Thursday, July 10, 2025

Kaganda awataka vijana kuwa walinzi wa mali za Serikali Babati



Na John Walter -Babati 

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Bi. Emmanuela Kaganda, amewataka wananchi hususan vijana kuhakikisha wanalinda na kutunza mali za Serikali, ikiwemo miundombinu ya barabara na madaraja, ili kuepusha uharibifu usio wa lazima.

Bi. Kaganda ametoa wito huo leo, tarehe 09 Julai 2025, wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa boksi kalavati kwenye barabara ya Mamire-Qash, katika kijiji cha Ngarenaro, kata ya Galapo, tarafa ya Babati.

Mradi huo unahusisha:

  • Ujenzi wa boksi kalavati moja kubwa,

  • Makalavati madogo matatu, na

  • Uwekaji wa changarawe katika urefu wa kilomita moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Mhandisi Naftali Lyatuu kutoka TARURA wilaya ya Babati, mradi huu unagharimu shilingi milioni 272,320,400, ambazo zote zimetolewa na Serikali Kuu.

Mradi huu unatarajiwa kuboresha mawasiliano na usafirishaji kati ya kata tatu muhimu za Galapo, Mamire na Endakiso, ambazo ni maeneo makuu ya kilimo.

Bi. Kaganda ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huu muhimu.

Kwa upande wao, viongozi wa vijiji pamoja na wananchi wamenufaika, wakiishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu hiyo, kwani awali kipindi cha mvua walikuwa wakikumbana na changamoto kubwa za usafiri.

Daraja hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 15 Julai 2025, wakati Mwenge wa Uhuru utakapo kimbizwa katika miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...