Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amewasili leo katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Ziara ya Al-Sisi nchini Iraq ni sehemu ya mkutano wa kilele kati ya Misri, Jordan na Iraq unaonuiwa kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama, uchumi, biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo tatu ya kiarabu.
Al-sisi anakuwa mkuu wa kwanza wa dola la Misri kuzuru Iraq tangu hayati Saddam Hussein kuivamia Kuwait mwaka 1990 na kuvuruga kabisa mahusiano ya kidplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Mahusiano kati ya Misri na Iraq yamekuwa yakiboreka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni huku maafisa wa ngazi za juu wa pande zote mbili wakitembeleana.