Monday, November 10, 2025

BODABODA WENYE PIKIPIKI ZA MKATABA WALIA NA GHASIA ZA OKTOBA 29



Na Mwandishi wetu, Dodoma

Baadhi ya waendesha bodaboda jijini Dar es Salaam wameeleza kuathiriwa kiuchumi na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, zikisema matokeo ya tukio hilo yamewafanya wengi wao kuingia kwenye madeni makubwa kutokana na kusimama kwa shughuli zao za kila siku.

Akizungumza na Central, Bwana Issa Salala, dereva wa bodaboda anayefanya kazi kwa kutumia pikipiki ya mkataba, amesema vurugu hizo zilitokea wakati ambapo hakuwa na akiba yoyote, jambo lililosababisha kushindwa kulipa kodi ya pikipiki aliyokuwa akiitumia kwa kazi ya kila siku.

"Nililazimika kukaa ndani kwa zaidi ya siku tano bila kutoka kazini. Nilikosa fedha za kulipia pikipiki, na mwenye pikipiki aliendelea kudai hela zake. Ilikuwa kipindi kigumu sana," amesema Salala kwa uchungu.


Aidha, ameeleza kuwa hali hiyo ilichangia mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa, ambapo unga uliokuwa ukiuzwa shilingi 1,500 kwa kilo uliuzwa hadi shilingi 4,000, huku mchele ukipanda kutoka shilingi 2,000 hadi zaidi ya shilingi 5,000 kwa kilo moja.

Salala amesema changamoto hiyo imeonyesha namna vurugu na maandamano yasiyo na mpangilio mzuri yanavyoweza kuathiri maisha ya wananchi wa kipato cha chini, hasa vijana wanaojitafutia kipato kupitia sekta ya usafirishaji wa bodaboda.

"Ni muhimu vijana kufikiria mbele kabla ya kuchukua hatua. Wengi walioingia mitaani hawakujua madhara ya baadae. Tumeumia sisi na familia zetu. Tumepata hasara kubwa na hata hali zetu za kiafya zimebadilika," amesisitiza.

Wakati huo huo, wadau mbalimbali wa usafirishaji wameendelea kutoa wito kwa vijana nchini kujiepusha na matukio ya vurugu na badala yake kutumia muda na nguvu zao katika shughuli za kiuchumi zinazochangia ustawi wao binafsi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.




Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...