UONGOZI wa Yanga umesema kuwa uamuzi wa kumpa timu kocha wao Juma Mwambusi mpaka mwishoni mwa msimu, umepunguza presha kubwa waliyokuwa nayo katika mchakato wa kumtangaza kocha mpya atakayekuja kufundisha kikosi hicho.
Yanga ipo kwenye mchakato wa kumtangaza kocha mpya atakayekuja kuchukua nafasi ya kocha Mrundi, Cedric Kaze aliyetimuliwa Machi 7, mwaka huu, ambapo Mfaransa, Sebastian Migne anatajwa kuwa kwenye nafasi kubwa ya kutwaa mikoba hiyo.
Mpaka Ligi Kuu Bara inasimama kupisha ratiba ya michezo ya kimataifa, Yanga imesalia kuwa vinara wa msimamo ambapo wamecheza mechi 23 na kukusanya pointi 50.Akizungumza na Championi Jumatatu, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa alisema:
"Uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na kamati yake ya ufundi unaendelea na mchakato wa kufanya upembuzi wa wasifu (CV), za makocha ambao waliwasilisha maombi ya kazi kufuatia kuondolewa kwa aliyekuwa kocha wetu Cedric Kaze.
"Tunatarajia kuweka wazi jina la kocha mkuu hivi karibuni, lakini kabla ya kufikia maamuzi ya kumpa timu kocha Mwambusi, kama uongozi tulikuwa na presha kubwa sana ya kusaka kocha mpya ili kuziba nafasi ya Kaze.
"Lakini kwa sasa mchakato huo hauna presha kubwa kwa kuwa tuna imani kubwa na kocha Mwambusi, na ndiyo maana tumekubaliana kumpa timu mpaka mwishoni mwa msimu."
STORI: JOEL THOMAS,Dar es Salaam