Na John Walter -Hanang'
Katika juhudi za kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi, leo julai 11,2025 mkoa wa Manyara umezindua rasmi mpango maalum wa usambazaji wa nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu kupitia ruzuku ya serikali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika wilayani Hanang', Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewataka Wakuu wa wilaya zote tano za mkoa huo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha unafikia malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa mawakala wanaosambaza mitungi hiyo ya gesi wanapaswa kuwa waaminifu kwa kuuza kwa bei iliyoelekezwa na serikali.
Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Matumizi ya nishati safi kwa kizazi cha sasa na kijacho, ambao umeanza tangu mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2034, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Mratibu wa mradi huo, Abdulrazack Mkomi, serikali imetoa ruzuku kwenye mitungi ya gesi ya kilo sita, ambapo kila wilaya imepokea mitungi 3,255.
Wananchi wataweza kununua mtungi mmoja kwa shilingi 17,500 pekee, kwa sharti la kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Mradi huu una lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia, kulinda afya za wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na moshi wa mkaa na kuni, kuboresha uchumi wa kaya na pia kuhifadhi mazingira kutokana na kupungua kwa ukataji wa miti.
Kwa mujibu wa takwimu, jumla ya mitungi 16,275 itasambazwa kwenye wilaya zote tano za Mkoa wa Manyara, huku zaidi ya shilingi milioni 284.8 zikitumika kugharamia mradi huo.
Kwa hatua hii, serikali inatarajia kuona mabadiliko makubwa katika mtindo wa maisha ya wananchi, kupungua kwa uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa matumizi ya nishati salama na rafiki kwa mazingira.