Sunday, June 27, 2021

Tahadhari vikundi vya ushirika kutosajiliwa

 


Vikundi vya ushirika vya  akiba na kukopeshana vimetakiwa  kujisajili kwa mujibu wa sheria ndogo ya huduma za fedha namba 10 ya mwaka 2018 ili kuendesha shughuli zao kwa weledi.


Vimeelezwa kuwa bila kufanya hivyo vitakuwa katika  hatari ya kukamatwa kwa makosa ya utakatishaji fedha au uhujumu uchumi.


Hayo yameelezwa na mkuu wa Mkoa wa Morogoro,  Martine Shighela wakati akizindua jukwaa la kwanza la ushirika  mkoani humo  lililohusisha wanaushirika wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vya ushirika ikiwemo ushirika wa mazao, ushirika wa kuweka na kukopa, ushirika wa viwanda, walaji, ufugaji na miradi ya pamoja ya  huduma.


Shigela amesema kuna  vyama vingi vya ushirika lakini havifuati sheria, kanuni wala taratibu na pindi vinapopata tatizo kusaidia inakuwa shida.


"Uwepo wa ushirika wenye kufuta sheria kunasaidia kupata mikopo na mitaji kwa urahisi kutoka kwenye taasisi na asasi za kifedha," amesema mkuu huyo wa mkoa.


Shigella aliaikitishwa namna vyama vya ushirika vinavyotambuliwa kutokuwa na maghala ya kuhifadhi mazao ya wakulimai, kuwataka warajisi wa vyama vya ushirika wa wilaya na mkoa kuanza safari ya kuhakikisha vyama vya msingi hasa vya mazao vinaanza mchakato wa kujenga maghala.


"Tuangalie vyama viko maeneo gani, vinafanya shughuli gani, vina wanachama kiasi gani na je vinapotaka kuwasaidia wakulima kwenye masoko vinatumia utaratibu gani na vinahifadhi sehemu moja ama kwa kutumia maghara ya watu binafsi ama wanunuzi wanashindanishwaje," ameelekeza.


Mwenyekiti wa jukwaa la ushirika Mkoa wa Morogoro,   Iddi Bilali amesema hadi sasa  vyama 60 vimeomba leseni kwenye mfumo na 21 vimeshapata huku 39 vikisubiri mchakato toka tume ya maendeleo ya ushirika.


Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Morogoro, Kenneth Shemdoe licha ya kubainisha kutokuwa na  mfumo mzuri na wa uhakika wa uuzaji mazao, alieleza namna ofisi hiyo ilivyofanikisha utatuzi wa migogoromingi akisema ni ya kurithi kutokana na awali vyama vingi kuendeshwa kinyume na sheria.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...