Wednesday, June 25, 2025

RAIS SAMIA AMEWEKA ALAMA KWA WATUMISHI WA MAGEREZA ARUSHA, AWAGAWIA MITUNGI 528




📌Nishati safi ya kupikia ni endelevu

📌Yaelezwa ni salama na mkombozi wa mazingira

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameacha  alama mkoani Arusha kwa kugawa mitungi ya gesi 528 na majiko yake kwa watumishi wa jeshi la magereza mkoani ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama nchini. 

Hayo yamebainishwa leo Juni 25, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu wakati wa  uzinduzi wa kugawa  majiko ya gesi kwa watumishi wa magereza iliyofanyika gereza kuu mkoani Arusha. 

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  ndiye kinara wa nishati safi ya kupikia nchini ambaye anaendelea kuhamasisha taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi na salama," Amesema. 

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuhamasisha na kuwataka watanzania wote kuhakikisha wanatumia nishati safi ya kupikia kama njia mahususi ya kutunza na kulinda mazingira na pia kuokoa uharibifu wa misitu

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amewaeleza watumishi wa magereza kuwa nishati safi ni salama kwa Taifa kwa kuwa inaondoa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo safi na salama ya kuni na mkaa

"Ndugu zangu watumishi wenzangu, nawasihi sana kutumia nishati safi na salama katika matumizi yenu kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi ili kila mtanzania atumie nishati safi ya kupikia kuliko kutumia kuni na mkaa," Ameongeza Mha. Saidy.

Akizungumzia kuhusu Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati safi ya kupikia ameeleza kuwa, lengo kuu la mkakati huo ni kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na malengo mengine mahususi ni kuandaa na kutekeleza kampeni maalum za uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi. 

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Magereza mkoa wa Arusha, ACP Prosper Kapinga ameipongeza REA kwa tukio hilo muhimu la kugawa mtungi wa gesi na majiko ya sahani mbili na kusema kuwa inaonesha kwa vitendo juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia Nishati Safi ya Kupikia.

Source

Wakulima Babati Wavutwa Kulima Karanga Baada ya Utafiti wa TARI


Na John Walter -Babati 

Wakulima wa Wilaya ya Babati, hususan wa ukanda wa Mbugwe mkoani Manyara, wameonyesha mwitikio mkubwa katika kulima zao la karanga kufuatia utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha Naliendele.

Utafiti huo umebainisha kuwa mazingira ya eneo hilo yanafaa kwa kilimo cha karanga na kwamba zao hilo lina soko la uhakika, hatua ambayo imewapa matumaini wakulima na kuchochea hamasa ya kulima kwa tija.

Mtafiti kutoka TARI Naliendele, Bw. Anthony Bujiku, amesema Tanzania ipo katika nafasi nzuri kwenye uzalishaji wa karanga ukilinganisha na mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ameeleza kuwa Tanzania ina takribani hekta milioni tatu zenye rutuba zinazofaa kwa kilimo cha karanga, lakini kwa sasa ni hekta milioni moja na nusu pekee ndizo zinazotumika.

"Tunayo ardhi ya kutosha na mbegu bora, hivyo tunawahimiza wakulima watumie mbegu zilizofanyiwa utafiti ili kuongeza tija," amesema Bw. Bujiku.

Mkulima kutoka Kijiji cha Kiru, Jitu Vrajilal Son, ambaye shamba lake limehusika moja kwa moja kwenye utafiti wa mbegu bora za karanga, amesema kuwa TARI imekuwa mkombozi mkubwa kwao.

 "Tulikuwa tukipanda kienyeji, lakini sasa tunatumia mbegu bora na teknolojia ya kisasa, matokeo ni mazuri na ya kutia moyo," amesema kwa furaha.

Wakulima wengine waliopata nafasi ya kushiriki kwenye mafunzo na majaribio ya kilimo hicho wamesema utafiti uliofanywa na TARI umewapa matumaini makubwa na wameiomba Serikali kuendeleza utafiti kama huo kwenye mazao mengine pia, ili kuinua kilimo kwa ujumla.

Serikali kupitia wizara husika inaendelea kutuma wataalamu wake katika maeneo mbalimbali ili kufanya tafiti zaidi kuhusu zao hilo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji na kuhakikisha wakulima wanapata mazao yenye tija na soko la uhakika.

Kwa hatua hii, Babati inaelekea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya uzalishaji wa karanga nchini, na mfano wa kuigwa kwa maeneo mengine ya Tanzania.

TRA SHINYANGA YATOA ELIMU YA KODI KWA WANACHUO CHA UFUNDI STADI VETA


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga imeendesha semina ya elimu ya ulipaji kodi kwa wanachuo wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uelewa vijana kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.

Semina hiyo imefanyika leo Juni 25, 2025 katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga kilichopo manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza wakati wa semina hiyo, Afisa wa kodi kutoka TRA Shinyanga Semeni Mbeshi, amesema lengo ni kuwajengea msingi mzuri wa kizalendo vijana wanaotarajia kuingia kwenye soko la ajira na kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.

Ameongeza kuwa elimu hiyo ni endelevu na inalenga kujenga taifa la watu waaminifu katika ulipaji wa kodi, huku akisisitiza matumizi ya IFD kwa wafanyabiashara na kutoa na kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa.

"Haki ya mlipa kodi ni kuaminiwa pindi anapofika kwenye ofisi za TRA kwa ajili ya kufanyiwa makadilio yanayoendana na biashara yake, ni wajibu wa kila mfanyabiashara kutoa taarifa ya ufanyaji wa biashara kwa mamlaka ya mapato TRA, utoaji wa risiti za IFD zinasaidia kuweka rekodi sahihi ya kumbukumbu ya biashara kwa muda wa miaka 5, lakini kodi hiyo inakwenda moja kwa moja kwenye mfuko wa serikali na kuwezesha maendeleo kwenye taifa letu", amesema Semeni Mbeshi.

Kwa upande wake, Mkufunzi katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga, Emili Shirima amesema vitendo vya baadhi ya watu kutumia vishoka kujipatia huduma za kikodi si sahihi na ni hatari kwa uchumi wa taifa, alisema na kuwataka wanachuo kujiepusha na tabia hizo mara watakapoingia kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Baadhi ya wanachuo walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru TRA kwa kuwapa elimu hiyo muhimu, wakisema itawasaidia  mara baada ya kuhitimu na kuanzisha biashara au shughuli za kujitegemea na kuo ngeza kuwa sasa anaelewa kwamba ulipaji wa kodi unasaidia huduma za jamii kama afya, elimu na miundombinu.

Afisa wa kodi kutoka TRA Shinyanga Semeni Mbeshi akizungumza wakati wa mafunzo hayo.






Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo.































 

Tuesday, June 24, 2025

SERIKALI YAZIDI KUHAMASISHA NISHATI SAFI, YATOA MITUNGI 225 KWA WATUMISHI GEREZA KUU MAWENI



📌Shilingi bilioni 35 kupeleka nishati safi magereza yote nchini

📌Mitungi ya gesi 653 kupatiwa watumishi magereza Tanga

📌Mha. Saidy asisitiza uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi wa magereza na wananchi ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 – 2034).

Hayo yamebainishwa leo Juni 24, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu wakati wa uzinduzi wa kugawa majiko ya gesi kwa watumishi wa magereza iliyofanyika Gereza Kuu la Maweni jijini Tanga. 

"Hii yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 zihame kutoka katika matumizi ya nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia, " Ameongeza. 

Vile vile ameongeza kuwa, Magereza yote ya mkoa wa Tanga tayari yanatumia makaa ya mawe ya Rafiki Briquette unaozalishwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). 

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mha. Hassan Saidy amewataka watumishi wa magereza kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu matumizi na umuhimu wa nishati safi ya kupikia ili kuifanya nishati hiyo kuwa endelevu, pia ni chachu kwa wananchi katika kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa.

Amesema kuwa, gharama ya mradi wote ni zaidi ya shilingi Bilioni 35.2 ambapo Wakala wa Nishati Vijijini unatoa ruzuku ya shiling bilioni 26.5 Sawa na asilimia 75.4 ya gharama ili kuwezesha utekelezaji wake.

Kwa upande wake, ACP Nade Baynit, Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga ameishukuru REA kwa kuwezesha watumishi magereza kutumia nishati safi ya kupikia. Aidha, amewakata watumishi hao kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa na REA kwa watumishi wa magereza kwa kujipatia mtungi wa gesi na majiko ya gesi ya sahani mbili  bure na waeendelee kuwa mabalozi wa nishati hiyo kwa wananchi.

Naye, Mratibu wa nishati safi kutoka kampuni ya Lake Gas Ltd Bw. Ramadhani Siasa amesema watatekeleza mradi huo kwa kuzingatia makubaliano ya Mkataba wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia pamoja na kutoa elimu, kuhamasisha wananchi ili kuchochea matumizi ya nishati hiyo.









FOUNDATION FOR DISABILITY HOPE YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU, YAISHUKURU STAMICO




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Shirika la Foundation for Disability Hope limeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna linavyowajali na kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli za maendeleo, likieleza kuwa hatua hiyo imeleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa kundi hilo.

Akizungumza Juni 24, 2025 jijini Dodoma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mitambo ya wachimbaji wadogo na vitendea kazi vya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mkurugenzi wa shirika hilo, Michael Salali, amesema ushirikiano mzuri kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na shirika hilo umeongeza imani na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya taifa.

"Tumejionea wenyewe jinsi Serikali inavyotupa kipaumbele kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu,Siku hizi watu wenye ulemavu wanajihusisha na biashara, kilimo na sasa nishati mbadala,haya ni mafanikio ambayo miaka ya nyuma yalionekana kama ndoto," amesema Salali.

Salali pia ametoa shukrani kwa Shirika hilo la madini la Taifa kwa kushirikiana na Shirika lake katika utekelezaji wa mradi wa duka la kuuza mkaa mbadala, ambao unalenga kusaidia watu wenye ulemavu kupata ajira na kukuza matumizi ya nishati safi, salama kwa afya na mazingira.

Amesema mradi huo unatoa fursa kwa watu wenye ulemavu kujitegemea, sambamba na kuwa sehemu ya juhudi za taifa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

"Sisi kama Foundation for Disability Hope, tunajivunia kuwa sehemu ya harakati za Nishati safi, na tunahitaji kuungwa mkono zaidi," amesisitiza.

"STAMICO wamekuwa nguzo kubwa katika kutuwezesha kufanikisha mradi huu,Wametupatia nyavu za uvuvi ambazo ni vifaa kazi, na kutuwezesha pia kupata nishati safi," ameeleza kwa msisitizo.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt.Venance Mwasse amethibitisha kuwa msaada wao kwa watu wenye ulemavu, hususan wenye Ualbino, ni sehemu ya mkakati wa shirika huo kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kujikwamua kiuchumi.

"Kutokana na wao kuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi, tuliona ni vyema kuwapatia nyavu za uvuvi ambazo ni nishati safi kwa matumizi ya nyumbani ili wajitegemee," amesema mwakilishi wa shirika hilo.

STAMICO imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na mashirika kama Foundation for Disability Hope na Taasisi nyingine kuhakikisha kuwa watu wote wanapata fursa sawa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za serikaki katika matumizi ya Nishati safi.

Monday, June 23, 2025

WAZIRI MKUU AZINDUA RASMI MFUMO WA KUBADILISHANA TAARIFA SERIKALINI (GovESB)




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), amezindua rasmi Mfumo wa Kubadilishana Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus – GovESB) kwa kutumia kishikwambi, katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2025, yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Uzinduzi huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya utoaji wa huduma serikalini, ukilenga kuhakikisha Taasisi zote za umma nchini zinaweza kusoma na kubadilishana taarifa kwa njia ya kidijitali, kwa haraka, usahihi na kwa gharama nafuu.

Mfumo huo umesanifiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa mujibu wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.

Lengo kuu la mfumo wa GovESB ni kuimarisha mawasiliano kati ya mifumo ya Serikali kwa njia ya kisasa ili kuongeza uwazi, ufanisi, urahisi wa huduma, na kupunguza urasimu kwa wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

"Mfumo huu utaondoa urudufu wa kazi, kuongeza kasi ya utoaji huduma na kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa taasisi husika bila kuchelewesha haki ya mwananchi," amesisitiza Majaliwa wakati wa uzinduzi.

Aidha Waziri Mkuu amezitaka Taasisi zote za Serikali ambazo bado hazijajiunga na mfumo huo kuhakikisha zinafanya hivyo kufikia Julai 30, 2025, kama alivyoagiza awali, ili kuhakikisha Serikali inakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani.

TAMKO ZITO LA CCM KUELEKEA ZOEZI LA KUCHUKUA FOMU, UCHUJAJI NA UTEUZI WAGOMBEA

Dodoma, Juni 23, 2025

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kusitishwa kwa mikutano, ziara, semina na makongamano yote yanayohusisha wajumbe wa vikao vya UCHUJAJI na UTEUZI wa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani hadi baada ya kupiga kura za maoni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, chama hicho kinaendelea na maandalizi ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wanachama watakaowania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kupitia CCM.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mchakato huo utafanyika kwa hatua, ikiwemo uchukuaji na urejeshaji wa fomu, vikao vya awali na hatimaye kura za maoni. Hivyo, chama kimeagiza kusitishwa kwa shughuli zozote zinazohusiana na vikao vya uteuzi kabla ya hatua ya kura za maoni.

"Ni kwa kuzingatia hilo, CCM inasisitiza marufuku ya ZIARA, MIKUTANO, SEMINA na MAKONGAMANO yanayohusisha wajumbe wa vikao vinavyopiga kura za maoni kuhusiana na wagombea wa ngazi zote hadi kura za maoni zitakapopigwa," imesisitizwa kwenye taarifa hiyo.

Aidha, CCM imeonya wanachama wote wanaotarajia kugombea au wawakilishi wao dhidi ya kufanya vitendo vyovyote vinavyoweza kuashiria ukiukwaji wa Katiba, kanuni au miongozo ya chama hicho.

Chama hicho pia kimewataka viongozi, watendaji na wanachama wake kusimamia nidhamu, maadili na mshikamano katika kipindi hiki muhimu cha maandalizi ya uchaguzi. Viongozi wote wametakiwa kuhakikisha kuwa michakato yote inaendeshwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amehitimisha taarifa hiyo kwa kuwataka wanachama wote kutimiza wajibu wao katika kuimarisha umoja ndani ya chama na kudumisha imani ya wananchi waliyopewa na CCM.

Kidumu Chama Cha Mapinduzi!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...