Jamii, serikali na wadau wa elimu wanavyoshirikiana kukabiliana na ongezeko la wanafunzi litakalotokana na wanafunzi wa darasa la sita na la saba kuingia kidato cha kwanza kwa pamoja mwaka 2028
Na John Walter – Manyara
![]() |
| "Wananchi wa Kata ya Magugu wakishiriki ujenzi wa madarasa ili kujiandaa na ongezeko la wanafunzi litakalotokana na utekelezaji wa sera mpya ya elimu." |
Tanzania ipo katika kipindi muhimu cha mageuzi ya elimu yanayolenga kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza kwa muda mrefu zaidi na kupata maarifa yanayomwandaa kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, serikali imefanya maboresho makubwa ya mfumo wa elimu kwa kuongeza elimu ya lazima kutoka miaka saba hadi miaka 10. Maboresho hayo yanalenga kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata elimu ya sekondari, kuimarisha usawa katika elimu na kuwajengea wanafunzi maarifa, ujuzi na stadi za maisha zitakazowawezesha kujitegemea.
Tofauti na mfumo wa zamani ambao ulitambua darasa la saba kama mwisho wa elimu ya lazima, mfumo mpya unapanua wigo huo hadi ngazi ya sekondari. Aidha, maboresho hayo yanaweka mkazo katika elimu ya ujuzi, ubunifu, ujasiriamali na matumizi ya maarifa katika kutatua changamoto za maisha badala ya kutegemea elimu ya taaluma pekee.
Hata hivyo, pamoja na matarajio makubwa ya sera hiyo, utekelezaji wake umeibua changamoto mpya inayohitaji maandalizi ya haraka ya miundombinu ya elimu.
Mwaka 2028, Tanzania itashuhudia hali ya kipekee ambapo wanafunzi wa darasa la sita wanaohitimu kupitia mfumo mpya na wanafunzi wa darasa la saba wanaomaliza mfumo wa zamani wataingia kidato cha kwanza kwa wakati mmoja. Hali hiyo inayojulikana kama “double cohort” inatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi watakaojiunga na shule za sekondari nchini.
Ongezeko hilo lina maana moja kubwa; hitaji la madarasa zaidi, walimu zaidi, vitabu zaidi na mazingira bora zaidi ya kujifunzia.
Bila maandalizi ya kutosha, shule nyingi zinaweza kukabiliwa na mrundikano wa wanafunzi madarasani, hali inayoweza kuathiri ubora wa elimu na ufanisi wa ufundishaji.
Katika maeneo mbalimbali nchini, maandalizi tayari yameanza. Miongoni mwa maeneo yanayoonesha mfano wa namna jamii inavyoweza kushiriki katika utekelezaji wa sera mpya ni Kata ya Magugu, Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Katika kata hiyo, mjadala wa elimu umehamia kwenye jambo moja kubwa; madarasa.
Si kwa sababu shule zimefungwa. Si kwa sababu wanafunzi wamepungua. Bali kwa sababu mwaka 2028 unakuja na changamoto ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni ya elimu nchini.
Kwa mwanafunzi wa shule ya msingi, Shamila Juma, utekelezaji wa sera mpya una maana moja kuu; watoto wengi zaidi watapata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari.
"Elimu ya sekondari ni muhimu kwa sababu inamfanya mtu aweze kujitambua na kujitegemea," anasema.
Mawazo hayo yanaungwa mkono na mwenzake John Bayyo ambaye anaamini elimu ya sekondari ndiyo daraja la kuwapa vijana stadi za maisha na kuwaandaa kwa maisha ya baadaye.
Lakini wakati wanafunzi wakiona fursa, viongozi wa elimu wanaona changamoto kubwa inayohitaji maandalizi ya haraka.
Katika Shule ya Sekondari Magugu Day yenye wanafunzi zaidi ya 1,000, tayari dalili za changamoto hiyo zinaonekana.
Mkuu wa shule hiyo, Revokati Kimario, anasema shule hiyo kwa sasa ina upungufu wa madarasa saba.
Anabainisha kuwa mwaka 2026 shule ilipokea wanafunzi 338 wa kidato cha kwanza. Hata hivyo, makadirio yanaonesha kuwa mwaka 2028 shule hiyo inaweza kupokea wanafunzi zaidi ya 600.
Hii ni ongezeko la zaidi ya asilimia 77 ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Kwa lugha rahisi, kama maandalizi hayatafanyika mapema, wanafunzi wengi zaidi wataingia katika madarasa yale yale yaliyopo sasa.
Matokeo yake yanaweza kuwa mrundikano wa wanafunzi, kupungua kwa ufanisi wa ufundishaji, changamoto za usimamizi wa masomo na mazingira magumu ya kujifunzia.
Tatizo hilo si la Magugu pekee.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Paskalina Lowekelo, anasema halmashauri hiyo ina upungufu wa madarasa 60.
Kwa mujibu wake, changamoto hiyo imekuwa sehemu ya mjadala katika vikao vya wadau wa elimu vinavyoangalia namna ya kujiandaa na ongezeko la wanafunzi linalotarajiwa.
"Baadhi ya madarasa yatakayobaki wazi katika shule za msingi yanaweza kutumika kwa muda. Pia tumekuwa tukijadili namna ya kutumia uwezo uliopo katika baadhi ya shule za sekondari binafsi zenye wanafunzi wachache ili kupunguza shinikizo la wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza," anasema.
Kauli hiyo inaonesha kuwa changamoto ya mwaka 2028 haiwezi kutatuliwa na taasisi moja pekee, bali inahitaji ushirikiano wa serikali, sekta binafsi na jamii.
Lakini kinachoifanya Magugu kuwa mfano wa kipekee si ukubwa wa changamoto, bali namna wananchi walivyoamua kuikabili.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Magugu, Mary Simba, anasema kata hiyo inatarajiwa kuwa na upungufu wa vyumba 25 vya madarasa ifikapo mwaka 2028.
Kata hiyo inayojumuisha shule za sekondari za Magugu, Matufa, Gichameda na Sarame ndiyo kata kubwa zaidi katika Wilaya ya Babati.
Badala ya kusubiri kila kitu kifanywe na serikali, wananchi waliamua kuchukua hatua.
Kupitia mikutano ya vijiji iliyoandaliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata, wakazi walikubaliana kuchangia shilingi 10,000 kwa kila kaya ili kusaidia ujenzi wa madarasa.
Uamuzi huo unaweza kuonekana mdogo kwa mtu wa nje, lakini ndani yake umebeba ujumbe mkubwa; jamii imeanza kuiona sera ya elimu kama jukumu lake pia.
Diwani wa Kata ya Magugu na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, Stanley Charles, anasema michango hiyo ilianza Mei 15 na itaendelea hadi Julai 2026 huku ujenzi ukitarajiwa kuanza mwezi Agosti.
Anasema viongozi wa kata wameamua kuanza maandalizi mapema ili ifikapo mwaka 2028 changamoto ya madarasa isiwe kubwa kama inavyohofiwa sasa.
Kwa zaidi ya kaya 5,102 zilizopo Magugu, mchango huo unaweza kuzalisha nguvu kubwa ya kifedha kwa ajili ya maandalizi ya mwaka 2028.
Kwa sasa baadhi ya wazazi tayari wanashiriki katika ujenzi hadi kufikia hatua ya upauzi wa majengo ambapo boma moja linagharimu takribani shilingi milioni 12.5.
Kasimu Bakari ni miongoni mwa wananchi waliounga mkono mpango huo.
Kwake, elimu si jukumu la serikali pekee.
"Hakuna ombi hapa. Lazima tujenge kwa ajili ya watoto wetu. Watoto ni wetu," anasema.
Naye Mwanahamisi Hussein anaunga mkono jitihada hizo lakini anashauri kuwe na uratibu mzuri wa michango ya maendeleo.
"Tuko tayari kuchanga, lakini michango mingine ipunguzwe ili wananchi wabaki na nguvu ya kushiriki katika ujenzi wa madarasa," anasema.
Maoni hayo yanaonesha kuwa wananchi wako tayari kushiriki katika utekelezaji wa sera mpya mradi washirikishwe na waone matokeo ya michango yao.
Katika ngazi ya taifa, serikali imeendelea kusisitiza kuwa utekelezaji wa sera hiyo unaenda sambamba na maandalizi ya miundombinu na rasilimali watu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema mwaka 2027/2028 wanafunzi wa darasa la sita na darasa la saba wataingia sekondari kwa pamoja kutokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu.
Amesisitiza kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu ili kukabiliana na changamoto za madarasa, walimu na miundombinu mingine inayohitajika katika utekelezaji wa sera hiyo.
Katika kuimarisha utekelezaji wa mtaala mpya, serikali pia inatarajia kuajiri walimu 4,000 wa masomo ya biashara ili kuwajengea wanafunzi maarifa ya ujasiriamali na kuwawezesha kujitegemea baada ya masomo yao.
Hatua hiyo inaendana na lengo kuu la maboresho ya elimu; kuhamisha msisitizo kutoka elimu ya taaluma pekee kwenda elimu inayojenga ujuzi, ubunifu na uwezo wa kujiajiri.
Katika Shule ya Sekondari Kiru, maandalizi ya utekelezaji wa sera mpya tayari yanaonekana.
Mkuu wa shule hiyo, Isaack Makena, anasema serikali imejenga madarasa matano ya ziada, imetoa vitabu 1,100 vya mtaala mpya ulioboreshwa na kuongeza walimu watano.
Kwa mtazamo wake, mtaala mpya utawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi na kuwawezesha kujiandaa vyema kwa maisha ya baadae.
Mtazamo huo unaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya elimu, Lucas Alphonce, ambaye anaamini Tanzania imefika wakati wa kufanya mageuzi hayo ili kuendana na nchi nyingine zilizotangulia katika mfumo huo.
Anasema maboresho hayo yanaweza kusaidia kuandaa vijana wenye uwezo mkubwa wa kujitegemea na kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi za Afya Haydom, Bathomolayo Madangi, anasema mtaala mpya unapaswa kuendelea kuzingatia stadi za maisha, ujasiriamali na uwezo wa wanafunzi kujiajiri.
Anaamini mafanikio ya sera mpya hayatapimwa kwa idadi ya wanafunzi wanaohitimu pekee, bali kwa uwezo wao wa kutumia maarifa waliyojifunza kutatua changamoto za maisha.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2023 imekusudia kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu kwa usawa na kwa muda mrefu zaidi.
Lakini sera yoyote, hata ikiwa nzuri kiasi gani, haiwezi kufanikiwa bila ushiriki wa jamii.
Mfano wa Magugu unaonesha kuwa mafanikio ya sera hayawezi kutegemea serikali pekee. Yanahitaji ushiriki wa wazazi, viongozi wa jamii, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Wakati wengine wakisubiri kuona nini kitatokea mwaka 2028, wananchi wa Magugu tayari wanachanga fedha, wanajenga madarasa na wanashiriki katika kupanga mustakabali wa watoto wao.
Pengine mafanikio makubwa ya sera hii hayatakuwa idadi ya madarasa yatakayojengwa au walimu watakaoajiriwa.
Mafanikio yake yatakuwa pale ambapo wananchi wataacha kuiona elimu kama jukumu la serikali pekee na kuanza kuiona kama uwekezaji wao wenyewe.
Katika Kata ya Magugu, safari hiyo tayari imeanza kwa shilingi elfu kumi tu kutoka kila kaya, lakini thamani yake inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko fedha hizo; ni uwekezaji katika kizazi kijacho cha Tanzania.


.jpeg)