha HESLB kuendelea na hatua nyingine.

"Kwa wanaorekebisha taarifa, wanapaswa kuingia katika akaunti zao walizofungua kuombea mkopo na watapata ujumbe kuhusu maeneo ya kurekebisha. Tunawasihi watumie muda huu wa siku tano kurekebisha na kukamilisha maombi yao'' alisema Badru.

Katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga TZS Bilioni 464 zitakazowanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000. Kati yao, wanafunzi 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 91,000 ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo. Mwaka 2019/2020 jumla ya TZS 450 bilioni zilitengwa na zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119.

MWISHO



Source

Watuhumiwa 4 wa mauaji ya kada wa CCM Njombe,waidhinishiwa mashtaka ya mauaji ya kukusudia


Na Amiri Kilagalila, Njombe.

Ofisi ya taifa ya Mashtaka imewaidhinishia mashtaka ya mauaji ya kukusudia watuhumiwa wanne wa mauaji ya kada wa Chama cha Mapinduzi na kiongozi wa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu mkoa wa Iringa Emmanuel Mlelwa aliyeuawa mkoani Njombe.




 

Barabara za juu kutoka Mwenge kwenda Buguruni katika makutano za barabara ya morogoro,Nelson Mandela na Sam Nujoma zaanza kutumika rasmi leo

Barabara za juu kutoka Mwenge kwenda Buguruni katika makutano za barabara ya morogoro,Nelson Mandela na Sam Nujoma zaanza kutumika rasmi leo( Picha- MAELEZO)


 


Shauri la Muungano latolewa ufafanuzi

 


Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata amesema kuwa Mahakama ya Afrika Mashariki haina mamlaka kisheria kusikiliza hoja za kupinga uwepo wa Taifa la Tanzania lililotokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. 


Wakili Malata amesema hayo leo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu usikilizwaji na uamuzi wa shauri namba 09/2016 katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki baina ya Rashid Salum na wenzake 39,999 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyosikilizwa jana Septemba 29, 2020.


Wakili Malata amesema kuwa Mahakama ilikubaliana na hoja hizo ambazo kwa mujibu wa mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Tanganyika na Zanzibar sio nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bali mwanachama wa jumuiya hiyo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mnamo Novemba 2, 2016 Rashid Suleiman Adily na wenzake 39,999 walikwenda Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kufungua shauri namba 09 ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu kiongozi wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huyu Hapa Director wa Video WCB Wasafi Kenny na Mkewe...Wapata Mtoto


Huyu Hapa Director wa Video WCB Wasafi Kenny na Mkewe...Wapata Mtoto

Director Kenny ndio anahusika na Video zote za Wasafi ..Mwaka Jana Alipata tuzo ya Muongozaji bora wa Video Afrimma

Marekani Yampa Shavu Mondi



HUJATAJWAhata na mkuu wa mkoa, msanii unavimba kichwa! Sikia hii: "Serikali ya Marekani yampa shavu msanii Diamond au muite Nasibu Abdul a.k.a Mondi.


Kapu la stori za sanaa mwishoni mwa wiki iliyopita, lilijaa ishu kubwa ambayo Risasi liliinyaka kwamba, baada ya Diamond kufanya kolabo ya heshima na msanii wa Marekani, Alicia Augello Cook 'Alicia Keys', ubalozi wa nchi hiyo Bongo, umetoa shavu kwa Mondi kwa kuandika katika ukurasa wake wa Twitter: "Great to see American artist @aliciakeyscollaborate w/Tanzanian artist @DiamondPlatnumz."



 

Ambapo kwa Kiswahili ubalozi huo uliandika: "Inafurahisha kuona msanii @aliciakeys akimshirikisha msanii wa Kitanzania, @diamondplatnumz."


Jicho la mwandishi limebaini kuwa 'Twiti' hiyo ya ubalozi wa Marekani nchini, unaoongozwa na balozi Donald Wright, ni ya kipekee kwa Mondi na kwamba inawasha taa ya kijani kwa msanii huyo kutamba kimataifa.


CHANZO CHA PONGEZI NI HIKI


Chanzo cha pongezi za Marekani kwa Mondi, ni baada ya msanii huyo wa Bongo kushirikishwa na staa huyo wa muziki wa Marekani katika wimbo wake wa Wasted Energy, ambao unapatikana katika Albam mpya ya Alicia Keys iitwayo Alicia, ambayo aliifyatua Ijumaa, Septemba 18, mwaka huu.


Katika wimbo huo wa Wasted Energy, mtoto wa Tandale alitupia mashairi yake kwa Lugha ya Kiswahili, jambo ambalo wengi wamempongeza kwa kusema ameijenga heshima ya Tanzania kimataifa.


Kionjo cha mistari ambayo Mondi alimuonjesha msanii huyo wa kike mwenye mvuto wa Marekani, ni:"Kwa nini penzi umelikata miguu,Unalibidua mara chini mara juu?Why? (Kwa nini?)Why? (Kwa nini?)Moyo unaumia, Moyo unaumia Moyo unaumia kwa nini unaugeuza nguo karaha?


Eti karaha, oh-oh," yaani kama hivyo tu mzee baba; huku Alicia Keys yeye akitiririka sehemu ya mashairi yake kama ifuatavyo:


"Too many times, you turned a blind eye to the way I feel Oh, you're the reason why I'm numb And when I try to give you my time, it's never, ever ideal Had to learn it the hard way, oh yeah," akimaanisha hivi kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili:


"Mara nyingi sana, ulifumbia macho jinsi ninavyohisi Ah, wewe ndio sababu nimeshikwa na ganzi,Na ninapojaribu kukupa wakati wangu, sio bora kabisa, Ilibidi nijifunze kwa njia ngumu, oh ndio."


FAIDA KWA MONDI KWA KUTAJWA NA MAREKANI


Macho ya watazama mambo ya muziki kwa kina, yanaona kwamba kitendo cha Mondi kushirikishwa na Alicia Keys na kupewa heshima na ubalozi wa Marekani, kitamfanya msanii huyo kujulikana zaidi kimataifa, jambo ambalo lina faida kubwa kwake.


"Naona muziki wetu unakua sasa, kama wasanii wa Marekani wanaomba kolabo na sisi, hii ni hatua kubwa, hongera Diamond."


"Mzee jiandae kwa shoo za kufa mtu baada ya Corona kuisha.""Hii ni level nyingine kabisa ya Diamond, ila kuna wengine bado wanamchukulia poa, wakati dogo (Mondi) kapasua anga za Trump (Donald, rais wa Marekani).Hizo ni baadhi ya komenti ambazo zilitupia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kusherehesha kile alichoki-skoo kibabe mtoto wa Tandale.


REKODI TATU ZA KIPEKEE


Uchunguzi unaonesha kuwa, tukio la Mondi kushirikishwa na staa huyo wa Marekani, kumemfanya msanii huyo kuweka rekodi tatu kibabe.


Rekodi ya kwanza aliyoweka Mondi ni kwamba, anakuwa msanii wa kwanza Bongo kuombwa, rudia tena "kuombwa", siyo kuomba kolabo kwa msanii huyo mkubwa; kama ambavyo wasanii wengine huwa wanafanya; usichanganye madawa.


Nyingine ya ajabu ambayo ameiweka Mondi ni ile ya msanii kutoka Bongo kufanya kolabo hiyo na msanii nyota wa Marekani na wimbo wake kuingizwa kwenye nyimbo zinazokamilisha Albam kwa Bongo haijapata kutokea.Rekodi ya tatu ni kitendo cha ubalozi wa nchi kubwa kama Marekani kupongeza ushirikiano wa msanii wa nchi yake kufanya kolabo na msanii wa Bongo.


ALICIA KEYS ALIVYOANZA KUMZIMIA MONDI


Mapema wiki hii, Keys alitupia orodha ya nyimbo anazopenda kuzisikiliza ukiwemoNana ambao Mondi amemshirikisha staa wa Nigeria, Mr Flavour.


Kama hiyo haitoshi, alisikiliza pia Wimbo wa African Beauty ambao Mondi amemshirikisha staa wa Marekani, Omarion, hiyo ni kuonesha kuwa msanii huyo wa Marekani alianza kumkubali Mondi kitambo.


Kama hilo alitoshi mapema mwaka huu, mume wa Alicia Keys, Beatz naye aliposti wimbo wa Gere wa Mondi alioshirikishwa na aliyekuwa mwandani wake, Tanasha Donna ambapo alisema anatamani kuufanyia remix wimbo huo.


ALICIA KEYS NI NANI?


Alicia Keys ni mrembo, staa wa muziki wa R&B kutoka pande za Marekani, ambaye ana umri wa miaka 39. Amesumbua na ngoma zake kali ikiwemo No One ambayo ilikamata namba moja katika chati za Hot 100.


Wimbo huo ulikuwa kwenye Albam yake iliyofahamika kwa jina la As I Am, ambayo iliitoa mwaka 2007 na kusimama namba moja kwenye Billboard 200 nchini humo na kuuza kopi 742,000 kwa wiki ya kwanza.Hii ina maana kwamba, Alicia Keys siyo msanii wa kispotispoti ukilinganisha na wasanii wa Bongo.


NI SOMO KWA HARMO, KIBA NA ZUCHU


Katika kitu ambacho kinaonesha kuwa Wabongo wamekuwa na kiu ya kuona vitu vyao vinapenya kimataifa, waliwatolea mwito wasanii wengine kama Ali Kiba, Zuhura Othman 'Zuchu' na Rajab Abdul Kahali 'Harmonize' nao kuzidi kukaza buti, ili nao wapenye zaidi kimataifa.


"Umefika muda wa kuelewana, Wabongo tuzidi kuongeza sauti kwenye vitu vyetu, iwe michezo, sanaa na mambo mengine, ili tutoke kimataifa."


"Kazi kwenu wasanii wengine Bongo, mkichukulia ishu ya Mondi kichawi mtaishia kununa, lakini mkiichukulia positive, mtakaza buti ili nanyi mpite njia anayotoboa Diamond."


Baadhi ya komenti zilizotupiwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu ishu ya Mondi na pongezi za ubalozi wa Marekani.



Mambo muhimu mnayopaswa kufanya ili kuyafurahia mahusiano yenu


Mahusiano ya mwanaume na mwanamke hukutanisha watu kutoka koo mbalimbali. Kila mtu anakuwa amelelewa tofauti kwa wazazi wake.  Tabia haziwezi kufanana. Huyu anaweza kuwa na tabia fulani ambayo mwenzake anakuwa hana. Mnapokutana wawili, ili muweze kwenda sawa ni lazima muelewane tabia, mshibane na kila mmoja amvumilie mwenzake. Hakuna binadamu aliyekamilika. Inawezekana kuna vitu ambavyo mwenzako anavyo, na pengine si vizuri. Suala la msingi ni kupata muda sahihi wa kumbadilisha mwenzako ili naye aweze kukubaliana na mabadiliko unayotaka kumpa, na mwisho wa siku mtakwenda sawa.

Unapomuelekeza mwenzako juu ya tabia fulani, unapaswa kutumia lugha rafiki; lugha ya mtu na mpenzi wake! Ambayo itamfanya asijisikie vibaya, akubaliane na kile kitu unachomueleza bila hata ya kuweka kipingamizi. Ukitumia lugha ya ukali, yenye kuonesha dharau na kuona anachokifanya ni cha kijinga, basi jua unakaribisha ugomvi. Utamfanya akuone unamdharau na mtu akishaona anadharaulika, hata kama kitu unachomueleza ni kizuri, anaweza kukipinga tu.

Inahitaji busara, hekima ya hali ya juu ili uweze kumkosoa mwenzi wako. Yawezekana kwa mazingira aliyolelewa, anachokifanya huamini ni sahihi lakini sasa amekuja kwako, mnaanzisha ulimwengu wenu, hivyo inahitajika akili ya ziada kuweza kumbadilisha. Tengeni muda mzuri wa kuelezana mambo mbalimbali ya kudumisha uhusiano wenu. Mzungumze na kusikilizana. Kila mmoja amueleze mwenzake kile anachoamini kinaweza kusaidia kustawi wa penzi lao, kwa kutumia lugha nzuri isiyokuwa na kebehi.

Mnapokuwa kwenye uhusiao, kwanza kila mmoja ajifunze namna ya kujipenda mwenyewe. Unapojua kujipenda mwenyewe na ukajua unahitaji nini ili kuipata furaha yako, basi ni rahisi sana kumtafutia mwenzako pia furaha unayoipata wewe. Usiwe na ubinafsi, furaha unayoipata wewe mpe na mwenzako. Unavyojijali, basi mjali na mwenzako. Kujipenda unavyojipenda basi kwa kiasi hichohicho mpende na mwenzi wako. Ukifanya hivyo, mwenzi wako naye hatakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kukurejeshea upendo.Related image

Jifunze kuwa na imani na mwenzako. Unapomjengea mwenzako imani, inamfanya wakati mwingine ashindwe kufanya maovu. Unapomuamini, unamfanya mwenzako ajiheshimu, maana anajua unamuamini na akifanya lolote la kijinga, lazima nafsi yake itamsuta. Muamini mwenzi wako. Mtengenezee mazingira ya kumuamini ili na yeye pia akuamini. Msiishi kwa kufuatiliana, maana maisha  hayapo hivyo. Binadamu hawezi kuchungwa kama kondoo au mbuzi. Kubwa linalohitajika ni kujua thamani ya kuaminiana.

Anayekuamini anakujali, anayekujali atakulindia heshima. Hivyo, mkigundua hilo na mkaelekezana kiutu uzima, hakika mtaaminiana. Kila moja awe mkweli na mwaminifu. Ni ukweli pekee utakaowafanya muwe na furaha muda wote. Mkiwa waongowaongo, hamtadumu. Uongo una madhara. Ujanja ujanja ni tatizo katika uhusiano. Kuwa mwaminifu kwa mwenzako, naye pia awe mkweli na mwaminifu.

Kuweni nyinyi, tengenezeni maisha yenu. Msijilinganishe na mtu mwingine. Wekeni mikakati yenu na namna mnavyotaka kuishi, ishini maisha yenu. Mkiyafanya hayo yote, hakika penzi lenu litastawi na mtafurahia maisha ya uhusiano, uchumba na hata ndoa!


ASKOFU SANGU AOMBA MSAADA KUKARABATI KANISA KATOLIKI NGOKOLO NA MITAMBO YA REDIO FARAJA ILIYOATHIRIWA NA MVUA YENYE UPEPO


Kushoto ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu,kulia ni muonekano wa sehemu ya kanisa iliyoathirika kwa kuangukiwa na mnara wa Redio Faraja

Na Simeo Makoba - Shinyanga
Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amewaomba wadau,waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na kutoa michango mbalimbali ili kusaidia ukarabati wa miundombinu ya kanisa kuu la jimbo na Redio Faraja ambayo imeathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.

Askofu Sangu ametoa ombi hilo katika kikao cha dharura ambacho kiliwahusisha Mapadre wa Parokia zote zilizopo katika manispaa ya Shinyanga,Viongozi wa Halmashauri ya walei kutoka kanisa kuu la Ngokolo pamoja na uongozi wa Redio Faraja Fm Stereo.

Askofu Sangu amebainisha kuwa,mvua kubwa iliyonyesha mjini Shinyanga jioni ya jana tarehe 28.09.2020 ambayo iliambatana na upepo mkali ilisababisha mnara unaotumika kurushia matangazo ya Redio Faraja Fm Stereo kuangukia kanisa na kusababisha uharibifu mkubwa wa sehemu ya kanisa na miundombinu ya Redio inayotumika kurushia matangazo.

Shinyanga limeguswa ikizingatiwa kuwa,kanisa kuu la Mama mwenye Huruma la Ngokolo ndiyo lililobeba sura ya jimbo halikadhalika Redio Faraja ndiyo chombo kikuu cha mawasialiano na uinjilishaji katika jimbo ambayo nayo miundombinu yake imeathiriwa.

Askofu Sangu amewaomba wadau wa Redio na Kanisa,Waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na kutoa michango mbalimbali ili hatua za kufanya ukarabati wa kanisa na mitambo ya Redio iliyoathiriwa ziweze kuanza mara moja.

Ameelekeza michango yote iwekwe kwenye Akaunti maalum ya jimbo la Shinyanga Benki ya CRDB yenye namba 01J1058390001 (DIOCESE OF SHINYANGA) na kwa njia ya M-PESA kwa namba 0762444746 yenye jina la Liberatus Sangu.

Wakati huo huo, Askofu Sangu ameunda kamati maalum ambayo itashughulika na mchakato wote wa tathmini pamoja na kusimamia hatua zote za ukarabati wa kanisa na miundombinu ya Redio iliyoharibiwa,ambayo itaongozwa na Paroko wa Parokia ya Ngokolo Padre Aldof Makandagu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Idara ya mawasiliano wa jimbo la Shinyanga Padre Anatoly Salawa amesema hivi sasa wanaendelea na mchakato wa kurejesha matangazo ya Redio katika eneo la Shinyanga kwa kufunga Antena katika sehemu ya mnara iliyobakia ili kuwawezesha wananchi wa Shinyanga kufuatilia Matangazo ya Redio wakati hatua nyingine za kufanyia matengenezo miundombinu iliyoharibiwa zikiendelea.
Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu akiwa katika eneo la tukio wakati wa zoezi la kuondoa mnara juu ya paa la kanisa la Mama Mwenye Huruma Ngokolo. Picha na Samir Salum
Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu akiwa katika eneo la tukio wakati wa zoezi la kuondoa mnara juu ya paa la kanisa la Mama Mwenye Huruma Ngokolo.

Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Jimbo la Shinyanga, Padre Anatoly Salawa akionesha Mnara wa Matangazo ya Redio Faraja ulioangukia Kanisa la Mama Mwenye Huruma Ngokolo.

Muonekano wa mnara wa kurushia matangazo Redio Faraja Fm Stereo ukiwa umeangukia paa la Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga 
Muonekano wa mnara wa kurushia matangazo Redio Faraja Fm Stereo ukiwa umeangukia paa la Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga 
Muonekano wa sehemu ya ndani ya Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga baada ya kuangukiwa na Mnara wa Matangazo ya Radio Faraja Fm Stereo 
Muonekano wa sehemu ya ndani ya Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga baada ya kuangukiwa na Mnara wa Matangazo ya Radio Faraja Fm Stereo 
Muonekano wa sehemu ya ndani ya Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga baada ya kuangukiwa na Mnara wa Matangazo ya Radio Faraja Fm Stereo 
Muonekano wa sehemu ya ndani ya Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga baada ya kuangukiwa na Mnara wa Matangazo ya Radio Faraja Fm Stereo 
Muonekano wa mnara wa kurushia matangazo Redio Faraja Fm Stereo ukiwa umeangukia paa la Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga 
Muonekano wa mnara wa kurushia matangazo Redio Faraja Fm Stereo ukiwa umeangukia paa la Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga.

Tuesday, September 29, 2020

Mbaroni Kwa Kumbaka Mwanae Wa Kumzaa Shinyanga

SALVATORY NTANDU, SHINYANGA
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Kambarage Manspaa ya Shinyanga Petro Maro (43) kwa tuhuma ya Kumbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 13 Mwanafunzi wa Darasa la Saba.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Leo Septemba 29,2020 na Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema kuwa Petro alitekeleza tukio hilo Septemba 27 majira ya usiku nyumbani kwake.

Alisema kuwa Mama Msamaria mwema anayeishi jirani na Petro aligundua  binti huyo kubakwa na baba yake Mzazi na kisha kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ambao walifika na kisha kumkamata.

"Binti huyu alibakwa na baba yake usiku akiwa amelala na chanzo cha tukio hilo ni tamaa za kingono baada ya kutengana na Mke wake hali iyosababisha kuendelea kuishi na mwanae wa kike nyumba mmoja," alisema Magiligimba.

Kamanda Magiligimba alitoa wito wananchi mkoani humo kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ili kukomesha matukio na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto mkoani humo.

Aliongeza kuwa hatua Kali za kisheria zitachukuliwa kwa mtuhumiwa huyo na upelelezi ukikamilika atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

Mwisho.



Source

Mke wa King Kiki awaonya wanaojidai wasemaji wa familia



COSTANSIA Kalanda ambaye ni mke wa msanii muziki wa dansi nchini Tanzania, King Kiki, amefunguka kuhusu kuumwa kwa mumewe huyo huku akiwaonya wanaochukuwa jukumu la kuzungumzia afya ya mumewe.


King Kiki ni mmiliki wa bendi ya La Capital, inayotesa na mtindo wake wa Kitambaa Cheupe.


Habari za kuumwa kwa King Kiki zilizagaa wiki iliyopita  zikimuonyesha akiwa katika picha na familia yake kitandani  wakimpa msaada wa kukaa.



 

Taarifa hizo zilisema "Anaumwa yuko kitandani mwanamuziki nguli  anahitaji msaada wa hali na mali. Alikuwa anaumwa mgongo na baadae kupooza alilazwa Muhimbili gharama zikawa kubwa sasa uanugulia nyumbani kwake,".


Akizungumzia jambo hilo, mke wa msanii huyo Costansia, amesema taarifa za kuwa mume wake anaumwa ni za kweli japokuwa amekanusha kuwa familia haijashindwa kumuhudumia kimatibabu.


"Ni kweli King Kiki anaumwa, lakini taarifa kuwa ametoka hospitali kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu hazina ukweli wowote kwani familia tupo tunamuhudumia,"amesema.


Akizungumzia kuhusu ugonjwa unamsumbua, Costansia amesema alipata tatizo la uti wa mgongo kama mwezi mmoja uliopita na kufanyiwa upasuaji wa pingili za shingo wiki mbili zilizopita.


Amesema kutokana na upasuaji huo alijikuta akishindwa kunyanyuka na kukaa mwenyewe kutokana na madhara aliyopata wakati wa kuwekewa ganzi.


"Madaktari wametumbia kwa kuwa kutokana na King Kiki kuwa mtu mtu mzima ilibidi wampige ganzi ile ya kuuwa mwili mzima wakati wa kumfanyia upasuaji.


"Ni kutokana na hilo walisema ingemchukua takribani wiki mbili kurudi katika hali yake ya kawaida na mpaka tunafika leo wiki mbili hizo tayari zimefika, hapa tunafanya utaratibu kesho tumrudishe hospitali kwa uchunguzi zaidi," amesema Costansia.


Hata hivyo amewaonya watu wanajitwika usemaji wa familia kwa kumzungumzia msanii huyo  na kusema kwamba wanaopaswa kufanya hivyo ni yeye na mtoto wake mkubwa wa kiume.


Pia aliwaondoa hofu mashabiki wa msanii huyo na kueleza kuwa hayupo katika hali mbaya kihivyo kama inavyosemwa huku akiwaomba wamuombee  ili aweze kunyanyuka na kuendelea na kazi zake za sanaa.

Monday, September 28, 2020

KUTANA NA CHUCK FEENEY BILIONEA ALIYEGAWA MALI ZAKE ZOTE KWA WALIMWENGU


Chuck Feeney katikati amekuwa bilionea kwa muda wa miaka 40 iliyopita.
**
Charles "Chuck" Feeney ni bilionea ambaye alikuwa na ndoto za kumaliza mali yake yote akiwa hai, kwa kutoa fedha zake zote kwa mashirika ya hisani.

Mfanyabiashara huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 89 , hatimaye amefikia lengo lake siku chache ziliopita alipotoa dola ,milioni 8,000 kusimamia miradi ya hisani duniani.

Hivi sasa hana nyumba wala gari na ni maarufu kwa kuvalia saa iliyonunuliwa kwa dola 15 pekee.

''Nilikuwa na wazo ambalo halikuondoka katika fikra zangu , kwamba unapaswa kutumia mali yako kuwasaidia watu'', alisema mfanyabiashara huyo. Na kwa kipindi kirefu alichangisha fedha bila kujulikana.

Wakati mwandishi Gerardo Lissardy, kutoka BBC Mundo alipomuuliza 2017 kwanini alikuwa akifanya kuwa siri, alijibu, ''kwa sababu hakuna haja ya kuelezea watu kwanini unafanya hivyo''.

Kulingana na Conor O'Clery, aliyeandika kitabu kuhusu Feeney, anasema kwamba mtu huyo alipatiwa msukumo na kitabu cha 'Mali', kikijulikana, 'The Gospel of Wealth', kilichoandikwa na Andrew Carnegie.

Mishororo kama ''Kufa tajiri ni kufa kwa aibu'', iliwacha kovu katika fikra za Feeney. Alisafiri kote duniani kwa siri , akitafuta njia za kukamilisha kazi yake ndio maana aliitwa jina la Utani James Bond wa hisani.

Je Chuck Feeney ni nani? 

Charles F. Feeney alizaliwa mjini Elizabeth, New Jersey mwaka 1931. Mama yake alifanya kazi kama nesi katika hospitali huku baba yake akiwa wakala wa bima.

Akiwa kijana mdogo alionesha uwezo wake wa kufanya biashara.

Aliuza kadi za krisimamsi mlango hadi mlango akiwa na umri wa miaka 10. Akiwa kijana alisajiliwa katika jeshi na kushiriki katika vita vya Korea.
Chuck Feeney

Alitumia fursa ya mpango wa elimu wa Marekani kwa wakongwe na kuwa mtu wa kwanza wa familia yake kujiunga na chuo cha masomo.

Baada ya kuhitimu katika chuo kikuu cha Cornell University mjini New York , alianza biashara yake akiuza bidhaa kwa wanajeshi wa Marekani waliopo katika kambi barani Ulaya.

Biashara hiyo ilipiga hatua na kuwa maduka yasiotoza ushuru DFS kampuni ya mauzo isiotoza ushuru alioanzisha kwa pamoja na Robert Miller 1960.
Chuck Feeney alitoa fedha ya msaada Australia, Cuba na Ireland

''Mali inakuja na majukumu'' alikuwa akinukuliwa akisema.

''Sikufanya hivyo ili kuthibitisa chochote: Tajiri huyo aliyechangisha dola bilioni nane na kuwachwa na bila kitu.

''Watu wanapaswa kuchukua jukumu kutumia baadhi ya mali yao kuimarisha maisha ya wanadamu wenzao, la sivyo watajenga matatizo makubwa katika vizazi vya siku za baadaye''.

Kwa sasa anaishi katika nyumba ya vyumba viwili katika mji wa San Fransisco na mkewe Helga.

James Bond wa hisani
Mwaka 1982 alianzisha wakfu wa Atlantic Philanthropies Foundation , shirika la kimataifa kusambaza mali kwa miradi ya hisani duniani.

Katika kipindi cha miaka 15 ya kwanza, Feeney kisiri alichangisha fedha, na kumfanya kuitwa James Bond wa hisani, hadi alipojitokeza 1997.
Ufadhili umetajwa kubadili maisha ya wengi

Tangu alipoanzisha wakfu wa Atlatntic Phillanthropies, ametoa karibia dola bilioni nane kama misaada.

Wakfu huo umetangaza kwamba utasitisha operesheni zake siku ya mwisho ya mwaka wa 2020 baada ya lengo la Feeny kuafikiwa,

Filosofia yake ya kutoa wakati unapoishi imewapatia msukumo mabilionea wengi , ikiwemo mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates na mwekezaji Warren Buffet.

Feeney hajulikana sana kama matajiri wengine kwasababu ya kutoa michango yake kisiri katika kipindi cha kwanza cha miaka 15 cha kazi yake.

CHANZO- BBC SWAHILI

Bodi ya ligi yaufungia uwanja wa Jamhuri Morogoro

 


Bodi ya ligi kuu Tanzania (TPLB) imeufungia uwanja wa mabatini unaotumiwa kwa michezo ya nyumbani na klabu ya Ruvu Shooting kwa kukosa sifa za kimashindano.



Wednesday, September 23, 2020

NITAKUWA KIUNGANISHI KATI NGO'S,BUNGE,SERIKALI NA WAFADHILI KULETA MAENDELEO ENDELEVU-NEEMA

Mbunge Mteule Viti Maalum Kundi la Asasi za kiraia Tanzania bara Neema Lugangira (kulia) akizungumza jambo na baadhi ya viongozi wa Mtandao wa Vikundi vya wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) alipotembelea ofisi hiyo.



MBUNGE Mteule Viti Maalum kundi la Asasi za kiraia Tanzania bara kwa tiketi ya CCM Neema Lugangira, amesema kuwa atakuwa kiunganishi kati ya Asasi za kiraia(NGO'S), bunge, serikali, wafadhili na chama ili kubadilishana mawazo katika kuleta maendeleo endelevu.

Neema ameyasema hayo wakati alipotembelea Mtandao wa Vikundi vya wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) mkoani Morogoro ili kujua changamoto zinazo wakabili na namna ya kuzitatua. 

Ameeleza kuwa kwa kuongea na wadau hao anapata fursa ya kupata mambo ya kujadili yaliyomo kwenye ilani ya CCM yanayohusiana na Asasi hizo na kuweza kubadilishana mawazo yatakayosaidia kwenye utekelezaji.

Akizungumzia maeneo yaliyoguswa na ilani ya CCM amesema lengo kubwa ni kuongeza tija katika kilimo ili kusaidia viwanda, kuimarisha miundo mbinu na uzalishaji, kumsaidia mkulima kuzalisha na kupata masoko, usimamizi wa mazao ya kimkakati, lishe na kuzijengea uwezo Asasi za ndani.

Naye Mkurugenzi wa MVIWATA Stephen Ruvuga akitoa shukrani zake kwa chama na serikali amesema kwa kitendo hicho cha kiongozi kuwatembelea na kujua changamoto zao wanatarajia kuwepo kwa maelewano mazuri kati ya serikali na Asasi hizo, hali itakayochochea maendeleo kwa haraka.

Mkongo Wa Taifa Wa Mawasiliano Waunganisha Visiwa Vya Pemba Na Unguja

Na Prisca Ulomi, WUUM, Zanzibar
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka saini ya mkataba wa makubaliano wa kuunganisha visiwa vya Pemba na Unguja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Zanzibar

Utiaji saini huo umeshuhudiwa na katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Utiaji saini huo umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba kwa upande wa Bara na Mhandisi Shukuru Awadh Slueiman, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar (ZICTIA) kwa upande wa Zanzibar

Kabla ya kushudia tukio hilo, Dkt. Zainabu Chaula alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 700 na kuunganisha kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwenye nchi jirani za Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Malawi ambapo maunganisho haya yanaenda kufungua fursa za wawekezaji na watumia wa huduma za mawasiliano wa ndani na nje ya nchi  kuunganishwa na Zanzibar kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia kuibuka kwa mifumo ya TEHAMA ambayo inawezesha utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa kasi zaidi

Naye Dkt. Jumbe amesema kuwa haya ndio matunda ya mapinduzi, matunda ya mapinduzi sio maembe wala mapapai bali ni maendeleo yanayopatikana katika nchi yetu, na Serikali yetu ya SMZ imetumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kuunganisha mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba bali kulikuwa na changamoto ya kuunganisha Unguja na Pemba ila sasa kwa kupitia makubaliano haya, tutatumia barabara ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuunganisha visiwa Pemba na Unguja na hivyo Zanzibar kuunganishwa na Tanzania Bara moja kwa moja na utawezesha kupunguza gharama za mawasiliano ili ziwe nafuu

Ndugu Kindamba amesema kuwa ufunguzi wa njia za mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa sana kwa taifa hasa katika kuwezesha kuongezeka kwa matumizi ya data na intaneti na makubaliano hayo yanahusisha kutunza vifaa vya miundombinu ya TEHAMA vya ZICTIA kwenye majengo ya TTCL 

Mhandisi Suleimani ameongeza kuwa ZICTIA imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Zanzibar na sasa unaunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo itakuza na kuongeza huduma za mawasiliano; kuondoa changamoto iliyokuwepo Zanzibar ya kutumia njia ya mawasiliano ya mawimbi ya radio kutoa huduma za mawasiliano ambayo hayana kasi na ubora unaohitajika, kupunguza gharama za mawasiliano na kuingizia mapato kwa Serikali

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano


Bia iliyotengenezwa Kwa Kutumia Majitaka

Katika juhudi za kuongeza ufahamu juu ya uwezekano wa kuyabadilisha Majitaka kuwa maji salama kampuni moja inayozalisha bia jijini Stockholm nchini Swaeden imetengeneza bia iliyobatizwa jina la PU: REST kwa kutumia Majitaka yaliyotibiwa (recycled sewage water).

Kampuni hiyo ambayo katika uzalishaji wa bia hiyo wameshirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mazingira nchini Sweden imedhamiria kupitia kinywaji hicho kuwashawishi wakazi wa nchi hiyo kuwa 'Maji taka yaliyotibiwa (recycled sewage water)' ni maji safi na salama kama yanayotoka kwenye mabomba.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Mazingira nchini Sweden wamesema kuwa changamoto ya watu kutoyaamini majitaka yaliyotibiwa sio ya kiufundi bali ni changamoto ya kisaikolojia na ndio maana wametengeneza bia ili kuwashawishi watu kuyatumia Majitaka yaliyotibiwa.

Kwa sasa PU:REST bia inapatikana pekee katika mgahawa wa New Camegie Brewery's jijini Stockholm na July 2 itauzwa kwenye migahawa na kwenye matamasha yote nchini Sweden.
Source

Kiongozi wa kijeshi wa Mali ashinikiza kuondolewa vikwazo


Kiongozi wa kijeshi nchini Mali, Kanali Assimi Goita ametaka taifa lake kuondolewa vikwazo vya kiuchumi, ambavyo vimewekwa baada ya mapinduzi ya mwezi uliopita katika taifa hilo masikini la Sahel.

 Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Mali hapo jana, Goita amesema uteuzi wa hivi karibuni wa rais wa mpito raia, unamaanisha kwamba viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi lazima wasitishe marufuku yao ya kufanya biashara na Mali. 

Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi yenye mataifa15 wanachama ECOWAS mpaka wakati huu haijasema lolote lakini Ufaransa, ambayo ina vikosi vyake kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi nchini Mali, imeupokea vyema uteuzi wa waziri wa zamani wa ulinzi Bah Ndaw na viongozi wengine wa mpito kama hatua yenye kutia moyo. 

ECOWAS, iliifunga mipaka ya mataifa yake na Mali na kuweka vikwazo, baada ya jeshi la Mali Agosti 18, kumuondoa madarakani rais Boubacar Keita.

Majaliwa: Tarehe 28 Oktoba Siyo Siku Ya Mzaha

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amemaliza ziara yake mkoa wa Mara na kuwaeleza wananchi kwamba tarehe 28 Oktoba, 2020 siyo siku ya mzaha.

"Tarehe 28 Oktoba, 2020 siyo siyo ya mzaha na wala siyo siku ya majaribio. Ni siku ya kuchagua Kiongozi atakayetufaa, na huyo si mwingine bali Dkt. John Pombe Magufuli, " amesema.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumanne, Septemba 22, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Kibara, wilayani Bunda, mkoani Mara kwenye mkutano wa kuwanadi wagombea wa CCM uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Kibara.

Amesema kiongozi wa nchi anayefaa kuchaguliwa ni yule anayeweza kusimamia rasilmali za Taifa. "Ni yule anayeweza kusimamia tunu za Taifa... siyo mnapata kiongozi halafu akipewa nchi anabadilisha hadi wimbo wa Taifa."

"Tunahitaji kiongozi anayeweza kupambana na rushwa, awe mtu wa kutetea watu wake wapate haki bila kuombwa rushwa. Huyo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Magufuli," amesema. 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la kuwaombea kura Charles Kajege na diwani wa Kibara, Bw. Nyanguli Mtesigwa na madiwani wengine wa jimbo hilo. Jioni hii anaingia mkoa wa Mwanza.

Akielezea umuhimu wa chama kuwa na Ilani ya Uchaguzi, Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama cha Mapinduzi kimeandaa ilani yake yenye kurasa 303 ikisimamia yale yaliyokuwemo kwenye ilani iliyopita ambayo ilikuwa na kurasa 236 na mengine mengi mapya. 

"Watekelezaji wa hayo yote yaliyoainishwa kwenye Ilani ni hawa watatu ambao nawaombea kura leo. Namwombea kura Dkt. Magufuli ili akamilishe aliyoyaanza na atekeleze yaliyomo kwenye Ilani ya sasa. Ni lazima tumpatie mbunge na diwani wa CCM ili waweze kuzungumza lugha moja."

Kuhusu uboreshaji kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema zilitumika sh. bilioni 1.8 za kujenga hospitali ya wilaya hiyo na bado kuna sh. milioni 152 zilitolewa ili kuisaidia Halmashauri kujenga zahanati.

Kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 6.2 zimetumika kukarabati na ujenzi wa miradi mbalimbali kwenye Halmashauri ya wilayani Bunda, ikiwemo uchimbaji wa visima virefu na vifupi, utengenezaji wa matenki ya kuvuna maji na uchimbaji wa mabwawa. 
"Vijiji vilivyonufaika na miradi hii ni Nyatwali, Nyamuswa, Mgeta –Nyang'aranga, kinyabwiga, Bulamba na Kibara. Pia jumla ya shilingi milioni 90.1 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na usafishaji wa pampu za mkono 67 na visima vitatu," amesema.

Mapema asubuhi, akiwa kata ya Kisorya, Mheshimiwa Majaliwa aliwaeleza wananchi hao kwamba Serikali ya CCM ina mpango wa kuboresha kituo chao cha afya kwa kuongeza wodi tatu za wanawake, wanaume na watoto.

Pia alisema zimetengwa sh. milioni 550 za kuimarisha kituo hicho kwa kuongeza majengo ya jiko, chumba cha kufulia na chumba cha kuhifadhia maiti.

Kuhusu barabara, amesema kiasi cha sh. bilioni 2.9 kimetumika kutengeneza barabara za kuunganisha vijiji kwa vijiji, kukarabati sehemu korofi zilizoharibiwa na mafuriko, madaraja, makalvati na matengenezo ya kawaida.

Kuhusu umeme, amesema vijiji 77 kati ya 78 vina umeme isipokuwa kijiji kimoja tu cha Nafubu kilichopo kisiwani, ambacho amesema watapelekewa huduma ya umeme wa jua kwa vile siyo rahisi kupitisha nyaya za umeme majini.

(mwisho) 


Tuesday, September 22, 2020

AKINA MAMA MKOANI MWANZA WAPEWA ELIMU YA MTOTO


Wanawake wakinyonyesha watoto wao wakati wa mafunzo ya unyonyeshaji na makuzi kwa watoto wenye umri chini ya miezi sita yaliyoandaliwa na mradi wa USAID Tulonge afya katika  halmashauri ya Nyamagana jijini Mwanza jana.

****
Iwapo mama ataanza kumpatia vyakula mtoto ambaye hajafikisha miezi sita anaweza kumsababishia magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuharibu mfumo mzima wa makuzi yake hivyo ni vyema kuzingatia maelekezo na makuzi ya mtoto.

Pia, watoto wanapoumwa au kuonyesha dalili za kuumwa wazazi wanapaswa kuwakimbiza hospitalini badala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji ambao huweza kuharibu mfumo wa makuzi yao.

Hayo yamebainishwa na wataalaamu wakati wa kongamano la afya ya mama na mtoto lilioandaliwa na Mradi wa Usaid Tulonge Afya kwa ajili ya kuwapatia elimu makuzi ya watoto wanawake wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza jana.

Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Bertha Yohana alisema kumekuwapo na changamoto ya afya ya makuzi ya watoto kutokana na mila, tabia na desturi za jamii kushindwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.

"Tumekuwa na tabia kwenye jamii wanafundishana wao kwa wao, wapo wanaoamini kwamba mtoto akinyonya maziwa ya amma pekee hashibi, jambo hili sio kweli, mtoto anaweza kunyonya maziwa ya mama akashiba bila kula chakula kingine mpaka afikishe miezi sita," alisema

Alisema wakati mwanamke anapokuwa ananyonyesha mtoto mchanga anatakiwa asiwe na msongo wa mawazo, ale ashibe ili aweze kuzalisha maziwa ya kutosha.

Naye mhudumu ngazi ya jamii kata ya Mhandu, Rachael Mahulu alisema hakuna budi jamii ikaondokana na mila potofu za kuataka kuwalisha watoto wadogo vyakula na dawa kwa misingi ya kuwakuza kumbe kufanya hivyo wanawaharibu.

"mtoto akiota meno haya yanaitwa ya plstikli, wengi wnawakimbiza kwa waganaga na kuwapaka dawa kienyeji, kufanmya hivi ni kosa nenda hospitali utapewa mwongozo," alisema

Alisema iwapo mama akimnyonyesha mtoto wake mara kwa mara anamjengea uhusiano mzuri kati yake na yeye katika makuzi.

Naye Ofisa Uwanda (field officer), kutoka mradi wa USAID Tulonge afya wilaya ya Nyamgana, Esuphvat Lewis, alisema katika kongamano hilo wamefundisha tabia nne za kiafya katika makuzi ya mtoto ambayo ni pamoja na unyonyeshaji wa maziwa kwa kipindi cha miezi sita.

Zingine ni kuhakikisha mama analala na mtoto kwenye chandarua kimoja angalau mpaka afikishe miezi tisa, mama akiona dalili zozote hatarishi ampeleke mtoto hospitalini na njia za uzazi wa mpango baada ya mtoto kufikisha miezi 24.

Alisema katika mafunzo hayo jumla ya wanawke 50 wameshiriki kutoka kata za wilaya ya Nyamagana.

Nao baadhi ya wanawake walioshiriki mafunzo hayo, Tatu Ramadhani na Ester Suleiman kwa nyakati tofauti walisema mafunzo hayo yameweza kuwafungua na kutambua mambo muhimu katika makuzi ya mtoto ambayo walikuwa hawayajui awali..

"Nimejifunza unyonyeshaji wa mtoto na jinsi ya kumlinda na malaria, kiukweli kuna changmoto kubwa wanawake wengi wnashauriana kuwapa watoto uji hasa wa udaga kumbe unaweza kumsbaishia matatizo makubwa," alisema Tatu mkazi wa Igoma.

Mradi huu ambao unafahamika kama Mothers Meets Up events unafanyika kati ya wilaya 27 za Tanzania ambapo kupitia majukwaa ya watu wazima ya Naweza chini ya mradi wa Tulonge afya Tanzania kwa lengo la kuhamasisha huduma bora za afya kwa ngazi ya familia na jamii kwa kuondoa Mila pitiful na kuwapata mbinu za kiafya kujikinga na maradhi kama ukimwi , malaria, uzazi wa mpango na afya ya uzazi pamoja na ugonjwa wa kifua kikuu.
 Wanawake wakibeba watoto wao wakati wa mafunzo ya unyonyeshaji na makuzi kwa watoto wenye umri chini ya miezi sita yaliyoandaliwa na mradi wa USAID Tulonge afya katika  halmashauri ya Nyamagana jijini Mwanza jana.

 Wanawake wakicheza wakati wa mafunzo ya unyonyeshaji na makuzi kwa watoto wenye umri chini ya miezi sita yaliyoandaliwa na mradi wa USAID Tulonge afya katika  halmashauri ya Nyamagana jijini Mwanza jana. 


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...