Na Veronica Kazimoto
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewafikia na kuwaelimisha wafanyabiashara zaidi ya 700 kupitia kampeni ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyofanyika mkoani Morogoro.
Lengo la kampeni hiyo ilikuwa ni kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na maoni kutoka kwa wafanyabiashara hao.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, Afisa Msimamizi wa Kodi Mkuu wa TRA, Julius Mjenga amesema kuwa, mamlaka hiyo ililenga kuwafikia wafanyabiasha 500 lakini kutokana na mwitikio mkubwa, TRA imefanikiwa kuvuka lengo hilo na kuwafikia zaidi ya 700.
"Wiki hii moja ya elimu kwa mlipakodi, tuliwalenga wafanyabiashara wa wilayani ambapo kumekuwa na changamoto ya kutokupata elimu ya kodi kwa wakati. Nashukuru tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu tumeweza kuwaelimisha wafanyabiashara 774 katika kampeni hii", alisema Mjenga.
Mjenga ameongeza kuwa "Tumefika karibu wilaya zote za mkoa huu wa Morogoro ambazo ni Malinyi, Ulanga, Kilosa, Mvomero, Kilombero na Gairo na kila mahali tulipopita tumepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi mbalimbali."
Kwa upande wa wafanyabiashara waliotembelewa na TRA, wameishukuru mamlaka hiyo kwa kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi na kuomba elimu hiyo iwe endelevu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema kuwa, TRA ya sasa sio ile ya zamani kwa sababu sasa hivi maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wamekuwa karibu na walipakodi na siku hizi hawana tabia ya kufunga biashara zao.
"Zamani mtu alikuwa akisikia watu wa TRA wanakuja, anafunga duka anaondoka lakini siku hizi, TRA wamekuwa marafiki, wanatuelimisha na wala hawafungi biashara zetu, kwakweli tunashukuru sana," alisema Eleonora Kisimba, mfanyabiashara wa duka la nguo wa wilayani Mvomero.
Naye Stanphord Mjumbe ambaye ni mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi wilayani Gairo mkoani hapa alisema kuwa, kampeni ya elimu kwa mlipakodi ifanyike mara kwa mara kwa sababu wafanyabiashara walio wengi hususani wadogo hawajasoma hivyo wanahitaji kuelimishwa zaidi juu ya haki na wajibu wao katika ulipaji kodi.
"Sisi wafanyabiashara wadogo, tulio wengi hatujasoma hivyo tunahitaji elimu hii angalau kwa mwaka mara tatu ili tuweze kuelewa kwa kina haya mambo ya ulipaji kodi maana wakati mwingine tunakuwa hatujui haki zetu," alisisitiza Mjumbe.
Aidha, wafanyabiashara hao wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania kurejesha Kodi ya Zuio kwa wamiliki wa majengo kwa kuwa baadhi yao hawataki wapangaji kuzuia asimilia kumi na kuiwasilisha TRA.
Vilevile, wameomba kuelimishwa jinsi ya kulipa kodi ya mapato kwa awamu mara tu wanapokadiriwa kodi hususani kwa wafanyabiashara wapya kwani wengi wao wanapitiliza tarehe za kulipa kodi hiyo kwa kukosa uelewa.
Kampeni ya huduma na elimu kwa mlipakodi imemalizika tarehe 17 Novemba, 2019 na ilifanyika katika Mikoa ya Morogoro na Pwani ambapo wafanyabiashara wamepata fursa ya kutembelewa katika maduka yao na wengine walihudhuria semina kwa ajili ya kuelimishwa masuala mbalimbali yanayohusu kodi.
Mwisho.