Monday, March 3, 2025

KATAMBI AKEMEA WATUMISHI WA SERIKALI KUPANDISHA MABEGA




Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu,amekemea baadhi ya Watumishi wa Serikali kupandisha Mabega na kutoa huduma mbovu kwa wananchi.

Amebainisha hayo leo Marchi 2,2025 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kambarage kwenye mkutano wa hadhara, wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Amesema kwenye maeneo ya kutolea huduma za wananchi,yamekuwa yakilalamikiwa sana na wananchi kuwa na huduma mbovu,kutokana na baadhi ya Watumishi kupandisha Mabega.
"Kwenye mikutano yangu nimekuwa nikipokea kuwapo kwa huduma mbaya kwenye hospitali zetu, na leo nimepokea tena malalamiko katika shule ya Msingi Kambarage, nawaomba Watumishi wa Serikali fanyeni kazi kwa uaminifu msipandishe Mabega kwa wananchi wahudumieni vizuri,"amesema Katambi.


"Watumishi wenye lugha chafu kwa wananchi,na wapandisha Mabega hatuwataki hapa Shinyanga,Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anahangaika kutafuta fedha kuboresha huduma za afya na elimu, lakini kuna Watumishi wachache wanataka kumkwamisha hilo sikubaliani nalo,"ameongeza.
Aidha,akizungumzia mambo ya maendeleo kwenye Kata hiyo ya Kambarage,kuwa wameboresha huduma za Afya katika kituo cha Afya Kambarage, ikiwamo upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na sasa wanajenga uzio.


Amesema pia kwa sasa ujenzi unaendelea wa barabara kiwango cha Lami kwenye Kituo hicho cha Afya Kambarage na pia hivi karibuni watajenga Soko kubwa la kisasa.
Awali wananchi wa Kambarage wakiwasilisha kero kwa Mbunge Katambi,akiwamo Suzana Balele wamelalamikia Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kambarage, kuwa ana nyanyasa wazazi kwa kuwatolea lugha chafu,pamoja na kuwaambia wahamishe watoto katika shule nyingine kuwa shule imejaa na wakitaka kumpatia ushauri ana waambia wasimfundishe kazi.


Mwananchi Mwingine Pili Shija,amelalamikia wazazi wanapokwenda kujifungua kwenye Kituo cha Afya Kambarage, hua wanatozwa pesa kuanzia sh.300,000 mpka 600,000 kwa wale wa huduma za upasuaji,na wakati serikali ilishasema huduma za uzazi ni bure.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Peres Kamugisha,awali akitoa majibu kwenye mkutano huo, amekiri kwamba huduma uzazi ni bure na kwamba hata yeye ameshitushwa kusikia wanatozwa pesa na kwamba atalifuatilia.


Akijibu juu ya Malalamiko ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kambarage nalo amesema atalifuatilia sababu lipo kinidhamu zaidi na siku ya jumanne atampatia majibu Mbunge katika juu ya hatua ambayo itachukuliwa.
Mbunge Katambi ameendelea na ziara yake ya Kata kwa Kata, ambapo leo alikuwa Kata ya Lubaga na Kambarage, kesho atakuwa Kata ya Ndala na Masekelo.


TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu akizungumza na wananchi wa Kata ya Kambarage.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Peres Kamugisha akitoa majibu kwenye mkutano kujibu kero za wananchi.
Wananchi wakiuliza maswali na kutoa kero zao.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...