Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wengine nchini Kenya wametuma salamu zao za rambi rambi kwa familia ya marehemu Yusuf Haji.
Rais Uhuru Kenyatta ametuma salamu zake kwa familia na wakazi wa kaunti ya Garissa kwa ujumla kwa kumpoteza Seneta huyo Mohammed Yusuf Haji.
''Kifo cha Haji ni pigo kubwa kwa nchi hasa katika kipindi cha mabadiliko ya BBI ambapo mchango wake kama kiongozi utakosekana kwa kiwango kikubwa', amesema rais Uhuru Kenyatta.
Katika ujumbe wake, Rais Kenyatta amemuomboleza mwanasiasa huyo mkongwe ambaye hadi kifo chake alikuwa mwenyekiti wa Jopo la Maridhiano (BBI), kiongozi wa kujitegemea na mzalendo.
Viongozi wengine waliotuma salamu za rambirambi ni makamu Rais William Ruto ambaye amesema Kenya imepoteza kiongozi imara na kuongeza kuwa hayati ''Yusuf Haji alikuwa mwanasiasa aliyebarikiwa, mwenye mikakati na ujuzi wa kipekee katika kuleta maridhiano''.
Waziri wa Usalama wa ndani, Dkt Fred Matiangi amesema:
''Salamu zangu za rambi rambi ni kwa familia ya marehemu Seneta Yusuf Haji na wakazi wa Garissa. Alikuwa kiongozi wa muhimu mwenye hekima katika uongozi wake. Kama mwenyekiti wa Usalama wa Taifa, Ulinzi na uhusiano wa Nchi za Nje''.
Wengine waliotuma salamu zao za rambirambi ni pamoja na Waziri wa michezo Amina Mohamed, kiongozi wa walio wachache katika bunge la Seneti James Orengo, Spika wa Bunge la Taifa Justine Muturi, wabunge na watu mbalimbali nchini Kenya.