Tuesday, September 9, 2025

Ajali ya Malori Kona ya Sigino Yaendelea Kugharimu Maisha


Na John Walter-Babati

Kona ya Sigino, maarufu kwa kuwa tishio kwa madereva wa magari ya mizigo, imeendelea kuwa chanzo cha maafa baada ya ajali mbaya kutokea tena alfajiri ya Septemba 8, 2025.

Tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku, ambapo gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 859 ASR lililokuwa limebeba mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, mbaazi na dengu, lilishindwa kudhibiti mwendo na kupinduka katika Kijiji cha Sigino, wilayani Babati, mkoani Manyara. 

Gari hilo lilikuwa likitokea Wilaya ya Hanang' kuelekea mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa za Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Dkt. Mathias Kimaro, walipokea mwili wa mwanaume mmoja aliyefariki dunia pamoja na majeruhi wawili wanaume, ambao hali zao zinaendelea kuimarika.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sigino Chini, Victor Mollel, amesema eneo hilo limekuwa likisababisha ajali mara kwa mara kutokana na kona kali na mteremko mkali, hasa kwa magari ya mizigo yanayopoteza breki. 

Ameiomba serikali kuweka vizuizi au kuchukua hatua madhubuti ili kuokoa maisha na mali za wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sigino, Manfred Sumaye, amesema makumi ya maisha yamepotea katika eneo hilo kwa miaka mingi, huku malalamiko ya wananchi yakipuuzwa na mamlaka husika. 

"Tumekuwa tukipeleka maombi yetu mara kwa mara, lakini hatua madhubuti bado hazijachukuliwa,  ajali ya jana imetokea majira ya saa sita usiku na imeacha simanzi kubwa," amesema Sumaye.

Miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo ni Faustin Nada, mkazi wa Alosabida aliyekuwa akisafiri kuelekea Arusha na mzigo huo. 

Zakayo Ibrahim mkazi wa Gehandu Hanang',  alieleza kuwa baada ya ajali alipigiwa simu na Faustin akiomba msaada, akaanza safari ya kuja Babati lakini alikuta akiokolewa na watu waliokuwa wakishirikiana na jeshi la Zimamoto na uokoaji majira ya saa 12 asubuhi akiwa hoi huku akidai ana njaa kali kwa sababu tangu jana hakuwa amekula.

Eneo la kuanzia Singu kuelekea Sigino linatajwa kuwa hatari zaidi kutokana na mteremko mkali na kona zinazohitaji uangalizi wa hali ya juu. 

Madereva wengi wa malori makubwa hutegemea breki za upepo ambazo mara nyingine hushindwa kufanya kazi, na kufikia daraja la Sigino ambapo maafa hutokea.

Licha ya mafunzo na maonyo kwa madereva, Kona ya Sigino imeendelea kuwa "mwiba mkali" kwa usalama barabarani – ikipoteza maisha ya watu, kuacha wengine na ulemavu wa kudumu, na kuisababishia jamii hasara kubwa kutokana na magari na mizigo kuharibika.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...