Tuesday, April 14, 2026

Picha : CHEREHANI AFANYA MKUTANO MKUBWA WA SHUKRANI USHETU, DARAJA LA MWABOMBA 99% ...MABALA ASEMA 'NI MBUNGE WA VITENDO!

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mwabomba Kata ya Idahina Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga - Picha na Kadama Malunde
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani akikaribishwa katika kijiji cha Mwabomba kata ya Idahina Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani amefanya ziara muhimu ya kukagua na kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Idahina, Halmashauri ya Ushetu, sambamba na kufanya mkutano mkubwa wa shukrani kwa wananchi waliomchagua kuwa mbunge wao.

Katika ziara hiyo iliyofanyika leo Jumatatu Aprili 13, 2026 Mhe. Cherehani ametembelea Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Mwabomba uliokamilika kwa asilimia 99 na tayari kuanza kutumika, pamoja na kuzindua rasmi ujenzi wa Kituo cha Afya Mwabomba (Idahina), hatua inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mwabomba, Mhe. Cherehani ametoa shukrani zake kwa wananchi pamoja na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi kwa uaminifu.
“Leo Aprili 13, 2026 ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima sote wananchi wa Ushetu. Nimekuja kusherehekea nanyi na kusema neno moja tu  ‘Asante’. Asanteni sana kwa kunichagua kuwa Mbunge wenu na kwa kumchagua Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais na madiwani wa CCM” amesema Cherehani.

Mbunge huyo ameeleza kuwa serikali imetoa shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mwabomba, ambalo sasa limeanza kuwahudumia wananchi bila hofu, huku akitangaza kukabidhi shilingi milioni 657 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Idahina.

“Nimekuja kuwakabidhi kiasi cha shilingi milioni 657 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na wananchi wasichangishwe hata shilingi mia. Tayari milioni 250 zipo kwenye akaunti, nataka ujenzi uanze mara moja ili wananchi waanze kupata huduma,” amesisitiza.

Aidha, ametoa maagizo kwa watendaji wa sekta ya afya kuhakikisha huduma kwa wajawazito zinatolewa bila malipo, akipiga marufuku vitendo vya kuwatoza fedha.

“Ni marufuku kumtoza hata shilingi 10 mama mjamzito. Wapokeeni, wapimeni na wahudumieni. Hawa ni wananchi wa kawaida, wanashinda mashambani ,wanatoa wapi fedha?” amehoji.
Mbali na afya, Mhe. Cherehani amezungumzia mipango ya maendeleo ikiwemo upatikanaji wa maji kupitia mradi wa Ziwa Victoria, ufunguzi wa soko la dhahabu Mwabomba na utatuzi wa changamoto za wafugaji kupata maeneo ya malisho.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa aliyekuwa mgeni rasmi amempongeza Mhe. Cherehani kwa kusimamia kwa vitendo miradi ya maendeleo.
“Ushetu mna mbunge mchapakazi, mmelamba dume sana, ni mbunge wa Vitendo, Cherehani inashona maendeleo kweli kweli Ushetu. Ni vigumu kupata kiongozi mwenye upendo na jitihada kama hizi. Daraja la Mwabomba sasa linapitika, wananchi wanavuka bila hofu,” amesema Mlolwa.

Ameongeza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na maono ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, huku akihimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, mshikamano na kuunga mkono serikali yao ili kuharakisha maendeleo zaidi.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na kudumisha amani, akibainisha kuwa maendeleo yanayoonekana ni matokeo ya sera na utekelezaji wa CCM chini ya uongozi wa Rais Samia.

Mradi wa Daraja la Mwabomba kwenye barabara ya Masumbwe–Mwabomba unaounganisha mikoa ya Shinyanga na Geita, umetekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na mkandarasi M/s Jossam & Co. Ltd, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kufuatia uharibifu wa miundombinu uliotokea hapo awali.
@malundeblog

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani amefanya mkutano mkubwa wa kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa Mbunge. Akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mabala Mlolwa, Mbunge Cherehani amesherehekea Siku ya Kuzaliwa na Wananchi wa Kijiji cha Mwabomba kata ya Idahina. Hali kadhalika amekagua daraja la Mwabomba ambalo limekamilika kwa asilimia 99 pamoja na kukabidhi fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mwabomba! Tazama hivi Vibe!!

♬ original sound - Malunde

Monday, April 13, 2026

SEKTA YA VIWANDA YASHIRIKIANA NA VETA, ENABEL KUANDAA WATAALAMU


Ushirikiano kati ya VETA, Enabel na kiwanda cha Kasulu Sugar umeanza kuzaa matunda baada ya vijana 36 waliokuwa wakifanya kazi bila vyeti kutathminiwa na kupatiwa vyeti kupitia mfumo wa urasimishaji wa ujuzi (RPL).

Meneja Rasilimali Watu wa Kasulu Sugar, Samweli George Aoram, amesema hayo wakati Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alipotembelea kiwanda hicho Aprili 9 hadi 10, 2026.

Amesema hatua hiyo imechangiwa na ushirikiano thabiti baina ya taasisi hizo, akibainisha kuwa pia wanafunzi 20 kutoka VETA Kasulu wanaendelea na mafunzo kwa vitendo kiwandani hapo huku wakichangia uzalishaji.

Aoram amesema kampuni iko tayari kuendeleza ushirikiano huo ili kupata wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya kazi.

Naye Meneja wa Mradi wa Wezesha Binti kutoka taasisi ya Enabel, Christine Karungi, amesema lengo ni kuelewa mahitaji ya waajiri ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanatatua changamoto za ajira kwa vijana.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na viwanda ni nguzo muhimu katika kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.

Amesema ziara hiyo imelenga kujionea mahitaji ya ujuzi viwandani na kuimarisha ushirikiano utakaosaidia kuboresha mitaala ya mafunzo ili iendane na mazingira ya kazi.

Amefafanua kuwa kupitia ushirikiano huo, VETA inalenga kuandaa mitaala inayozingatia mahitaji ya waajiri pamoja na kuongeza fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.

“Ushirikiano wa karibu na viwanda utatusaidia kuandaa wahitimu watakaoanza kazi moja kwa moja bila kuhitaji mafunzo ya ziada,” amesema.

Aidha, amesema hatua hiyo inawajengea uwezo wakufunzi kwa kuwapatia uzoefu wa teknolojia za kisasa viwandani, hali inayoongeza ufanisi wao wanaporejea kufundisha.

TANESCO Hanang Yapokea Gari Jipya la Kisasa Kuimarisha Huduma za Umeme





Na John Walter -Hanang'

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara limepokea gari jipya aina ya Isuzu FRR lenye mitambo ya kisasa kwa ajili ya kuboresha huduma za umeme wilayani humo.

Gari hilo limekabidhiwa leo rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almish Hazal, katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za TANESCO Hanang’.

 Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Hazal amesema gari hilo lina uwezo mkubwa wa kubeba vifaa vizito, kubadilisha nguzo pamoja na transfoma kwa urahisi, hivyo litasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.

Hazal amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mafanikio ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za umeme, akieleza kuwa vijiji vyote 96 vya Wilaya ya Hanang’ tayari vimepata umeme, na sasa juhudi zinaelekezwa kwenye vitongoji 116 vilivyopo katika kata 33 za wilaya hiyo.

“Gari hili litasaidia sana utendaji kazi wa TANESCO, hasa kuwafikia wananchi kwa haraka pale changamoto za umeme zinapotokea,” amesema Hazal.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Hanang’, Mhandisi Mwitondi Charles Rugembe, amesema kabla ya kupatikana kwa gari hilo walilazimika kukodi gari kwa gharama kubwa, hali iliyoongeza matumizi yasiyo ya lazima.

“Awali tulikuwa tunakodi gari na kutumia gharama kubwa, lakini sasa serikali imeokoa fedha hizo kupitia upatikanaji wa gari hili jipya,” amesema Rugembe.

Ameongeza kuwa gari hilo litasaidia kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, kwani sasa wataalamu wataweza kufika kwa wakati kwenye maeneo yenye hitilafu na kufanya matengenezo haraka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Hanang’, Asia Halamga, amesema kuwa TANESCO wilayani humo tayari imepata gari la kutembelea pamoja na gari hilo jipya la kazi nzito, jambo linaloonesha dhamira ya serikali katika kuboresha miundombinu ya huduma za umeme.

Asia amewataka wananchi kuendelea kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kupeleka miradi zaidi ya maendeleo katika Wilaya ya Hanang’.


Saturday, April 11, 2026

BAYI: AMANI NDIO MUHIMILI WA MAFANIKIO KATIKA MICHEZO

 

Amani na michezo vimetajwa kuwa ni vitu vyenye uhusiano wa karibu, ambapo kila kimoja kinakiimarisha kingine katika kujenga jamii na taifa imara.

 Michezo hustawi zaidi katika mazingira yenye utulivu, huku ikiwa ni chombo muhimu cha kukuza umoja, mshikamano wa kijamii, na maelewano miongoni mwa watu wenye asili na tamaduni tofauti. 

Kupitia michezo, jamii hujenga jukwaa la pamoja lenye ushindani unaoambatana na heshima, nidhamu, na urafiki, hali inayopunguza hofu na kuongeza kuaminiana.

Mmoja wa wanamichezo mashuhuri na sauti yenye heshima duniani katika riadha, Filbert Bayi, anaamini kuwa amani na michezo haviwezi kutenganishwa. 

Katika mahojiano maalum, Bayi ambaye amewahi kushikilia rekodi ya dunia, alibainisha kuwa hakuna nchi inayoweza kukuza vipaji vya michezo bila kuwepo kwa amani na utulivu. Alisisitiza kuwa michezo si burudani pekee, bali ni chanzo kikubwa cha ajira, huduma za kijamii, na undugu miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali.

Bayi alieleza kuwa amani huweka mazingira rafiki kwa wanamichezo kufanya mazoezi na kuonesha vipaji vyao bila hofu ya usalama. 

Alitolea mfano Tanzania kama kioo cha namna amani inavyochochea maendeleo ya michezo, kwani wanamichezo wana nafasi ya kushindana katika hali ya utulivu. Aliongeza kuwa katika ngazi ya kimataifa, michezo imekuwa ikitumika kupunguza uhasama kati ya mataifa yaliyowahi kuwa kwenye migogoro, akitolea mfano wa mataifa hayo kutembea pamoja wakati wa ufunguzi wa michezo mikubwa.

Mbali na hayo, Bayi alikumbusha tukio la kihistoria la kususia michezo ya Olimpiki ya mwaka 1976 kupinga ubaguzi wa rangi kama ujumbe wa kusisitiza haki, usawa, na amani. Alihitimisha kwa kutoa rai kwa serikali, vyombo vya michezo, na jamii kwa ujumla kuendelea kuwekeza katika michezo kama njia ya kukuza amani, hasa kwa vijana. Alisisitiza kuwa kudumisha amani na umoja ndiyo siri ya kujenga Tanzania imara na yenye ustawi kwa vizazi vijavyo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...