Sunday, August 10, 2025

Mama Manyara adaiwa kumuua mtoto wake kikatili kwa shoka.


Na John Walter Babati, Manyara

Wakazi wa Kitongoji cha Vituwey, Kijiji cha Ngoley, Kata ya Mwada wilayani Babati mkoani Manyara wameshtushwa na tukio la kikatili lililofanywa na mwanamke anayejulikana kwa jina la Mariam Mohamed, anayedaiwa kumuuua mtoto wake wa kumzaa wa kiume mwenye umri wa miaka 2.5 kwa kumtenganisha viungo vya mwili wake kwa kutumia shoka.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Vituwey, Jackson Mombo, amesema tukio hilo lililotokea majira ya saa nne asubuhi Agosti 8, 2025, limewaacha wananchi midomo wazi na kushindwa kuamini kilichotokea. 

Ameongeza kuwa ni muhimu jamii kuwa karibu na mtu yeyote anayeonyesha dalili za mawazo mazito au matatizo ya afya ya akili ili kuepusha madhila kama hayo.

Mashuhuda wamesema kuwa baada ya mauaji hayo, Mariam alipiga yowe akisema "jamani nisaidieni, nimemuua mwanangu", hali iliyowafanya majirani kukimbilia nyumbani kwake ambapo walipofika, walimkuta akiwa hajakimbia, huku mwili wa mtoto ukiwa juu ya godoro wanalolalia.

Baadhi ya majirani wamesema hawaamini kuwa mama huyo amefanya kitendo hicho kwa akili timamu, wakidhani huenda alikuwa na tatizo la afya ya akili.

Baba mkwe wa Mariam, Kimweri Juru, ameeleza kuwa aliwahi kumpa onyo mara kadhaa kuhusiana na tabia ya unywaji wa pombe, lakini hakutaka kusikia, na kwamba matokeo haya yanaweza kuwa ni sehemu ya madhara ya tabia hiyo.

Wakati tukio linatokea, mume wa Mariam hakuwepo nyumbani kwani usiku alikuwa akilinda mazao shambani dhidi ya wanyama waharibifu.

Jeshi la Polisi limefika eneo la tukio, kuchukua mwili wa marehemu na kumkamata Mariam kwa uchunguzi zaidi.

Tukio hili limeongeza hofu kwa wakazi wa Tarafa ya Mbugwe, kwani ni la pili ndani ya wiki moja, baada ya lile la kitongoji cha Mbugani, Kata ya Magugu, ambapo mwanaume alimuua jirani yake mbele ya watoto wake wawili wadogo kwa kumkatakata kwa panga.

Wakazi wanasema matukio haya ya mauaji miongoni mwa watu waliokuwa wakiheshimika na kuonekana wema, yanahitaji uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo chake na kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo.

Thursday, August 7, 2025

Vasco Mgimba aibuka mshindi kwenye kura za maoni Ludende

 



Aliyekuwa Diwani wa kata ya Ludende wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Ndugu Vasco Weston Mgimba ameibuka mshindi wa kura za maoni za wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata hiyo kwa ajiri ya kupata ridhaa ya kuwa diwani.

Mgimba aliyekuwa akitetea nafasi hiyo ameibuka kidedea kwa kupata kura 382 akimshinda mpinzani wake Stephano Weston Luoga aliyepata kura 11 za wajumbe ikiwa katika kata hiyo ni wajumbe wawili pekee waliokuwa wakishindania nafasi hiyo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...