Sunday, November 1, 2020

Jeshi la India lauwa kamanda wa waasi Kashmir


Jeshi la India leo hii limemuuwa kamanda wa juu wa waasi katika eneo tete la Kashmir, baada ya kutokea makabiliano makali ya risasi. India imeeleza tukio hilo kuwa mafanikio makubwa dhidi ya mapambano ya muda mrefu ya waasi hao dhidi ya utawala wa India. 


Kwa mujibu wa polisi, aliyeuwawa ni Saiffullah Mir, ambae alikuwa mkuu wa operesheni wa kundi kubwa la uasi la Hizbul Mujahideen, ambalo limekuwa mstari wa mbele katika uasi wa kijeshi dhidi ya utawala wa India kwa miongo kadhaa. 


Inspekta Jenerali Vijay Kumar alisema polisi na vikosi vya jeshi vilianzisha operesheni katika eneo la Srinagar, baada ya kupata taarifa za kiongozi huyo yupo katika maeneo hayo.

Tommy Flavour wa Alikiba akata mzizi wa fitna

Msanii wa lebo ya Kings Music ya Alikiba Tommy Flavour amesema hataki kufananishwa na wasanii wengine ambao wapo kwenye menejmenti zingine kwa sababu kila mtu ana mikakati yake kwenye suala zima la kufanya kazi.

Tommy Flavour amesema 'promotions' wanazofanyiwa wasanii wengine kwenye lebo zao wala hata hazimshuti ila anachoamini ni uwezo na kipaji cha mtu ndiyo kitamfanya awe juu kuliko kutumia nguvu ya 'promotions'.

"Hata kama unam-promote vipi msanii ila uwezo na kipaji chake ndiyo kitambeba na ndiyo itamfanya aendelee kwenye muziki, mimi naamini nitafika mbali na menejmenti yangu itanifikishia hilo, hata walivyonisaini haikuwa kwa ajili ya kunishindinisha na wasanii wengine kutoka lebo zingine" amesema Tommy Flavour 
 

The Story Book Msitu Wa Shetani wenye Vituko Vya Kutisha Vya Nguvu za Giza


The Story Book Msitu Wa Shetani wenye Vituko Vya Kutisha Vya Nguvu za Giza

VIDEO:

NEC YAMKABIDHI MAGUFULI CHETI CHA USHINDI KITI CHA URAIS TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akionesha Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Urais alichokabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage mara baada ya kutangazwa mshindi kwa Kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Urais kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage mara baada ya kutangazwa mshindi kwa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, hafla hiyo ya kukabidhiwa Cheti imefanyika katika Makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi NEC Njedengwa jijini Dodoma leo tarehe 01 Novemba 2020.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Makamu wa Rais kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kutangazwa mshindi kwa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Kiongozi wa Jopo la Waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020 Rais Mstaafu wa Burundi Silvestre Ntibantunganya mara baada ya kukabidhiwa Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Urais kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage leo tarehe 01 Novemba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama na Waliogombea Urais kupitia vyama Mbalimbali vya Upinzani nchini wakati Wimbo wa Taifa ukipigwa katika hafla fupi ya kukabidhi Cheti cha Ushindi kwa Kiti cha Urais zilizofanyika katika Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Njedengwa jijini Dodoma leo tarehe 01 Novemba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mara baada ya kukabidhiwa Cheti cha Ushindi kwa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wageni mbalimbali waliofika katika hafla fupi ya kukabidhiwa Cheti cha Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.

Sudan imesema imesaini na Marekani mpago wa kuzuia malipo ya fidia

 


Serikali ya Sudan imesema imetia saini makubalano na Marekani ambayo yatasimamisha kuendelea kulipa fidia zaidi, kutokana na kesi dhidi ya taifa hilo la Afrika zinazowasilishwa katika mahakama za Marekani, ikiwa ni baada ya serikali ya Marekani, kuliondoa taifa hilo katika orodha ya mataifa yenye kufadhili ugaidi. 

Waziri wa Sheria wa Sudan, Nasredeen Abdulbari amesema hatua hiyo inatekelezwa baada ya takribani mwaka mmoja wa majadiliano kati ya serikali ya Rais Donald Trump na uongozi mpya wa Sudan. Hatua hiyo itaanza kutekelezwa baada ya bunge la Marekani kupitisha sheria inayohitajika katika utekelezaji wa makubaliano hayo.

 Serikali ya mpito ya Sudan ilikubali kulipa dola milioni 335 kama fidia kwa waathirika wa mashambulizi ambayo yalifanywa na mtando wa al-Qaida, katika kipindi hicho kiongozi wa kundi hilo Osama bin Laden akiishi nchini Sudan.


Rais Mteule Dkt. Magufuli Kuapishwa Novemba 5, 2020 Dodoma

 


Rais Mteule wa Tanzania, Dkt. John Magufuli Novemba 5, 2020 ataapishwa katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa. Wananchi wanaopenda kuhudhuria wanakaribishwa kufika uwanjani kabla saa 1 asubuhi.

Magufuli Afunguka "Hiki ni Kipindi Changu cha Mwisho"

 


By Peter Elias, Mwananchi pelias@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020  na kubainisha kuwa baada ya kuibuka na ushindi ataliongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mingine mitano  na ndio itakuwa ya mwisho.


Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumapili Novemba Mosi, 2020  jijini Dodoma baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi na mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage.


Amewashukuru Watanzania kwa ushindi huo na kusema ana deni kubwa la kuwalipa kwa imani kubwa waliyoionyesha kumchagua tena kuliongoza Taifa hilo kwa miaka mingine mitano.


"Ninaipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kufanikisha uchaguzi huu kwa kuwahisha matokeo. Ninawashukuru Watanzania kwa kunichagua tena…, hiki ni kipindi cha pili cha mwisho."


 "Mmetupa ushindi mkubwa sana ambao umetuachia deni kubwa sana, ninamuomba Mungu anisaidie katika kipindi hiki cha pili tuweze kukidhi haja za Watanzania," amesema Rais Magufuli ambaye ameshinda uchaguzi kwa kura 12,516,252.


Amesema ushindi huo siyo wake peke yake wala wa chama chake bali ni wa Watanzania wote. Amesema atawatumikia wote bila kujali wanapotoka, dini au kabila.


 

Amewapongeza baadhi ya wagombea wenzake kwa kukubali matokeo na kwenda kushiriki hafla hiyo akisisitiza kuwa ni ishara ya kukomaa kwao kisiasa.


 "Tutajitahidi kuzingatia maoni yenu hasa yale yenye lengo la kuiletea Tanzania maendeleo," amesema kiongozi huyo.


 

Dkt. Magufuli na Dkt. Mwinyi kuapishwa wiki ijayo


 Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema shughuli ya kuapishwa kwa Rais Mteule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi na Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Magufuli zitafanyika wiki ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za chama hicho jijini Dar es Salaam Polepole amesema Dkt. Mwinyi ambaye alishinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020 ataapishwa Novemba 2, 2020 katika Uwanja vya Amani Zanzibar kuwa Rais wa awamu ya nane wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya rais Dkt. Ali Mohamed Shein kumaliza muda wake.

Siku mbili zimepita tangu Tume ya ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kumtangaza Dkt. Mwinyi kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa kujipatia kura 380,02 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote halali.

Kwa upande wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, Polepole amebainisha kuwa shughuli ya kuapishwa kwake kuongoza dola kwa muhula itafanyika Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Dkt. Magufuli alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali.

Katibu mkuu huyo amewashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukipatia ushindi wa kishindo, hivyo kuwataka kujitokeza kwa wingi katika matukio hayo muhimu la kuapishwa kwa viongozi wateule
.

Chama tawala Ujerumani CDU kumchagua kiongozi mpya mwezi Januari

 


Katibu Mkuu wa chama tawala cha Christian Democratic CDU nchini Ujerumani Paul Ziemiak ametangaza kuwa chama hicho kimeamua kufanya mkutano katikati ya mwezi Januari kumchagua kiongozi mpya wa chama hicho. 

Baada ya mazungumzo ya kina, wagombea watatu wa nafasi hiyo wameitaka bodi ya utendaji ya chama hicho kufanya mkutano huo Januari. 

Wagombea hao ni mwanabiashara wa zamani na kiongozi wa CDU bungeni Friedrich Merz, Waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia Armin Laschet na mtaalam wa masuala ya mambo ya nje katika chama hicho Norbert Röttgen. 

Mkutano huo wa wanachama 1001 ulikuwa umepangiwa kufanyika mwezi Disemba ila uliahirishwa kwa sababu ya janga la virusi vya corona. 

Chama cha CDU ndicho chama kikubwa zaidi katika bunge la Ujerumani, Bundestag, na kuwa kiongozi wa chama hicho inaonekana kuwa kama mwanzo wa kuchukua mikoba ya Kansela Angela Merkel kama kiongozi serikali ya nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Ulaya.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...