Monday, September 3, 2018

Serikali yapanga kuigomea Kenya kutumia Mto Mara


Serikali ya Tanzania imesema itapinga mipango ya serikali ya Kenya kujenga mabwawa ya kuzalisha umeme na kilimo cha umwagiliaji kwenye Mto Mara.

Kwa mujibu wa waziri wa mazingira wa Tanzania, January Makamba iwapo mipango hiyo ya Kenya itatekelezwa, itapunguza mtiririko wa maji na kutishia ustawi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mto Mara unaanzia nchini Kenya kwenye milima ya Mau na kutiririka mpaka Tanzania ambako unatengeneza sehemu ya mpaka wa nchi hizo mbili. Mto Mara pia unatenganisha Hifadhi za Taifa za Masai Mara ya Kenya na Serengeti ya Tanzania.

Ni katika Mto Mara pia ambapo Nyumbu huvuka kwa wingi kutoka upande wa Tanzania kwenda Kenya na kuvutia maelfu ya watalii kwenye mbuga za Serengeti na Masai Mara kushuhudia tukio hilo ambalo linatajwa kama moja ya kivutio cha asili cha dunia.

"…Mto Mara, unaoanzia Kenya, ni mhimili wa Hifadhi ya Serengeti. Kulikuwa na taarifa za mipango ya Kenya kujenga mabwawa. Tulituma timu ya wataalam kufuatilia. Tuna Protocol ya Mto Mara, pia Lake Victoria Basin. Nitaenda Kenya na wenzangu kuongea na ndugu zetu," ameandika Makamba kwenye mtandao wake wa Twitter.

Ujumbe huo wa Twitter pia umeambatana na video ambayo inamwonesha Makamba akizuru kando ya Mto Mara ambapo amesema, "... Hii rasilimali (Mto Mara) ni ya kwetu sote, na sisi kama nchi hatuwezi kuruhusu jambo ambalo linaweza kuhujumu uchumi. Serengeti ni moja ya mali kubwa sana ya nchi yetu, na uti wa mgongo ni huu mto na ukiuvuruga huu mto kama nchi hatuwezi kukubali."

"Hairuhusiwi wewe mto unatoka nchi moja kwenda nyengine basi wewe (wa nchi ya) kule juu kufanya chochote maji yasifike huku chini. Kuna mikataba ya kimataifa tuliyosaini na tutasimama katika hiyo," amesema Makamba.

Sakata la Mto Mara linakuja siku chache baada ya vyombo vya habari nchini Kenya kuripoti kuwa mamlaka za hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania zimefanya hujuma kwa kuchoma moto eneo la hifadhi ili kuzuia nyumbu kuvuka kuelekea nchini Kenya. Serikali ya Tanzania ilikanusha tuhuma hizo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...