MBUNGE Mteule Viti Maalum kundi la Asasi za kiraia Tanzania  bara kwa tiketi ya CCM Neema Lugangira, amesema kuwa atakuwa  kiunganishi kati ya Asasi za kiraia(NGO'S), bunge, serikali, wafadhili  na chama ili kubadilishana mawazo katika kuleta maendeleo endelevu.
Neema ameyasema hayo wakati alipotembelea Mtandao wa  Vikundi vya wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) mkoani Morogoro ili kujua  changamoto zinazo wakabili na namna ya kuzitatua. 
Ameeleza kuwa kwa kuongea na wadau hao anapata fursa ya  kupata mambo ya kujadili yaliyomo kwenye ilani ya CCM yanayohusiana na  Asasi hizo na kuweza kubadilishana mawazo yatakayosaidia kwenye  utekelezaji.
Akizungumzia maeneo yaliyoguswa na ilani ya CCM amesema  lengo kubwa ni kuongeza tija katika kilimo ili kusaidia viwanda,  kuimarisha miundo mbinu na uzalishaji, kumsaidia mkulima kuzalisha na  kupata masoko, usimamizi wa mazao ya kimkakati, lishe na kuzijengea  uwezo Asasi za ndani.
Naye Mkurugenzi wa MVIWATA Stephen Ruvuga akitoa shukrani  zake kwa chama na serikali amesema kwa kitendo hicho cha kiongozi  kuwatembelea na kujua changamoto zao wanatarajia kuwepo kwa maelewano  mazuri kati ya serikali na Asasi hizo, hali itakayochochea maendeleo kwa  haraka.

