Sunday, October 12, 2025

Serikali yazindua mfumo wa kielektoniki ukaguzi wa vyombo vya Moto.


Na John Walter-Babati

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani amezindua mfumo mpya wa kielektroniki wa ukaguzi wa vyombo vya moto na utoaji wa stika za usalama barabarani, hatua inayolenga kuimarisha usalama na kupunguza ajali barabarani

Uzinduzi huo umefanyika katika Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mkoani Manyara Oktoba 11, 2025 ambapo mfumo huo unatarajiwa kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika ukaguzi wa magari kwa kutumia stika za karatasi, na badala yake kurahisisha huduma kwa njia ya Kidigitali.

Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Sillo amesema kuwa mfumo huo wa MIMIS ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayotekelezwa na Jeshi la Polisi kupitia Idara ya Mifumo ili kuhakikisha vyombo vyote vya moto vinakuwa salama kabla ya kutembea barabarani.

"Kupitia mfumo wa MIMIS, wamiliki wa Magari wataweza kuomba ukaguzi, kulipia na kupata stika zao za kielektroniki kwa urahisi zaidi. Hii ni hatua kubwa kuelekea matumizi ya Teknolojia katika kuhakikisha usalama wa wananchi barabarani." Amesema Sillo

Ameongeza kuwa Mfumo wa MIMIS utamuwezesha mmiliki wa chombo cha moto kuomba huduma hiyo akiwa popote, kisha kupeleka chombo chake kwa wakaguzi waliopo katika ofisi za Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa (RTOs) au Wilaya (DTOs) kwa tarehe na muda atakaochagua mwenyewe.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani SACP William Mkonda amebainisha kuwa elimu kuhusu matumizi ya mfumo huu mpya tayari imeanza kutolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na Askari wa kikosi cha Usalama barabarani 

"Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanauelewa mfumo huu na wanatumia fursa hii kuimarisha usalama wa vyombo vyao". Amesema SACP Mkonda

Uzinduzi wa mfumo wa MIMIS umekuja sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, ambayo hutoa nafasi ya kukumbushana umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani, kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, na kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto.

Friday, October 10, 2025

Mgombea wa CCM Mabibo atangaza neema rukuki


MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Mabibo, wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam,  kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ashura Mohammed  Seg'ondo, amewataka wananchi katika kata hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 mwaka huu kumpigia kura Mgombea  Urais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na yeye kwa nafasi ya udiwani  ili kuwaletea maendeleo ya haraka.

Aidha amewataka kumchagua Mgombea Ubunge  kwa tiketi ya CCM  katikaJimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo  hali itakayo harakisha maendeleo katika kata hiyo.

 Akihutubia mkutano wa kampeni  katika kata hiyo,  Ashura alisema akichaguliwa  kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha  anasimamia kikamilifu  ujenzi wa miundo mbinu.

"Miundombinu nimeigawanya katika sehemu  mbili. Barabara kuu na barabara za ndani. Katika Mtaa wa Jitegemee  mkandarasi  tayari  anaendelea na ujenzi wa Barabara ya Binti Kayenga. Nami kwa kushirikiana na nyie nitahakikisha kwa ujasiri wangu mkubwa kwa nguvu zangu zote mkandarasi afanye kazi kwa haraka kukamilisha ujenzi,"ameeleza  Ashura.

 Amebainisha,   Kata ya Mabibo, imejaaliwa viwanda  vikubwa hivyo  kwa kushirikiana na viongozi atahakikisha  kwa asilimia kubwa  wakazi wa kata hiyo watananufaika na  ajira.

"Pia katika sekta ya michezo nitahakikisha  tunashirikiana vyema  ili iwe fursa ya ajira kwa sababu Kata ya Mabibo ni  ni kitovu cha mchezo wa  ngumi.  Bondia Mfaume Mfaume anatoka katika   kata hiii,"ameeleza.

Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri , Ashura ameeleza atahakikisha inawasikia walengwa.

"Mikopo inakuja lakini haiwanufaishi walengwa. Nikichaguliwa nitahakikisha mikopo hii inawafikia walengwa. Inawanufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kausha damu itakuwa baibai,"ameeleza mgombea huyo.

Amesema atafanya jitihada kuleta walimu wa vikoba kutoa elimu  kwa wananchi katika kata hiyo ili viinue uchumi hasa wawanawake.






Friday, October 3, 2025

TAMASHA LA SIKU YA WANA 'STAND UNITED" NI KESHO JUMAMOSI CCM KAMBARAGE



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro ambaye ni mlezi wa Timu ya Stand United akizungumza na waandishi wa habari.

Na Marco Maduhu,SHINYANGA


WANANCHI na mashabiki wa soka mkoani Shinyanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi kesho, kushuhudia Tamasha la Siku ya Wana, litakalofanyika Uwanja wa CCM Kambarage, ambapo kutakuwa na utambulisho wa wachezaji wapya wa Timu ya Stand United watakaoshiriki Ligi ya Championship msimu huu.


Wito huo umetolewa leo Oktoba 3,2025 na Mlezi wa Timu ya Stand United Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea kwenye Tamasha hilo hapo kesho,ambalo litafanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage.
"Natoa wito kwa wananchi wa Shinyanga na wapenzi wote wa soko wajitokeze kwa wingi hapo kesho kwenye Tamasha la siku ya wana ili kutoa Motisha kwa Timu yao ya Stand United, na kuishuhudia ikishuka dimbani dhidi ya Timu ya Pamba Jijiji katika mchezo wao wa kirafiki,"amesema Mtatiro.


Aidha,amesema katika msimu uliopita wa Ligi ya Champioship,ambapo Timu hiyo ili cheza Playoff ili kufuzu kushiriki Ligi kuu, kwamba wamejifunza mengi na msimu huu wa Championship timu ambazo watakutananazo ni kichapo tu sababu wamejipanga vizuri.
Msemaji wa Timu ya Stand United Ramadhan Zorro,amesema wamefanya usajiri mzuri na wachezaji wao wana viwango bora kabisa na kwamba kwa uwezo walio nao lazima watarejea kucheza Ligi kuu.


Amesema katika mchezo wao kesho dhidi ya Pamba Jijiji kwenye Tamasha hilo, wataonyesha uwezo wa wachezaji wao huku akiionya Pamba ijiandae kubeba mzigo wa magoli sababu wapo kamili.
Naye Msemaji wa Timu ya Pamba Jijiji Moses William,wamesema Timu ya Stand United ni nzuri na kwamba wamejipanga vyema kupata ushindi kwenye Tamasha hilo na hawatakuwa na mzaha.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tamasha hilo Chripin Kakwaya,amesema maandalizi ya Tamasha hilo yanaendelea vizuri, na kwamba wakati wa Tamasha hilo kutakuwa na burudani mbalimbali ambapo wataanza na Jonging kilomita 5,Mbio za Baiskeli na Burudani kutoka wa Wasanii.
Amesema, pia kutakuwa na michezo ya utangulizi kati ya timu ya Bajaji na Bodaboda, Soko Kuu na Soko la Majengo pamoja na Dabi ya Upongoji FC na Ibinzamata, na baada ya hapo Timu ya Stand United itashuka dimbani dhidi ya Pamba Jiji.


Ameongeza katika Tamasha hilo kutakuwa na viingilio ambapo mzunguko sh.3,000,VIP Sh.5000 na VVIP sh.10,000.


TAZAMA PICHA👇👇


Mwenyekiti wa Tamasha la siku ya wana Chripin Kakwaya akizungumza na waandishi wa habari.
Msemaji wa Timu ya Stand United Ramadhan Zorro akizungumza na waandishi wa habari.
Msemaji wa Timu ya Pamba Jijiji Moses William akizungumzia mchezo wao wa kesho dhidi ya Stand United.
Msemaji wa Timu ya Pamba Jijiji Moses William(kushoto)wakipongezana na Msemaji wa Timu ya Stand United Ramadhan Zorro.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...