Mahusiano ya mwanaume na mwanamke hukutanisha watu kutoka koo mbalimbali. Kila mtu anakuwa amelelewa tofauti kwa wazazi wake. Tabia haziwezi kufanana. Huyu anaweza kuwa na tabia fulani ambayo mwenzake anakuwa hana. Mnapokutana wawili, ili muweze kwenda sawa ni lazima muelewane tabia, mshibane na kila mmoja amvumilie mwenzake. Hakuna binadamu aliyekamilika. Inawezekana kuna vitu ambavyo mwenzako anavyo, na pengine si vizuri. Suala la msingi ni kupata muda sahihi wa kumbadilisha mwenzako ili naye aweze kukubaliana na mabadiliko unayotaka kumpa, na mwisho wa siku mtakwenda sawa.
Unapomuelekeza mwenzako juu ya tabia fulani, unapaswa kutumia lugha rafiki; lugha ya mtu na mpenzi wake! Ambayo itamfanya asijisikie vibaya, akubaliane na kile kitu unachomueleza bila hata ya kuweka kipingamizi. Ukitumia lugha ya ukali, yenye kuonesha dharau na kuona anachokifanya ni cha kijinga, basi jua unakaribisha ugomvi. Utamfanya akuone unamdharau na mtu akishaona anadharaulika, hata kama kitu unachomueleza ni kizuri, anaweza kukipinga tu.
Inahitaji busara, hekima ya hali ya juu ili uweze kumkosoa mwenzi wako. Yawezekana kwa mazingira aliyolelewa, anachokifanya huamini ni sahihi lakini sasa amekuja kwako, mnaanzisha ulimwengu wenu, hivyo inahitajika akili ya ziada kuweza kumbadilisha. Tengeni muda mzuri wa kuelezana mambo mbalimbali ya kudumisha uhusiano wenu. Mzungumze na kusikilizana. Kila mmoja amueleze mwenzake kile anachoamini kinaweza kusaidia kustawi wa penzi lao, kwa kutumia lugha nzuri isiyokuwa na kebehi.
Mnapokuwa kwenye uhusiao, kwanza kila mmoja ajifunze namna ya kujipenda mwenyewe. Unapojua kujipenda mwenyewe na ukajua unahitaji nini ili kuipata furaha yako, basi ni rahisi sana kumtafutia mwenzako pia furaha unayoipata wewe. Usiwe na ubinafsi, furaha unayoipata wewe mpe na mwenzako. Unavyojijali, basi mjali na mwenzako. Kujipenda unavyojipenda basi kwa kiasi hichohicho mpende na mwenzi wako. Ukifanya hivyo, mwenzi wako naye hatakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kukurejeshea upendo.Related image
Jifunze kuwa na imani na mwenzako. Unapomjengea mwenzako imani, inamfanya wakati mwingine ashindwe kufanya maovu. Unapomuamini, unamfanya mwenzako ajiheshimu, maana anajua unamuamini na akifanya lolote la kijinga, lazima nafsi yake itamsuta. Muamini mwenzi wako. Mtengenezee mazingira ya kumuamini ili na yeye pia akuamini. Msiishi kwa kufuatiliana, maana maisha hayapo hivyo. Binadamu hawezi kuchungwa kama kondoo au mbuzi. Kubwa linalohitajika ni kujua thamani ya kuaminiana.
Anayekuamini anakujali, anayekujali atakulindia heshima. Hivyo, mkigundua hilo na mkaelekezana kiutu uzima, hakika mtaaminiana. Kila moja awe mkweli na mwaminifu. Ni ukweli pekee utakaowafanya muwe na furaha muda wote. Mkiwa waongowaongo, hamtadumu. Uongo una madhara. Ujanja ujanja ni tatizo katika uhusiano. Kuwa mwaminifu kwa mwenzako, naye pia awe mkweli na mwaminifu.
Kuweni nyinyi, tengenezeni maisha yenu. Msijilinganishe na mtu mwingine. Wekeni mikakati yenu na namna mnavyotaka kuishi, ishini maisha yenu. Mkiyafanya hayo yote, hakika penzi lenu litastawi na mtafurahia maisha ya uhusiano, uchumba na hata ndoa!