Thursday, June 11, 2026

NAMNA VITUO VYA KULELEA WATOTO YATIMA NA WANAOTOKA KWENYE MAZINGIRA MAGUMU VILIVYOSAIDIA KUPUNGUZA UKATILI KWA WATOTO.


Na Linda Mosseka-Manyara

Watoto ni taifa la kesho, msemo huu umezoeleka masikioni mwa wengi ukiwa umebeba maono makubwa ya maisha ya watoto wa kitanzania katika kuwaandaa kuwa watu muhimu kwenye jamii pale wanapofikisha umri wa utu uzima, ili waweze kulisaidia taifa kusonga mbele kimaendeleo kwa kutumia ujuzi, maarifa na vipaji walivyonavyo.

Mara nyingi mchakato wa watoto kuzifikia ndoto zao hukumbwa na mambo mengi mazito ikiwemo changamoto ya kiuchumi, maradhi na kubwa zaidi ni ukatili wanaofanyiwa kwenye jamii inayowazunguka hasa wazazi na ndugu wengine wakaribu wanaowategemea.

Kutokana na changamoto ya ukatili kuongezeka nchini kwa kiwango kikubwa, wadau mbalimbali kwa kushirikiana na serikali waliguswa kuwasaidia watoto wanaopitia changamoto mbalimbali kwa kuandaa vituo maalum vya malezi  ili kuhakikisha wanafikia ndoto zao.

Utaratibu wa kuanzisha vituo hivyo unasimamiwa na wizara ya maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum, kuanzia kwenye usajili na kuratibu namna vituo hivyo vinavyoendeshwa.

Vituo hivi ni vya binafsi, vinasajiliwa kama mashirika yasiyo ya kiserikali chini ya sheria inayosimamia mashirika hayo ya mwaka 2002 kifungu cha 56 na marejeo yake.

Katika makala hii tunaangazia ni kwa namna gani vituo hivyo vya kulelea watoto yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu vimesaidia kupunguza ukatili kwa watoto, ambatana nami kuanzia mwanzo hadi tamati ya makala hii jina langu ni Linda Moseka.

Kwa mujibu wa sheria za nchi ikiwemo katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 zinaweka bayana kuwa mtoto ni binadamu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18, na anastahili haki za msingi kama binadamu wengine ikiwemo haki ya kuishi, kulindwa kupata malezi bora, elimu na afya bora.

Kila kukicha nchini Tanzania na duniani kwa ujumla kumeripotiwa matukio mbalimbali ya ukatili dhidi ya watoto yanayopelekea watoto kushindwa kupata haki zao za msingi na badala yake wanajikuta kwenye dimbwi la mateso na manyanyaso yanayosababisha msongo wa mawazo na kupelekea  kufanya maamuzi magumu ikiwemo kujitoa uhai.

Kwa mujibu wa tafiti za shirika la afya duniani WHO takribani watoto bilioni moja wenye umri wa miaka 2-17 hupitia aina mbalimbali za ukatili kila mwaka ikiwemo ukatili wa kisaikolojia, kutokana na adhabu kali kutoka kwa wazazi au walezi wao.

Kwa upande wa tafiti za shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF 2025 zimeonesha kuwa watoto 6 kati ya 10 wenye umri wa miaka 2-14 hupitia ukatili wa kisaikolojia  wakiwa nyumbani ikihusisha kutukanwa, kufokewa kwa ukali au kudhalilishwa na wazazi au walezi wao.

Ripoti hiyo imeendelea kuonesha kuwa bara la Afrika ni miongoni mwa maeneo yenye viwango vya juu zaidi vya tatizo hili kwani takribani asilimia 80 ya watoto hupitia adhabu za vurugu nyumbani zinazojumuisha vipengele vya ukatili wa kisaikolojia na kimwili.

Nchini Tanzania utafiti wa kitaifa  wa ukatili dhidi ya watoto (VACS) wa mwaka 2024 ulionesha takribani asilimia 25 ya wasichana na asilimia 31 ya wavulana walipata ukatili wa kisaikolojia kutoka kwa watu wazima kabla ya kufikisha miaka 18.

Mtiririko wa ripoti hizi unaonesha wazi kuwa bado changamoto ya ukatili kwa watoto katika jamii ni kubwa na mikakati ya ziada inahitajika ili kuhakikisha ukatili unatokomezwa, ikiwa sambamba kabisa na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na marejeo yake ya mwaka 2019, ambapo kifungu cha 13 kinakataza mtu yeyote kumtesa mtoto au kumfanyia adhabu nyingine ya kikatili, isiyo ya kibinadamu  au inayodhalilisha utu wake.

Moja ya njia madhubuti ambayo serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania pamoja na wadau wameamua kuitumia ili kupunguza ukatili kwa watoto ni kuanzisha vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu, vituo hivi vinaendeshwa kwa uangalizi wa serikali na misaada ya wadau binafsi na wafadhili.

Nchini Tanzania kuna takribani mashirika 8,959 yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa, yanayohudumu katika sekta mbalimbali za maendeleo ya jamii kama afya, elimu, haki za binadamu na ustawi wa watoto.

Mashirika yaliyojikita kufanya kazi katika masuala ya maendeleo na ustawi wa mtoto nchini Tanzania hadi kufikia mwaka 2025 ni takriban mashirika 142.

Katika mkoa wa Manyara kuna takribani vituo saba (7) vinavyolea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu, moja kati ya vituo hivyo ni kituo cha Hossana Home Care Foundation kilichopo mtaa wa Nyawari, kata ya Singe wilayani Babati mkoani Manyara.


Nimepata fursa ya kutembelea kituo hicho ili kujionea maendeleo ya watoto wanaolelewa katuoni hapo, na kwa hakika nimekutana na watoto wenye nyuso nzuri za matumaini zilizojawa na tabasamu zinazoashiria kwamba wapo sehemu salama.

Nakutana na binti shupavu, mwenye kujiamini aliyebeba hadithi ya kusisimua kwa mapambano magumu aliyopitia yaliyomfanya kukataa tamaa hadi pale tumaini jipya lilipoingia baada ya kupata nafasi ya kulelewa katika kituo hicho.

Binti huyu anatambulika kwa jina la Doreen Dastan mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Ft Sumaye, Doreen anasimulia hadithi ya kusisimua ya maisha yake iliyomfanya apitie changamoto ya ukatili wa kisaikolojia kutoka kwa baba yake mzazi, kwani suala la ugomvi baina ya Baba na Mama ilikuwa ni maisha ya kawaida sana kwao, achilia mbali maisha duni ya familia.

Doreen anasema aliishi maisha ya kufokewa, kutukanwa na hadi kupelekea kuwa na msongo mkubwa wa mawazo akitafakari ni lini ataipata amani kwani alikosa tumaini kabisa na hali ikawa mbaya zaidi baada ya wazazi kutengana, mama yake aliamua kuhama kutoka Morogoro na kuhamia mjini Babati baada ya kushindwa kuvumilia maisha ya manyanyaso na vipigo kwake na kwa watoto wake.


"Baba yangu hakuwa mlevi bali alikuwa mtu mkorofi sana, licha ya ugumu wa maisha tuliokuwa nao lakini ugomvi usiokwisha nyumbani ilikuwa ni changamoto nyingine kubwa kwangu, nilitamani maisha ya amani na utulivu na hata uamuzi wa mama kuhama kutoka Morogoro kuja Babati uliongeza changamoto nyingine, kwani changamoto za magonjwa kwa mama zilikuwa nyingi na hatukuwa na pesa, na iliniongezea mawazo zaidi kwakuwa nilikosa tumaini la kusonga mbele". Ameeleza Doreen.

Licha ya changamoto hizo, ndoto ya kupata elimu kwa Doreen haikufa kwani aliendelea kujitahidi kwenda shule huku Mama yake akifanya jitihada za kutafuta msaada huku na kule kwa kushirikiana na ndugu na ndipo tumaini jipya likatokea baada ya kupata nafasi ya kulelewa katika kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu cha Hossana Home Care Foundation.

Doreen anasema ilikuwa furaha kubwa sana kwake kwenda kuanza maisha mengine ya utulivu na amani akiamini kutimiza ndoto zake za kuwa Mwandishi bora wa habari hapa nchini, na kwa sasa anakiri kupata utulivu wa akili kwani anaishi vizuri na anapata mahitaji ya msingi kama mtoto na hatamani kabisa kurudi kwa baba yake kwa kuhofia aliyoyapitia.

"Mama yangu ni fundi cherehani lakini kipato chake kilikuwa kidogo sana hata kodi ya nyumba alishindwa kulipa, ndipo kwa kushirikiana na Mama yangu mkubwa wakaamua kunitafutia msaada ili nimpunguzie mzigo wa mahitaji ya shule na ndipo nikapata nafasi kwenye kituo hichi ambacho kwakweli nimefurahi sana kwani ninaishi vizuri na nina amani hata msongo wa mawazo umeisha, naamini kwa hapa nilipo nitatimiza ndoto zangu za kuwa Mwandishi bora wa habari". Ameongeza Doreen.

Kwa sasa Doreen anafurahi kukutana na marafiki wapya katika kituo hicho akiwemo rafiki yake kipenzi Mwanaisha Juma ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Balang'dalalu, na kwa pamoja wanapambania ndoto zao, japo hadithi ya Mwanaisha iligubikwa zaidi na changamoto ya kiuchumi kwa familia yake kiasi cha kupata mlo mmoja tu kwa siku na jitihada zake binafsi zikamfanya kupata fursa hii baada ya kueleza changamoto yake kwa Mwalimu mkuu na kumuombea nafasi ya kulelewa kituoni hapo, kwa pamoja wanaamini kufanikiwa kwani wanafundishwa maadili mema na namna ya kukabiliana na changamoto.


"Mimi nilikuwa napata mlo mmoja tu kwa siku, hata shuleni nilikuwa sili kwakuwa wazazi walishindwa kulipia chakula, ndipo nikaamua kuzungumza na mwalimu mkuu ili aweze kunisaidia, na ninamshukuru sana kwani alinisaidia kuniombea nafasi kwenye kituo hichi cha Hossana na kwasasa naishi hapa nimepata marafiki kama Doreen na tunaamini tutatimiza ndoto zetu". Ameeleza Mwanaisha Juma rafiki yake Doreen Dastan

Kwenye vituo hivi vya kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu wapo wasimamizi wanaoishi na watoto na kuwahudumia mahitaji yao ya msingi ya kilasiku, ndivyo ilivyo pia katika kituo cha Hossana yupo mwanadada anayetambulika kwa jina la Annagress Justin anayefanya kazi ya kuwahudumia na kuwafundisha mambo mbalimbali ya kimaadili.

Annagress anasema ameanza kazi katika kituo hicho tangu mwaka 2021 na amewapokea watoto wengi ambao baada ya kufika katika kituo hicho walionesha mabadiliko makubwa ikiwemo kuwa na afya njema na furaha, kwani watoto wengi walikuwa wamedhoofu na wanamsongo mkubwa wa mawazo kutokana na yale waliyopitia huko nyumbani.

Ukiachilia mbali chakula na malazi Annagress anasema wanafundisha maadili na kumjua Mungu kupitia dini zao ili wafuate yale ambayo mwenyezi Mungu anaamuru kupitia vitabu vyake vitakatifu na zaidi kabisa ni kuhusu stadi za maisha kwani wanafanya kazi mbalimbali za mikono ikiwemo kupika, kuosha vyombo, kutunza bustani na kulima, yote haya ni kwa lengo la kuwajengea uimara wa kimwili na kiakili na kuujua uhalisia wa maisha na nafasi zao katika jamii na wanashirikiana vyema na maafisa ustawi ikiwemo kuwaletea miradi ya kuku na mbuzi.


"Watoto wengi wanaokuja hapa changamoto zao kubwa huko nyumbani ni wazazi kuwa walevi, akija nyumbani hamjali tena kama mtoto, ni kumchapa na adhabu nyingine zisizostahili, sisi kwanza sheria yetu ni kilasiku lazima tuungane pamoja na tusali, lakini pia siku za ijumaa kwa waislamu wanaenda msikitini na wakristo jumapili kanisani na pia tunawafundisha shughuli za mikono na tunamiradi ya kuku na mbuzi". Amesema Annagress mlezi wa watoto.

Annagress anasema wapo watoto wengi wenye uhitaji lakini wao kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii wanawasidia kufuatilia kwenye maeneo yao ili kugundua kama kuna watoto wenye changamoto na wanaandika barua ya kuomba nafasi ya malezi.

"sisi tunaletewa na maafisa ustawi wa jamii, afisa ustawi baada ya kujua changamoto ndiyo anamleta hapa na atapiga simu kuomba na tunashirikiana nao vizuri".Ameongeza Annagress mlezi wa watoto kituoni hapo.

Matokeo ya utafiti wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto Tanzania (VACS) umeonesha kupungua kwa ukatili wa kisaikolojia, kwa wasichana umepungua kutoka 25% mwaka 2009 hadi kufikia 22% mwaka 2024 na kwa wavulana umepungua kutoka 31% mwaka 2009 hadi kufikia 16% mwaka 2024.

Takwimu hizi zinasadifiwa na maelezo ya afisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya mji wa Babati Agatha Patrice, ambaye amekiri kuwa uwepo wa vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu umesaidia kupunguza ukatili kwa watoto.

"Tunaona wazi kuwa vituo vimetusaidia kutulelea watoto na vimesaidia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto, kwani watoto wengi wanatoka kwenye familia zenye migogoro ya muda mrefu inayopelekea hata wazazi kuachana na kuwafanya watoto waishi katika mazingira magumu ya msongo wa mawazo kwasababu hakuna amani na utulivu nyumbani". Ameeleza Agatha Patrice afisa ustawi wa jamii halmashauri ya mji wa Babati.

Afisa ustawi Agatha Patrice ameongeza kuwa kwa sasa wanaendelea na jitihada za kubaini watoto wenye changamoto za ukatili kwenye jamii kwa kutumia utaratibu wa kupata taarifa mbalimbali kutoka kwenye mitaa na kata na kupitia kwa watu wanaoona familia zenye changamoto na watoto wanaothirika kama mabalozi na wenyeviti wa mitaa, na mara nyingi huwa wanafika ofisini na baada ya hapo wanaanza kufatilia na wakibaini huandika barua kwenye vituo kuomba nafasi.

"Utaratibu ambao tunautumia ni kupata taarifa mbalimbali kutoka kwenye kata na mitaa kupitia kwa watu wanaoona kabisa kwamba familia fulani watoto wanaathirika au kwa mabalozi na wenyeviti wa mitaa, kwahiyo tunavyopata hizo taarifa kama halmashauri tunachukua hatua ya kufika kwenye eneo husika tutawakuta hao watoto, tutaongea na majirani, tutamtafuta mzazi na tukijiridhisha tunaandika barua ya maombi kwenye hizi taasisi za kulelea watoto na tunawapeleka". Ameongeza Agatha Patrice afisa ustawi wa jamii halmashauri ya mji wa Babati.

Ushirikiano mzuri baina ya maafisa ustawi wa jamii na vituo vya kulele watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kiasi kikubwa unaonekana kusaidia ustawi wa watoto kwenye jamii kwani mazingira bora, amani na utulivu ni nyenzo kubwa sana za kumupeusha mtoto na ukatili.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa Saikolojia na Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Iringa kitivo cha Saikolojia Robert Lwiza anasema maendeleo ya mtoto huletwa na amani na utulivu, ambavyo vinamsaidia mtoto kujenga akili yenye afya, hisia zilizo imara, kujiamini na uwezo mzuri wa kujifunza na kuhusiana na wengine.

"Amani na utulivu humsaidia mtoto kujenga akili yenye afya, kujiamini, hisia zilizo imara na uwezo wa kuhusiana na wengine na kujifunza na hata uwezo kuzikabili changamoto na ndio maana huwa tunasisitiza sana umuhimu wa mazingira salama, yenye upendo na yasiyo na migogoro mikubwa katika malezi ya mtoto ili aepukane na ukatili wa kisaikolojia".Amesema Mwanasaikojia Robert Lwiza.

Mafanikio haya ya kupunguza ukatili kwa watoto yanakwenda sambamba na juhudi za wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu, inayoongozwa na mwanamama shupavu Dkt Dorothy Gwajima ambayo inasamimia sheria, sera na miongozo mbalimbali inayohusu ustawi wa watoto hapa nchini Tanzania.

Na mara kadhaa kupitia majukwaa mbalimbali ametoa wito kwa jamii kuacha ukatili kwa watoto  na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuwafundisha watoto bila kuwaletea madhara.


"Wapendwa walezi na walimu wa watoto wetu mashuleni, pamoja na kazi nzuri mnayofanya hima zingatieni kulea watoto pasipo kuwaletea madhara ya adhabu zilizo nje ya mwongozo, vinginevyo mtaendelea kuhatarisha ustawi wa watoto". Alisema Dkt Dorothy Gwajima waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu.

Kwasasa Doreen Dastan anamatumaini makubwa ya kutimiza ndoto zake za kuwa mwandishi bora wa habari ili aisaidie jamii kupaza sauti juu ya mambo ya ukatili na kuhakikisha jamii inakuwa sehemu salama na anaiomba serikali na wadau binafsi waendelee kuwashika mkono ili waendelee kusonga mbele.


Ama hakika mwanzo wa ngoma ni lele na hakuna marefu yasiyo na ncha na kufikia hapa ndio tamati ya makala hii, iliyoangazia ni kwa namna gani vituo vya kulele watoto yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu vinavyosaidia kupunguza ukatili kwa watoto, bila shaka umejifunza mengi, hadi wakati mwingine jina langu ni Linda Moseka.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...