Tuesday, September 22, 2026

MBUNGE AZZA AWATAKA WANANCHI KULINDA MIUNDOMBINU MIRADI YA MAJI, ATOA PESA KUNUNUA KOKI ZILIZOIBWA

 

Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masekelo.


Na Marco Maduhu, Elizabeth Cosmas- SHINYANGA

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, amewataka wananchi wa kijiji cha Masekelo, Kata ya Bukene wilayani Shinyanga, kulinda miundombinu ya miradi ya maji ili iweze kuwahudumia kwa muda mrefu, akieleza kuwa serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo.

TAZAMA VIDEO👇👇


Azza ametoa wito huo jana, Septemba 21, 2026, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji hicho, baada ya kubainika kuwa watu wasiojulikana wameiba koki 15 za maji na kusababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma hiyo.
Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maji, hivyo wananchi wanapaswa kuilinda na kutoa taarifa kwa viongozi na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu watu wanaohujumu miundombinu hiyo.

“Ninashukuru Shule ya Msingi Masekelo wenyewe wamenunua koki saba ili wanafunzi wapate maji, na zimesalia koki nane upande wa wananchi. Mimi kama Mbunge wenu ninatoa pesa hapa kwa Diwani, ili zinunuliwe koki nane na kufungwa, kisha maji yaanze kutoka kwa wananchi,” amesema Azza.
Aidha, amelitaka Jeshi la Jadi Sungusungu katika kijiji hicho kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya mradi huo wa maji ili kuzuia vitendo vya wizi na uharibifu.

Amesema wananchi wanapaswa kuwa na uzalendo katika kulinda miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, kwani vitendo vya uharibifu vinaweza kuwanyima huduma muhimu.

Aidha, amesema katika kijiji hicho miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa, ikiwamo miundombinu ya barabara na madaraja.
Kwa upande wake, Diwani wa Bukene Majaliwa Luhende, amesema serikali imefanya kazi kubwa ya kupeleka mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika kijiji hicho, lakini wizi wa koki umesababisha baadhi ya wananchi kushindwa kupata huduma.

Amesema ni muhimu wananchi kushirikiana na viongozi katika kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa ili wananchi waweze kunufaika na huduma hiyo.

TAZAMA PICHA NA ELIZABETH COSMAS👇👇

Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masekelo.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masekelo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...