Amani na michezo vimetajwa kuwa ni vitu vyenye uhusiano wa karibu, ambapo kila kimoja kinakiimarisha kingine katika kujenga jamii na taifa imara.
Michezo hustawi zaidi katika mazingira yenye utulivu, huku ikiwa ni chombo muhimu cha kukuza umoja, mshikamano wa kijamii, na maelewano miongoni mwa watu wenye asili na tamaduni tofauti.
Kupitia michezo, jamii hujenga jukwaa la pamoja lenye ushindani unaoambatana na heshima, nidhamu, na urafiki, hali inayopunguza hofu na kuongeza kuaminiana.
Mmoja wa wanamichezo mashuhuri na sauti yenye heshima duniani katika riadha, Filbert Bayi, anaamini kuwa amani na michezo haviwezi kutenganishwa.
Katika mahojiano maalum, Bayi ambaye amewahi kushikilia rekodi ya dunia, alibainisha kuwa hakuna nchi inayoweza kukuza vipaji vya michezo bila kuwepo kwa amani na utulivu. Alisisitiza kuwa michezo si burudani pekee, bali ni chanzo kikubwa cha ajira, huduma za kijamii, na undugu miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali.
Bayi alieleza kuwa amani huweka mazingira rafiki kwa wanamichezo kufanya mazoezi na kuonesha vipaji vyao bila hofu ya usalama.
Alitolea mfano Tanzania kama kioo cha namna amani inavyochochea maendeleo ya michezo, kwani wanamichezo wana nafasi ya kushindana katika hali ya utulivu. Aliongeza kuwa katika ngazi ya kimataifa, michezo imekuwa ikitumika kupunguza uhasama kati ya mataifa yaliyowahi kuwa kwenye migogoro, akitolea mfano wa mataifa hayo kutembea pamoja wakati wa ufunguzi wa michezo mikubwa.
Mbali na hayo, Bayi alikumbusha tukio la kihistoria la kususia michezo ya Olimpiki ya mwaka 1976 kupinga ubaguzi wa rangi kama ujumbe wa kusisitiza haki, usawa, na amani. Alihitimisha kwa kutoa rai kwa serikali, vyombo vya michezo, na jamii kwa ujumla kuendelea kuwekeza katika michezo kama njia ya kukuza amani, hasa kwa vijana. Alisisitiza kuwa kudumisha amani na umoja ndiyo siri ya kujenga Tanzania imara na yenye ustawi kwa vizazi vijavyo.