Raia wa Ivory Coast leo wameshiriki katika zoezi la kupiga kura. Taarifa zaidi zinafahamisha kwamba baadhi ya wafuasi wa upinzani walijaribu kuvuruga kura hiyo hatua inayochukuliwa kuwa walifuata wito kutoka kwa wagombeaji wawili wanaompinga rais Alassane Ouattara uliowataka raia kususia uchaguzi huo ambapo kiongozi huyo anawania muhula wa tatu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters barabara za mji mkuu wa kibiashara Abidjan zilikuwa na kimya bila watu tofauti na wakati mwingine ambapo zilikuwa zinakumbwa na vurugu uchaguzi.
Ouattara amesema anagombea tena chini ya katiba mpya iliyoidhinishwa mnamo mwaka 2016, na anafanya hivyo kwa sababu mgombea aliyechaguliwa na chama chake alifariki ghafla mnamo mwezi Julai. Kiongozi huyo anatarajiwa kushinda.