Mkuu wa polisi nchini Ujerumani Dieter Romann amezishutumu kampuni za ndege kwa kushindwa kuzingatia sheria za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona .
Katika mahaojiano na gazeti la Ujerumani la Bild am Sonntag yaliyochapishwa leo, Romann amesema katika muda wa siku sita zilizopita, polisi nchini humo wamegundua karibu matukio 600 ambapo kampuni za ndege zimekiuka masharti ya kupambana na COVID-19.
Ameongeza kuwa abiria kutoka maeneo yalio na viwango vya juu vya maambukizi ya virusi hivyo ama yale ambayo aina mpya ya virusi hivyo imegunduliwa, wameingia nchini Ujerumani bila ya kusajiliwa kidigitali ama kuonesha vyeti vya ushahidi wa kutokuwa na maambukizi ya virusi hivyo jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Romann amesema kuwa kampuni za ndege sasa zinakabiliwa na hatari ya kutozwa faini kutoka kwa mamlaka ya afya ya dola takriban elfu 30 kwa ukiukaji huo wa kanuni.