ZIKIWA zimesalia siku 35 kuelekea uchaguzi mkuu wa urais nchini Marekani utakaofanyika Novemba 3 mwaka huu, wagombea urais, Donald John Trump wa chama cha Republican na mpinzani wake Joe Biden wa Chama cha Democratic, wamekabana koo kwa mara ya kwanza kwenye mdahalo uliowakutanisha katika jiji la Cleveland, Ohio, nchini humo.
Mdahalo huo ulioongozwa na mtangazaji wa Fox News, Chris Wallace, ulichukua dakika 90 hadi kumalizika.
Wagombea walikabiliana kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uchumi, uongozi, afya na janga la Corona huku kauli zisizo za kiungwana na za kibabe zikitawala wakati wa kujibu maswali
Aidha, kabla ya kuanza kwa mdahalo huo taarifa zilisambaa zikieleza kuwa Rais Trump alipanga kutompa mwanya mpinzani wake kuzungumza na kumkatisha kila atakapokuwa anaongea jambo ambalo kweli amelifanya.
Katika suala la afya, Biden ambaye ni makamu wa rais mstaafu wa Marekani amelaumu uongozi wa Trump kwa kudai idadi kubwa ya Wamarekani wanaugua magonjwa hatari kiafya
"Watu milioni 100 (Marekani) wanaugua magonjwa yanayowaweka katika hatari," alisema Biden.
Katika kujibu hoja hiyo Rais Trump alikanusha na kueleza idadi hiyo ilikuwa ni uongo huku akiwa hana jibu sahihi kuhusu idadi ya Wamarekani wenye matatizo ya afya.
Kwa mujibu wa idara ya afya nchini Marekani, kati ya watu milioni 50 na 129 ambao sio wazee tayari wamepata matatizo ya kiafya.
Mdahalo huo ulichukua sura mpya mara baada ya Trump anayesaka muhula wa pili kumwambia Biden "Watu wanaelewa kuwa miaka yako 47 ndani ya siasa hujafanya chochote wanaelewa," Trump alisema huku Biden akijibu na kusema " endelea kupiga kelele, utanyamaza tu" alisema mgombea huyo wa Democratic.
Katika kujadili suala la ugonjwa wa Corona ambao umesababisha vifo 205,942 nchini humo, Biden alimlaumu Trump kwa kusema "Watu wengi walikufa na wengine zaidi watakufa usipopata akili ya haraka kushughulikia," alisema Biden.
Trump aliyeongoza kwa kumkaripia mshindani wake pamoja na mwendeshaji wa mdahalo huo, Chris Wallace, alijibu na kusema, " watu wachache zaidi wanakufa sasa hivi, vilevile maambukizi yamepungua. Wewe kamwe usingeweza kufanya kazi ambayo sisi tumeifanya. Hicho kitu huna kwenye damu yako," hili lilikuwa jibu ya Trump kwa Biden.
Wagombea wote walionyesha kutofautiana takribani kwenye kila swali waliloulizwa na mwenyekiti wa mdahalo huo, kuanzia masuala ya afya, usalama, hadi ya kifamilia.
Sehemu kubwa ya mdahalo ilitawaliwa na Trump, ambaye wachambuzi wanasema alifanikiwa kuuendesha kwa njia yake mwenyewe, yaani badala ya kujadili masuala muhimu alikuwa anarusha maneno kama vile "Nyamaza kimya…hebu nyamaza wewe!!"
Kura za maoni zinamuonesha Biden akiongoza lakini Trump amesisitiza kauli yake ya kutokuwa na imani na mfumo wa upigaji kura kwa njia ya posta.
Pia amekataa kutamka kama atayakubali matokeo ya uchaguzi huo licha ya mshindani wake kusema yuko tayari kwa matokeo yoyote.