Katibu Mkuu wa chama tawala cha Christian Democratic CDU nchini Ujerumani Paul Ziemiak ametangaza kuwa chama hicho kimeamua kufanya mkutano katikati ya mwezi Januari kumchagua kiongozi mpya wa chama hicho.
Baada ya mazungumzo ya kina, wagombea watatu wa nafasi hiyo wameitaka bodi ya utendaji ya chama hicho kufanya mkutano huo Januari.
Wagombea hao ni mwanabiashara wa zamani na kiongozi wa CDU bungeni Friedrich Merz, Waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia Armin Laschet na mtaalam wa masuala ya mambo ya nje katika chama hicho Norbert Röttgen.
Mkutano huo wa wanachama 1001 ulikuwa umepangiwa kufanyika mwezi Disemba ila uliahirishwa kwa sababu ya janga la virusi vya corona.
Chama cha CDU ndicho chama kikubwa zaidi katika bunge la Ujerumani, Bundestag, na kuwa kiongozi wa chama hicho inaonekana kuwa kama mwanzo wa kuchukua mikoba ya Kansela Angela Merkel kama kiongozi serikali ya nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Ulaya.