Wednesday, July 16, 2025

‎Mwenge wazindua daraja la watembea kwa miguu Tipri Mbulu. ‎


Na John Walter -Mbulu

Mradi wa ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu Tipri lililoko kata ya Gehandu, halmashauri ya mji wa Mbulu, umeleta afueni kubwa kwa wananchi takribani 3,995, wakiwemo wanafunzi ambao sasa wanaweza kuhudhuria masomo bila usumbufu wakati wote wa mwaka.

‎Akisoma taarifa ya mradi huo wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, Meneja wa TARURA wilayani Mbulu, Mhandisi Nuru Hondo, amesema kabla ya kujengwa kwa daraja hili, wanafunzi walikuwa wanakwamishwa na mvua kwa takribani miezi saba kila mwaka, jambo lililoathiri mahudhurio na maendeleo yao kielimu.

‎Ameeleza kuwa daraja hilo kutokana na uimara wake linaweza kudumu kwa miaka 70.

‎Mwenge wa Uhuru umepokelewa wilayani Mbulu kwa ziara ya kukagua, kutembelea, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali yenye thamani ya Shilingi bilioni 44, ikiwemo miradi ya afya, miundombinu ya barabara na miradi mingine ya maendeleo.

‎Miongoni mwa miradi hiyo ni daraja hili la Tipri, ambalo linaunganisha vijiji vya Tsawa na Tipri.

‎Kukosekana kwa daraja hilo kwa muda mrefu kulisababisha wananchi kupata changamoto kubwa katika kupata huduma muhimu, hasa wakati wa mvua ambapo mto huo ulikuwa unakuwa kikwazo kikubwa. Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 158.9.

‎Akizungumza kwenye eneo la mradi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, ameipongeza halmashauri ya mji wa Mbulu kwa ubunifu na utekelezaji wa mradi huu muhimu.

‎Vilevile, ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama kwa usimamizi mzuri wa fedha za mradi.

‎Mwenge wa Uhuru mwaka huu unaendelea na kaulimbiu isemayo: ‎"Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu."

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...