Wednesday, April 29, 2020

Rais Museveni “Dereva wa lori awe mmoja na asilale hotelini wala kwa mtu”



Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza hatua mpya za kudhibiti mienendo ya madereva wa malori yanayoingia nchini humo kutoka mataifa jirani baada ya zaidi ya madereva 20 kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Mataifa ya Uganda na Kenya yamekuwa yakiwafanyia vipimo wa virusi vya corona madereva wa malori katika mipaka yao hali ambayo imesababisha foleni ndefu ya magari hayo yaliopiga foleni ndefu

Madereva na wasaidizi wao upande wa Kenya wamelalamikia jinsi walivyosubiri kwa siku kadhaa kufanyiwa vipimo vya Covid-19 kabla ya kuruhusiwa kuvuka mpaka wa kuingia Uganda.

Njia ya usafirishaji mizigo kutoka bandari ya Mombasa nchini Kenya ni muhimu sana katika usafirishaji wa bidhaa muhimu kama vile chakula na dawa hadi Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemocrasia ya Congo.

Lakini wasafirishaji wa mizigo hiyo sasa wanahofiwa huenda wakaeneza virusi vya corona katika kanda ya Afrika Mashariki.

Sasa Rais Museveni anasema hatua zaidi zitachukuliwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua hizo ni pamoja na kila lori kuwa na mtu mmoja – dereva pekee yake ambaye hataruhusiwa kulala hotelini wala nyumbani kwa watu.

Bw. Museveni pia amesema mienendo ya madereva hao itachunguzwa

Katika hotuba yake kwa taifa usiku wa Jumanne Rais Museveni pia aliangazia kuongezeka kwa chuki dhidi ya madereva hao kutoka kwa baadhi Waganda ambao wanahofia wataleta maambukizi ya corona niching humo.

Museveni aliongeza kwamba kusitisha usafirishaji wa bidhaa itakuwa na athari kubwa lakini alikubali kuwa madereva hao ni tishio katika mapambano ya nchi hiyo dhidi ya corona ikitoa mfano wa janga la Ukimwi la miaka ya 1980 na miaka ya tisini wakati ambapo madereva wa malori katika kanda hiyo waliaambukiza watu virus vya HIV katika kila miji waliyopitia wakiwa safarini.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...