Thursday, July 10, 2025

CPA Mkama azindua mfuko wa uwekezaji wa iDollar awataka Watanzania kuchamkia fursa


Katika hatua ya kimkakati ya kuimarisha uwekezaji wa ndani na kuongeza mchango wa fedha za kigeni katika uchumi wa taifa, kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua rasmi Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja ujulikanao kama iDollar Collective Investment Scheme.

Mfuko huu utawawezesha Watanzania kuwekeza kwa kutumia sarafu za kigeni kama Dola za Marekani, Pauni za Uingereza, pamoja na sarafu nyingine za kimataifa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, alisema kuwa mafanikio haya ni matokeo ya mazingira bora ya kisera na kisheria yaliyowekwa na serikali kupitia CMSA kwa ajili ya kukuza sekta ya masoko ya mitaji nchini.

"Mfuko huu ni nyenzo muhimu ya kuhamasisha fedha za kigeni. Unachangia katika utulivu wa uchumi na kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na changamoto zinazohusiana na sarafu za kigeni. Pia unawawezesha Watanzania kuwekeza akiba zao za fedha za kigeni moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zao za benki," alisema CPA Mkama.

Aidha, aliongeza kuwa kwa kuzinduliwa kwa mfuko huu, Tanzania inajiunga na nchi nyingine za Afrika kama Kenya, Afrika Kusini, Mauritius na Ghana ambazo tayari zina mifumo kama hii. Aliwataka Watanzania, taasisi na kampuni mbalimbali kuchangamkia fursa hii ya kukuza uwekezaji kupitia sarafu za kigeni.


CPA Mkama alifafanua zaidi kuwa Mfuko wa iDollar ni miongoni mwa mifuko ya uwekezaji wa pamoja iliyosajiliwa na kuidhinishwa na CMSA, sambamba na ile inayoendeshwa na UTT AMIS. Alisisitiza kuwa mfuko huu pia utakuwa jukwaa la Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) kuwekeza mapato yao ya kigeni na kuchangia ukuaji wa uchumi wa ndani.

Kwa upande wake, Prof. Mohamed Warsame, Mkurugenzi Mtendaji wa iTrust Finance Limited, alisema kuwa lengo la mfuko wa iDollar ni kutoa suluhisho kwa Watanzania wengi ambao tayari wana akaunti za dola katika benki lakini wanakosa njia rasmi na yenye manufaa ya kuwekeza fedha hizo.

"Mfuko huu unawapa Watanzania fursa ya kuwekeza dola zao moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zao na kupata mapato katika dola. Tuliona umuhimu wa kuanzisha mfuko huu kufuatia mabadiliko ya kisheria yanayokataza matumizi ya sarafu za kigeni katika miamala ya ndani kama kulipa ada za shule, kodi au huduma nyingine," Prof. Warsame alieleza.

Aliongeza kuwa kufuatia agizo hilo la kisheria, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilielekeza kuwa sarafu za kigeni hazitakiwi tena kutumika katika miamala ya ndani, na hivyo mfuko huu unatoa njia mbadala ya uwekezaji kwa watu binafsi na taasisi zinazomiliki akiba ya fedha za kigeni.

Mfuko wa iDollar utasimamiwa na iTrust Finance Limited, taasisi iliyosajiliwa na kusimamiwa na CMSA, huku CRDB Bank ikihusika na kuhifadhi na kusimamia mali za mfuko huo kama mlezi (custodian).

Kwa uzinduzi huu, Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha ushirikishwaji mpana wa wananchi katika fursa za masoko ya mitaji na kuimarisha usimamizi wa fedha za kigeni kwa maendeleo endelevu ya taifa.






 

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...