Mzee Omary Said ameamua kujikita katika kilimo wilayani Rufiji mkoani Pwani, baada ya kuondolewa kazini miaka miwili iliyopita kwa sababu ya kuwa na elimu ya darasa la saba.
Saidi alikuwa akifanya kazi kama kibarua katika bandari ya Dar es Salaam tangu mwaka 1994, ilipofika mwaka 2007 aliajiriwa rasmi katika bandari hiyo na kufanya kazi mpaka mwaka 2018 alipoondolewa kwa kukosa sifa.
Alikuwa amebakisha miaka miwili astaafu kazi yake kama msimamizi katika shughuli ya kushusha mizigo kwenye meli (foreman), hivyo amepoteza mafao yake ambayo angepata baada ya kustaafu.
"Lazima maisha yaendelee, ukikosa plani A, unatafuta plan B. Ndiyo maana nimejikita kwenye kilimo ili niendelee kuihudumia familia yangu," anasema Said.
Said anasimulia jinsi alivyoanza kazi katika bandari hiyo kwamba alianza kama kibarua wa kupakia na kupakua mizigo na kwamba kadri siku zilivyozidi kwenda, Mamlaka ya Bandari nchni (TPA) ilianza kuwapatia mikataba ya muda mfupi; miezi mitatu, sita mpaka mwaka.
Anasema mwaka 2007, alifanikiwa kupata ajira ya kudumu katika bandari hiyo na wakati huo hakuwahi kusikia chochote kuhusu waraka wa ajira wa mwaka 2004 ambao unataka watumishi wa umma kuajiriwa kwa elimu ya kidato cha nne.
Mkulima huyo anasema makosa yalifanywa na viongozi waliopita kwa kuwaajiri wakati wakijua hawakuwa na sifa, hivyo anaiomba Serikali iwapatie stahiki zao kwa sababu walijitoa kwa muda mrefu kufanya kazi katika bandari hiyo.
"Tumekubali kuondoka, lakini tunaiomba Serikali itusaidie tupate stahiki zetu. Tuna haki zetu ambazo tuliziacha, tunastahili kulipwa," anasema Said na kuongeza kuwa Serikali iwahurumie kama watoto wake.
Anasisitiza kwamba kuwa darasa la saba haina maana kwamba hawana akili, wanaweza kuwa na akili pengine kuliko hata waliosoma mpaka sekondari.
Anasema waliokuwa darasa la saba wengi walipatiwa mafunzo mbalimbali kama vile ushonaji na udereva wa winch na focal.
"Katika hili kundi la walioishia darasa la saba, tupo sisi pia ambao tulifika kidato cha nne lakini hatuna cheti, yaani wale form four failure kabisa," anasema mzee huyo na kusisitiza kwamba maslahi yao yazingatiwe.
Kilio cha Said kinawakilisha waliokuwa wafanyakazi wa bandari zaidi ya 100 ambao walipunguzwa kazini kwa sababu wana vyeti vya darasa la saba, jambo ambalo ni kinyume na waraka wa ajira wa mwaka 2004.
Wafanyakazi hao wameshusha kilio chao kwa Rais John Magufuli wakitaka awaonee huruma na kuwalipa stahiki zao baada ya kuondolewa kazini mwaka 2018 kwa sababu wana elimu ya darasa saba.
Akizungumza na gazeti hili, kiongozi wa wafanyakazi hao, Fahki Athuman alisema wamekwenda kwa viongozi mbalimbali wa Serikali kutaka kupatiwa msaada ili wapate stahiki zao, hata hivyo, hawajapata msaada wowote.
"Suala hili bado liko Mahakamani, lakini sisi tunaamini kwamba tunaweza kulimaliza kwa mazungumzo na Serikali, ndiyo maana tumekwenda kwa Katibu mkuu wa Utumishi, tumekwenda Dodoma kwa Spika wa Bunge, tumekwenda kwa Waziri Mkuu mpaka Ikulu.
"Pamoja na jitihada hizo za kutafuta suluhisho, jambo letu limekwama. Tunamuomba Rais Magufuli asikie kilio chetu, tunahangaika sana tangu tuondolewe kazini, hatukulipwa chochote, wenzetu wengine walikuwa wanakaribia kustaafu," alisema Athuman.
Kiongozi huyo alibainisha kwamba kwa sasa wanachotaka ni kulipwa stahiki zao kwa sababu wamefanya kazi kwa muda mrefu katika bandari hiyo kama vibarua na baadaye wakaajiriwa rasmi kwa elimu hiyo hiyo waliyonayo. "Sisi hatukuwa na vyeti feki, tuna vyeti vya darasa la saba na tulikuwa tunafanya kazi za kubeba mizigo, wengine walipata mafunzo katika Chuo cha Bandari wakaanza kuendesha mitambo. Tunataka tupewe stahiki zetu," alisema.
Mwathirika mwingine katika kundi hilo, Kassimu Mnyani alisema waraka wa mwaka 2004 unaoelekeza ajira kutolewa kwa wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne haukuwafikia, lakini wanashangaa kwanini waliajiriwa wakati kulikuwa na waraka huo.
Alisema baada ya kufanya kazi kama kibarua kwa muda mrefu, mamlaka ya bandari ilitaka kuajiri watu kwa sharti la kuwa na ujuzi. Alisema baadhi ya watu walijiendeleza kwa kupata ujuzi tofauti, ndipo wakaajiriwa.
"TPA ilikuwa inaajiri kwa kuzingatia mahitaji yake yenyewe na huo waraka wa ajira wa mwaka 2004 haukuwahi kutufikia, tusingeweza kuajiriwa," alisema Mnyani na kusisitiza kwamba wanaomba Rais Magufuli awasaidie.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Deusdedit Kakoko alisema wafanyakazi hao waliondolewa kihalali kwa kufuata sheria kama ilivyokuwa kwa wafanyakazi katika taasisi nyingine za umma.
Alisema anashangaa kuona wafanyakazi hao wa zamani wakiendelea kulalamika kila siku, wakati wenzao wa maeneo mengine wamekubaliana na hali na hawazunguki kila kona kulalamika kwamba wameonewa.
"Sheria inapopitishwa, lazima wote tuiheshimu. Sheria ya ajira ya mwaka 2004 inaelekeza kwamba Serikali haitaajiri mtu wa kiwango cha elimu chini ya kidato cha nne, sasa sheria ikisema hivyo walitaka sisi tufanyaje?" alihoji Kakoko.
Kuhusu waliokuwa na elimu ya darasa la saba kabla ya mwaka 2004, Kakoko alisema hao hawakuguswa na mpaka sasa wapo wanaendelea na kazi zao na kusisitiza kwamba walioondolewa ni wale walioajiriwa baada ya mwaka 2004.
"Kama wangekuwa wameajiriwa kabla ya mwaka 2004 malalamiko yao yangekuwa sawa, lakini hao ni baada ya mwaka 2004, wamekwenda mpaka Ikulu lakini walirudishwa, hawana hoja," alisema Kakoko.
Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba wapo wengine katika kundi hilo waliondolewa kwa kuwa cheti feki cha kidato cha nne, baada ya kuona wameguswa wakatoa cheti hicho na kubaki na cheti cha darasa la saba kisha wanalalamika kuonewa.
Alipotafutwa Katibu mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Meli na Bandari Tanzania (Dowuta), Jonathan Msoma kuzungumzia suala hilo, hakutaka kuzungumza lakini akaelekeza suala hilo kwa kiongozi wa wafanyakazi hao.