Wafanyakazi wa nyumbani wameibua wanaokumbana nao wanapotekeleza majukumu yao katika nyumba wanazofanyia kazi, wakisema vitendo hivyo vinahatarisha usalama wao, vinadhalilisha utu wao na kuathiri afya zao ya kimwili na kisaikolojia.
Changamoto hiyo imeelezwa wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa majumbani kuhusu haki zao,katika Mradi unaotekelezwa na Chama Cha Wafanyakazi ‘CWM’Jimboni Morogoro ’’Wape wafanyakazi wa majumbani fursa ya kupata mafunzo ya kuwaongezea ujuzi” ambapo washiriki wametaka hatua madhubuti kuchukuliwa ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya unyanyasaji vinavyofanyika katika mazingira ya kazi.
Veronica Jonas mfanyakazi wa nyumbani amesema alianza kufanya kazi za nyumbani tangu mwaka 2020 akiwa mkoani Kigoma,amesema kazi za nyumbani zina changamoto nyingi anakabiliana nazo kuhakikisha malengo yake yanatimia na faida pia ni nyingi kwa sababu kazi hiyo inampatia kipato kukidhi mahitaji yake.
Aidha amesema kuwa miongoni mwa changamoto alizowahi kukutana nazo kupitia kazi yake ni baba mwenye nyumba kumtaka kimapenzi, hali iliyomlazimu kuacha kazi kwa ajili ya kulinda usalama wake na kuepusha fedheha kwa mama mwenye nyumba na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo amesema kuwa licha ya uzoefu wake kazini hakuwahi kujua namna ya kupigania haki zake inapotokea hali ya kudhulumiwa, kwa hiyo kupitia mafunzo hayo amejifunza kwamba wafanyakazi wa nyumbani wana haki kama wafanyakazi wengine pamoja na kuzijua sheria zinazowalinda ikiwemo suala la mkataba wa ajira.
’’Kiukweli kwenye suala la haki nilikuwa sijui lolote, kwa mfano changamoto yangu ya kutakwa kimapenzi na baba mwenye nyumba,sikudai chochote zaidi ya kutumia mbinu mbadala ya kukimbia na kutoroka lakini nimetambua kuwa tuna sheria zinazotulinda, nami nitaelimisha wenzangu wanaofanya kazi hizi’’ amesema Veronica.
Hata hivyo ameshauri waajiri wapewe elimu zaidi kupata uelewa ili kuondoa dhana ya kuajiri wafanyakazi wa nyumbani kwa mazoea wakiamini kwamba mfanyakazi wa ndani anachohitaji ni pesa tu na kusahau kwamba utu ni muhimu kuliko pesa yenyewe,akishauri serikali isaini mkataba kwa sababu wafanyakazi hao wameteseka kwa muda mrefu.
’’Niwaombe waajiri wetu watimize wajibu wao kwetu, kama wao wanavyopigania kuoanda vyeo na mshahara mzuri kazini kadhalika nasi pia tunaomba watuthamini, wanapoenda kazini wanatuacha nyumbani tukifanya kazi zao, kama wanavyochukia rushwa ya ngono kazini nasi pia tunachukia hivyo hivyo,walitambue hilo nasi tuna haki zetu’’amefafanua Veronica
Naye Witnes Joseph alianza kufanya kazi za nyumbani tangu mwaka 2020 baada yaya wazazi wake kuachana na familia kuachwa kwa bibi, ilimlazimu kufanya kazi hizo ili kupata fedha ya kumsaidia mdogo wake kuendelea na masomo ambaye kwa sasa yuko kidato cha tatu
Ameeleza kuwa yeye mwenyewe ameishia darasa la saba alitamani aendelee kusoma lakini hakufanikiwa baada ya kukosa mtu wa kumsaidia, kwa hiyo ataendelea kufanya kazi za nyumbani mpaka pale mdogo wake atakapotimiza ndoto zake za elimu.
Licha ya kulipwa mshahara mdogo Witnes amebeba mzigo mkubwa wa majukumu, mbali na kumsaidia mdogo wake lakini pia anamsaidia mjomba wake ambaye kwa sasa yuko chuo kikuu, furaha yake ni kuona ndoto za watu hao zinatimia.
’’Mjomba wangu anakaribia kumaliza chuo mwaka huu, mara nyingi akiwa na shida ananitafuta namsaidia,mtoto wa bibi yangu na mtoto wa dada yangu naye yuko chuo akiwa na shida ananitafuta kama ninacho nawapa’’
Ndoto ya Witnes ilianza kuzima ghafla pale ilipoanza kujitokeza changamoto ya kutakwa kimapenzi na watoto wa mwajiri wake,ikamlazimu kuacha kazi na kuja Mkoani Morogoro kutafuta kazi ambapo kwa sasa anaishi kwa amani na upendo kama mtoto wa familia.
Ameongeza kuwa fursa ya mafunzo iliyoandaliwa na CWM kushirikiana na Chuo cha Veta Mikumi masomo hayo yatamsaidia kuongeza ujuzi,kumwendeleza mdogo wake elimu ya juu, naye akiwa ni miongoni mwa kundi la kwanza linalotarajia kuanza rasmi mafunzo ya ufundi juni 15 mwaka huu.
