Nchi za Ulaya zimesema Shirika la Afya Ulimwenguni WHO linastahili kuwa na nguvu ya kuchunguza kwa uhuru milipuko ya magonjwa na pia kuweza kuzilazimisha nchi kutoa data zaidi.
Wito huo umetolewa baada ya kutokea janga kubwa la virusi vya corona ambalo limewezesha kuonyesha mapungufu katika shirika hilo.
Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema WHO inapaswa kuungwa mkono zaidi kisiasa na kifedha kutokana na juhudi zake za kusimamia migogoro ya kiafya.
Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetoa mapendekezo kadhaa ya kulirekebisha shirika hilo la afya duniani. Wakati huo huo mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema wataalam wa Shirika hilo walilijadili janga la corona hapo jana katika mkutano na wenzao wa China.