Na John Walter-Babati
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani amezindua mfumo mpya wa kielektroniki wa ukaguzi wa vyombo vya moto na utoaji wa stika za usalama barabarani, hatua inayolenga kuimarisha usalama na kupunguza ajali barabarani
Uzinduzi huo umefanyika katika Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mkoani Manyara Oktoba 11, 2025 ambapo mfumo huo unatarajiwa kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika ukaguzi wa magari kwa kutumia stika za karatasi, na badala yake kurahisisha huduma kwa njia ya Kidigitali.
Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Sillo amesema kuwa mfumo huo wa MIMIS ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayotekelezwa na Jeshi la Polisi kupitia Idara ya Mifumo ili kuhakikisha vyombo vyote vya moto vinakuwa salama kabla ya kutembea barabarani.
"Kupitia mfumo wa MIMIS, wamiliki wa Magari wataweza kuomba ukaguzi, kulipia na kupata stika zao za kielektroniki kwa urahisi zaidi. Hii ni hatua kubwa kuelekea matumizi ya Teknolojia katika kuhakikisha usalama wa wananchi barabarani." Amesema Sillo
Ameongeza kuwa Mfumo wa MIMIS utamuwezesha mmiliki wa chombo cha moto kuomba huduma hiyo akiwa popote, kisha kupeleka chombo chake kwa wakaguzi waliopo katika ofisi za Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa (RTOs) au Wilaya (DTOs) kwa tarehe na muda atakaochagua mwenyewe.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani SACP William Mkonda amebainisha kuwa elimu kuhusu matumizi ya mfumo huu mpya tayari imeanza kutolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na Askari wa kikosi cha Usalama barabarani
"Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanauelewa mfumo huu na wanatumia fursa hii kuimarisha usalama wa vyombo vyao". Amesema SACP Mkonda
Uzinduzi wa mfumo wa MIMIS umekuja sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, ambayo hutoa nafasi ya kukumbushana umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani, kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, na kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto.