Tuesday, September 30, 2025

CMSA Yaipongeza Tanga Saruji kuzindua Mauzo ya Hisa Stahiki za Bilioni 204

Kampuni ya Tanga Saruji imeweka historia mpya katika masoko ya mitaji nchini Tanzania kwa kuzindua rasmi mauzo ya Hisa Stahiki zenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 204. Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni nchini kutoa hisa stahiki za thamani kubwa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua inayotajwa kuwa ya kimkakati katika kuimarisha uwekezaji na kuongeza thamani kwa wanahisa.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama aliipongeza Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya Saruji Tanga kwa uongozi thabiti, ujasiri na maono ya kimkakati yaliyopelekea mageuzi makubwa ya kiutendaji ndani ya kampuni hiyo.

"CMSA tunaridhishwa na hatua za mabadiliko ya kimkakati yanayoendelea katika kampuni hii, ikiwa ni pamoja na kupunguza mikopo ya kigeni, kuongeza mapato na faida ya kampuni, na kutoa fursa zaidi za uwekezaji kwa wananchi," alisema CPA Mkama

Hisa hizi stahiki zinauzwa kwa wanahisa wa sasa wa Kampuni ya Tanga Saruji kwa bei ya shilingi 1,600 kwa hisa moja, ambayo ni punguzo la asilimia 38.2 ukilinganisha na bei ya soko ya shilingi 2,590 kwa hisa moja. Kiasi cha hisa kinachotolewa ni 127,342,090, katika uwiano wa hisa mbili kwa kila hisa moja anayomiliki mwekezaji kwa sasa.

Aidha Utoaji huo wa hisa umetajwa kuwa umekidhi kikamilifu matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania pamoja na Kanuni zake, baada ya kupokea idhini rasmi kutoka CMSA.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, ongezeko la thamani ya hisa za Kampuni ya Saruji Tanga limekuwa kubwa kwa kipindi cha muda mrefu – kutoka shilingi 300 mwaka 2002 hadi shilingi 2,590 kwa hisa moja mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 763.3.

"Tunaipongeza Kampuni ya Tanga Saruji  kwa mafanikio haya makubwa. Hili ni somo na mfano kwa kampuni nyingine zilizo orodheshwa katika soko la hisa kuendelea kuboresha ufanisi na utawala bora," aliongeza CPA Mkama.

Aidha, alieleza kuwa mafanikio ya Tanga Cement  ni uthibitisho wa nafasi muhimu ya masoko ya mitaji katika kukuza uchumi wa Taifa, kwa kutoa mitaji ya muda mrefu kwa kampuni, kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha umiliki wa pamoja wa rasilimali za uzalishaji.

Pia CPA Mkama amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (TDV 2050), ambayo inalenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu na kufikia Pato la Taifa la Dola Trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) pia imepongeza wadau waliohusika katika mchakato wa maandalizi ya Waraka wa Matarajio, akiwemo mshauri kiongozi wa kifedha iTrust Finance Limited, Mshauri wa Kisheria Joachim & Jacobs Attorneys, pamoja na wakaguzi Deloitte & Touche, kwa weledi wao mkubwa uliofanikisha hatua hii muhimu.

Mchakato wa mauzo ya hisa hizo unatarajiwa kufungwa Oktoba 24, 2025, na wanahisa wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo adhimu ya kuongeza uwekezaji wao kwa bei ya punguzo.

"Napenda kutoa wito kwa wanahisa wote kutumia fursa hii kununua hisa stahiki, ili kuimarisha uwekezaji wao na kuwa sehemu ya mafanikio endelevu ya kampuni hii ya kihistoria," aliongeza

CPA Mkama pia amezitaka kampuni nyingine katika sekta binafsi na umma kutumia kikamilifu masoko ya mitaji kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, badala ya kutegemea mikopo ya gharama kubwa.

 








Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...