



Source




Kampuni ya Tanga Saruji imeweka historia mpya katika masoko ya mitaji nchini Tanzania kwa kuzindua rasmi mauzo ya Hisa Stahiki zenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 204. Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni nchini kutoa hisa stahiki za thamani kubwa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua inayotajwa kuwa ya kimkakati katika kuimarisha uwekezaji na kuongeza thamani kwa wanahisa.
Hisa hizi stahiki zinauzwa kwa wanahisa wa sasa wa Kampuni ya Tanga Saruji kwa bei ya shilingi 1,600 kwa hisa moja, ambayo ni punguzo la asilimia 38.2 ukilinganisha na bei ya soko ya shilingi 2,590 kwa hisa moja. Kiasi cha hisa kinachotolewa ni 127,342,090, katika uwiano wa hisa mbili kwa kila hisa moja anayomiliki mwekezaji kwa sasa.
Aidha Utoaji huo wa hisa umetajwa kuwa umekidhi kikamilifu matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania pamoja na Kanuni zake, baada ya kupokea idhini rasmi kutoka CMSA.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, ongezeko la thamani ya hisa za Kampuni ya Saruji Tanga limekuwa kubwa kwa kipindi cha muda mrefu – kutoka shilingi 300 mwaka 2002 hadi shilingi 2,590 kwa hisa moja mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 763.3.
"Tunaipongeza Kampuni ya Tanga Saruji kwa mafanikio haya makubwa. Hili ni somo na mfano kwa kampuni nyingine zilizo orodheshwa katika soko la hisa kuendelea kuboresha ufanisi na utawala bora," aliongeza CPA Mkama.
Aidha, alieleza kuwa mafanikio ya Tanga Cement ni uthibitisho wa nafasi muhimu ya masoko ya mitaji katika kukuza uchumi wa Taifa, kwa kutoa mitaji ya muda mrefu kwa kampuni, kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha umiliki wa pamoja wa rasilimali za uzalishaji.
Pia CPA Mkama amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (TDV 2050), ambayo inalenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu na kufikia Pato la Taifa la Dola Trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) pia imepongeza wadau waliohusika katika mchakato wa maandalizi ya Waraka wa Matarajio, akiwemo mshauri kiongozi wa kifedha iTrust Finance Limited, Mshauri wa Kisheria Joachim & Jacobs Attorneys, pamoja na wakaguzi Deloitte & Touche, kwa weledi wao mkubwa uliofanikisha hatua hii muhimu.
Mchakato wa mauzo ya hisa hizo unatarajiwa kufungwa Oktoba 24, 2025, na wanahisa wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo adhimu ya kuongeza uwekezaji wao kwa bei ya punguzo.
"Napenda kutoa wito kwa wanahisa wote kutumia fursa hii kununua hisa stahiki, ili kuimarisha uwekezaji wao na kuwa sehemu ya mafanikio endelevu ya kampuni hii ya kihistoria," aliongeza
CPA Mkama pia amezitaka kampuni nyingine katika sekta binafsi na umma kutumia kikamilifu masoko ya mitaji kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, badala ya kutegemea mikopo ya gharama kubwa.










Na John Walter-Babati
Kona ya Sigino, maarufu kwa kuwa tishio kwa madereva wa magari ya mizigo, imeendelea kuwa chanzo cha maafa baada ya ajali mbaya kutokea tena alfajiri ya Septemba 8, 2025.
Tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku, ambapo gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 859 ASR lililokuwa limebeba mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, mbaazi na dengu, lilishindwa kudhibiti mwendo na kupinduka katika Kijiji cha Sigino, wilayani Babati, mkoani Manyara.
Gari hilo lilikuwa likitokea Wilaya ya Hanang' kuelekea mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa za Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Dkt. Mathias Kimaro, walipokea mwili wa mwanaume mmoja aliyefariki dunia pamoja na majeruhi wawili wanaume, ambao hali zao zinaendelea kuimarika.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sigino Chini, Victor Mollel, amesema eneo hilo limekuwa likisababisha ajali mara kwa mara kutokana na kona kali na mteremko mkali, hasa kwa magari ya mizigo yanayopoteza breki.
Ameiomba serikali kuweka vizuizi au kuchukua hatua madhubuti ili kuokoa maisha na mali za wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sigino, Manfred Sumaye, amesema makumi ya maisha yamepotea katika eneo hilo kwa miaka mingi, huku malalamiko ya wananchi yakipuuzwa na mamlaka husika.
"Tumekuwa tukipeleka maombi yetu mara kwa mara, lakini hatua madhubuti bado hazijachukuliwa, ajali ya jana imetokea majira ya saa sita usiku na imeacha simanzi kubwa," amesema Sumaye.
Miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo ni Faustin Nada, mkazi wa Alosabida aliyekuwa akisafiri kuelekea Arusha na mzigo huo.
Zakayo Ibrahim mkazi wa Gehandu Hanang', alieleza kuwa baada ya ajali alipigiwa simu na Faustin akiomba msaada, akaanza safari ya kuja Babati lakini alikuta akiokolewa na watu waliokuwa wakishirikiana na jeshi la Zimamoto na uokoaji majira ya saa 12 asubuhi akiwa hoi huku akidai ana njaa kali kwa sababu tangu jana hakuwa amekula.
Eneo la kuanzia Singu kuelekea Sigino linatajwa kuwa hatari zaidi kutokana na mteremko mkali na kona zinazohitaji uangalizi wa hali ya juu.
Madereva wengi wa malori makubwa hutegemea breki za upepo ambazo mara nyingine hushindwa kufanya kazi, na kufikia daraja la Sigino ambapo maafa hutokea.
Licha ya mafunzo na maonyo kwa madereva, Kona ya Sigino imeendelea kuwa "mwiba mkali" kwa usalama barabarani – ikipoteza maisha ya watu, kuacha wengine na ulemavu wa kudumu, na kuisababishia jamii hasara kubwa kutokana na magari na mizigo kuharibika.