Monday, June 23, 2025

WAZIRI MKUU AZINDUA RASMI MFUMO WA KUBADILISHANA TAARIFA SERIKALINI (GovESB)




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), amezindua rasmi Mfumo wa Kubadilishana Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus – GovESB) kwa kutumia kishikwambi, katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2025, yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Uzinduzi huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya utoaji wa huduma serikalini, ukilenga kuhakikisha Taasisi zote za umma nchini zinaweza kusoma na kubadilishana taarifa kwa njia ya kidijitali, kwa haraka, usahihi na kwa gharama nafuu.

Mfumo huo umesanifiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa mujibu wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.

Lengo kuu la mfumo wa GovESB ni kuimarisha mawasiliano kati ya mifumo ya Serikali kwa njia ya kisasa ili kuongeza uwazi, ufanisi, urahisi wa huduma, na kupunguza urasimu kwa wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

"Mfumo huu utaondoa urudufu wa kazi, kuongeza kasi ya utoaji huduma na kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa taasisi husika bila kuchelewesha haki ya mwananchi," amesisitiza Majaliwa wakati wa uzinduzi.

Aidha Waziri Mkuu amezitaka Taasisi zote za Serikali ambazo bado hazijajiunga na mfumo huo kuhakikisha zinafanya hivyo kufikia Julai 30, 2025, kama alivyoagiza awali, ili kuhakikisha Serikali inakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...