Wednesday, July 2, 2025

FAHAD AJITOSA UBUNGE SHINYANGA MJINI KUPITIA CCM: AVUNJA UKIMYA TETESI ZA ACT-WAZALENDO

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Fahad Gulamhafiz Mukadam akionesha fomu kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

 Mtoto wa mwanasiasa mkongwe na Meya mstaafu wa Manispaa ya Shinyanga, Mzee Gulamhafiz Mukadam, bwana Fahad Gulamhafiz Mukadam, ameibuka hadharani na kutangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza leo Julai 2, 2025 mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho, katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Fahad amesema ameamua kutumia haki yake ya kikatiba na ya msingi kama mwanachama wa CCM mwenye sifa stahiki, ili kuchangia maendeleo ya wananchi wa Shinyanga kupitia nafasi ya ubunge.

"Mimi ni mtoto wa Shinyanga. Nimechukua fomu kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi kugombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini. Kama ilivyo taratibu za chama chetu, kila mwenye sifa ana haki ya kugombea. Nimetumia haki yangu ya kikatiba na natamani kushirikiana na wana Shinyanga kuleta maendeleo," amesema Fahad.

Aidha, Fahad ameweka wazi kuwa amechukua hatua hiyo kama sehemu ya kutekeleza dhamira yake ya kweli ya kuwatumikia wananchi, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira ya wazi ya kisiasa nchini.
"Kupitia uongozi wa Rais Samia, kila mmoja ameruhusiwa kusema. Mengi yamesemwa kuhusu mimi, lakini leo nimeamua kuzungumza kwa vitendo. Nipo katika ofisi za CCM, chama chenye misingi, imani na miundo imara ya kuleta maendeleo kwa Watanzania," ameongeza.

Avunja Ukimya Kuhusu Tuhuma za ACT-Wazalendo

Fahad pia ametumia nafasi hiyo kukanusha vikali taarifa zilizoenea kwenye mitandao na midomo ya watu kwamba anapanga kugombea ubunge kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

"Wapo wanaosema nagombea kupitia ACT-Wazalendo. Pamoja na heshima kubwa niliyonayo kwa vyama vya upinzani, sijawahi kutamka wala kufikiria jambo hilo. Ni minong'ono tu ya watu, nami leo nimejibu kwa vitendo kwa kuchukua fomu kupitia CCM," amesema.

Tetesi hizo zilianza kusambaa kwenye duru za kisiasa zikidai kuwa maandalizi ya Fahad kugombea kupitia ACT-Wazalendo . 
Hata hivyo, kwa hatua ya kuchukua fomu ya CCM, mambo yamewekwa wazi.

Kwa kufanya uamuzi huo, Fahad Gulamhafiz Mukadam amejiunga na orodha ya makada kadhaa wa CCM waliokwisha tangaza nia ya kuwania ubunge Shinyanga Mjini, huku ushindani ukiendelea kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...