Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Shirika la Foundation for Disability Hope limeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna linavyowajali na kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli za maendeleo, likieleza kuwa hatua hiyo imeleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa kundi hilo.
Akizungumza Juni 24, 2025 jijini Dodoma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mitambo ya wachimbaji wadogo na vitendea kazi vya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mkurugenzi wa shirika hilo, Michael Salali, amesema ushirikiano mzuri kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na shirika hilo umeongeza imani na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya taifa.
"Tumejionea wenyewe jinsi Serikali inavyotupa kipaumbele kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu,Siku hizi watu wenye ulemavu wanajihusisha na biashara, kilimo na sasa nishati mbadala,haya ni mafanikio ambayo miaka ya nyuma yalionekana kama ndoto," amesema Salali.
Salali pia ametoa shukrani kwa Shirika hilo la madini la Taifa kwa kushirikiana na Shirika lake katika utekelezaji wa mradi wa duka la kuuza mkaa mbadala, ambao unalenga kusaidia watu wenye ulemavu kupata ajira na kukuza matumizi ya nishati safi, salama kwa afya na mazingira.
Amesema mradi huo unatoa fursa kwa watu wenye ulemavu kujitegemea, sambamba na kuwa sehemu ya juhudi za taifa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
"Sisi kama Foundation for Disability Hope, tunajivunia kuwa sehemu ya harakati za Nishati safi, na tunahitaji kuungwa mkono zaidi," amesisitiza.
"STAMICO wamekuwa nguzo kubwa katika kutuwezesha kufanikisha mradi huu,Wametupatia nyavu za uvuvi ambazo ni vifaa kazi, na kutuwezesha pia kupata nishati safi," ameeleza kwa msisitizo.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt.Venance Mwasse amethibitisha kuwa msaada wao kwa watu wenye ulemavu, hususan wenye Ualbino, ni sehemu ya mkakati wa shirika huo kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kujikwamua kiuchumi.
"Kutokana na wao kuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi, tuliona ni vyema kuwapatia nyavu za uvuvi ambazo ni nishati safi kwa matumizi ya nyumbani ili wajitegemee," amesema mwakilishi wa shirika hilo.
STAMICO imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na mashirika kama Foundation for Disability Hope na Taasisi nyingine kuhakikisha kuwa watu wote wanapata fursa sawa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za serikaki katika matumizi ya Nishati safi.