Monday, February 16, 2026

Picha : SHANGWE ZATAWALA KIKUNDI CHA 'BETTER TOGETHER' KIKIZINDULIWA KWA KISHINDO, DC MTATIRO ATAKA MSHIKAMANO ZAIDI


 Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together Mussa Ngangala akikata keki wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameongoza uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika hafla iliyogubikwa na shamrashamra, nderemo na vifijo vya wanachama waliojaa matumaini na mshikamano huku akikipongeza kikundi hicho kwa maono yake ya kuimarisha umoja, ustawi wa kijamii na kukuza maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa wanachama wake.

Uzinduzi huo ulifanyika tarehe Februari 14, 2026 ulitanguliwa na shughuli za kijamii na kiafya zikiwemo mbio za amani (jogging) zilizoanzia Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuhitimishwa katika Uwanja wa CCM Kambarage, sambamba na mazoezi ya viungo (aerobic na cardio). 

Wanachama pia walitembelea Kituo cha Afya Kambarage na kutoa matendo ya huruma kwa wagonjwa na wahitaji, kabla ya kuhitimisha siku hiyo kwa sherehe rasmi ya uzinduzi jioni katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mtatiro alisema kuwa vikundi vya kijamii kama Better Together vina mchango mkubwa katika kuimarisha mtaji wa kijamii, kusaidiana wakati wa changamoto na kujenga utamaduni wa uwajibikaji.

"Nawapongeza sana waanzilishi na wanachama wa Better Together kwa maono yenu. Kuanzisha na kuendesha kikundi chenye wanachama zaidi ya 400 ndani ya muda mfupi ni ishara ya uongozi makini na imani ya watu. Serikali inaamini katika nguvu ya umoja wa wananchi. Endeleeni kushikamana, kudumisha nidhamu ya fedha na uwazi ili kikundi chenu kiwe mfano bora wa kuigwa," alisema Mtatiro.
Aliongeza kuwa, vikundi vinapojengwa katika misingi ya uaminifu, husaidia kupunguza mzigo wa kijamii kwa familia na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya chini.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together, Mussa Jonas Ngangala, alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika safari ya kuimarisha taasisi yao na kuongeza wigo wa huduma kwa wanachama.

"Tulianza kama wazo la kuinuana katika changamoto za maisha, lakini leo tumekuwa familia kubwa yenye wanachama zaidi ya 400. Dhamira yetu ni kujenga mfumo imara wa kusaidiana kijamii na kiuchumi, kuhakikisha kila mwanachama anahisi kuthaminiwa na kulindwa katika nyakati za shida na furaha," alisema Ngangala.

Alibainisha kuwa kikundi kitaendelea kuandaa programu za kijamii, kuhamasisha utunzaji wa afya, pamoja na kuendeleza utamaduni wa kuchangia na kusaidiana kwa uwazi na uwajibikaji.
Better Together ni muunganiko wa wanachama zaidi ya 400, wengi wao wakiishi Mkoa wa Shinyanga huku wengine wakitoka nje ya mkoa huo. Kikundi hicho kilianzishwa mwezi Oktoba 2025 kwa lengo la kusaidiana katika nyakati za shida na raha, pamoja na kufanya matendo ya huruma katika jamii.

Katika hafla hiyo, wanachama pia walifanya harambee ya kuchangia mfuko wa kikundi ili kuimarisha uwezo wake wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi zaidi mwaka 2026.

Uzinduzi wa Better Together umeweka msingi wa kuendelea kujenga mshikamano, kuimarisha mtandao wa kijamii na kukuza ustawi wa wanachama wake, huku ukiwa mfano wa namna vikundi vya kijamii vinavyoweza kuwa chachu ya maendeleo katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga
 Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together Mussa Ngangala akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga
 Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together Mussa Ngangala (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga
 Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together Mussa Ngangala (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga



























































































































Saturday, January 31, 2026

Bilioni 24.9 kupeleka umeme vitongoji 218 Mkoani Njombe,REA Wamtambulisha Mkandarasi



📍Njombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ameelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobakia nchini ambavyo bado havina huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa leo Januari 30, 2026 na Frank Mugogo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha.Hassan Saidy wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha mkandarasi kutoka kampuni ya Central Electricals International Ltd katika Mradi wa HEP 2B ambaye anaenda kutekeleza kwenye vitongoji 218 mkoani Njombe.

"Jumla ya vitongoji vyote mkoa wa Njombe ni 1,833 na vitongoji vyenye umeme ni 1,276. Vilevile vitongoji ambavyo havina umeme ni 557. Hivyo mradi huu unakwenda kupeleka umeme kwenye vitongoji 218 katika mkoa huu na vitabakia vitongoji 339 ambavyo havina umeme navyo vitakamilika, " Amesema Mugogo.

Ameongeza kuwa, gharama za kuunganisha umeme huo ni shilingi 27,000 tu na kuwataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya kuunganisha umeme kwa gharama nafuu iliyowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Samia.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo mkoani Njombe, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Lewisi Mnyambwa amemshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha nyingi zaidi ya bilioni 24 ili kupeleka umeme kwenye vitongoji vya mkoa wa Njombe.

"Serikali kupitia REA imefanya kazi kubwa. Tunasisitiza miradi hii ikamilike kwa muda uliopangwa na tutaendelea kuusimamia ipasavyo ili mkandarasi aweze kutekeleza majukumu yake pasipo changamoto yeyote katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi," Amesema Mnyambwa. 

Aidha, ametoa rai kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi kumpatia ushirikiano mkandarasi huyo na ametakiwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ili kufanya shughuli mbalimbali katika mradi huo ili uchumi wa wananchi uongezeke na wanufaike na uwepo wa miradi hiyo katika mazingira yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi kutoka kampuni ya Central Electricals International Ltd, Bw. Zameer Meghji ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kupewa fursa ya kutekeleza mradi huo mkubwa. Amesema watahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, watashirikiana na wananchi na kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ili miradi hiyo ilete tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.


Friday, January 16, 2026

MUUNGANO WAZIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA KUIBUA VIPAJI VYA MICHEZO

Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na (Mazingira) wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.

******************

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itahakikisha uwepo wa Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar unaendelea kuimarika sambamba na kuibua fursa za ajira kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya michezo.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi (Januari 15, 2026) na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Ali wakati alipokuwa akizindua Ligi ya Taifa ya Muungano katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar.

Mhe. Abdulgulam amesema michezo ni fursa ya ajira kwa vijana wa na hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitahakikisha zinatumia fursa hizo kuibua vipaji kwa vijana na kuwatengeneza ajira.

"Mashindano haya ni sehemu ya matunda ya Muungano uliojengwa kwa misingi umoja, amani na mshikamano….Serikali zote mbili zitahakikisha zinatumia fursa ya mashindano haya kuwezesha vijana kujitengenezea fursa za ajira" amesema Mhe. AbdulGulam.

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inaendelea kushirikiana na Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANETA) na Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA)katika kuratibu mashindano hayo ili kuwa nguzo muhimu katika kukuza umoja, upendo na mshikamano kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa Serikali zote mbili ztaendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia sekta ya michezo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika viwanja mbalimbali hatua inayolenga kuibua vipaji kwa vijana na kutengeneza ajira kwa Kundi hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Hanifa Selengiu amesema Serikali zote mbili zimeanzisha mashindano hayo kwa aijli ya kuhakikisha Watanzania wanaendelea kufahamishwa umuhimu wa Muungano na fursa zinazoibuliwa zilizopo ikiwemo sekta ya michezo.

"Mashindano ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa mwaka 2024 kuhusu jukumu ilioipatia Ofisi ya Makamu wa Rais ya kuutangaza Muungano" amesema Selengu.

Amesema Michezo ni sehemu muhimu ya Muungano na hivyo mashindano hayo yamekuja katika wakati mwafaka hususani katika kipindi hiki ambacho Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA) Bi. Nasra Juma amesema mashindano hayo yameshirikisha jumla ya timu 11 ikiwemo timu sita (06)kutoka Tanzania Bara na tano (05) kutoka Zanzibar.

Amezitaja timu hizo kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Uhamiaji, Tamisemi, Kikosi cha Kujitolea Zanzibar (KVZ), Afya- Zanzibar, Jeshi la Zimamoto, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mbweni, Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Polisi Dodoma, Mafunzo na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).

Amesema Chama hizo kimeendelea kuweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha Ligi ya ya Netiboli ya Muungano itaendelea kupata washiriki wengi zaidi kwani mchezo huo kwa sasa umezidi kukua na kuweza kufungua milango ya fursa za ajira kwa vijana.

Katika michezo iliyochezwa mapema leo asubuhi Timu ya JKU iliwezesha kupata ushindi wa magoli 36 kwa 34 dhidi ya Polisi Arusha wakati Mafunzo Zanzibar iliiadhibu Timu ya Afya Zanzibar kwa magoli 79 kwa 24.
Watendaji Waandamizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)wakifuatilia matukio mbalimbali ya hafla ya uzinduzi Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Pete iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026. Aliyesimama ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Bi. Shumbana Taufiq.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Hanifa Selengu akiwasilisha salamu za Uongozi wa Ofisi hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Cecilia Nkwamu akifuatilia matukio mbalimbali ya hafla ya uzinduzi wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli)yaliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.

Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakipita mbele ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Hussein muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakipita mbele ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Hussein muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakiingia katika wa ndani wa Amani Complex, Zanzibar kwa ajili ya kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakiwa pamoja na wachezaji wa Timu mbalimbali zinazoshiriki mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli)iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.

Monday, December 1, 2025

SAANANE YAANDAA TUKIO LA KIHISTORIA: BIRTHDAY YA SIMBA — KEKI MAALUM KUPAMBA SIKU YA MFALME WA PORI

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Birthday ya Simba wa Saanane
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George akizungumza na waandishi wa habari

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane imeandaa tukio la kihistoria na la aina yake litakalowapa watalii na wananchi burudani ya kipekee, baada ya kutangaza kusherehekea miaka 10 ya simba anayeishi katika hifadhi hiyo. 

 Tukio hilo la kihistoria, ambalo halijawahi kufanyika katika hifadhi yoyote Tanzania, limepangwa kufanyika Desemba 20, 2025 katika kisiwa hicho kilichopo katikati ya Ziwa Victoria, jijini Mwanza.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 1, 2025, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George, amesema sherehe hiyo itafanyika chini ya kauli mbiu "Saanane King Turns Ten" na itahusisha matukio ya aina yake yanayolenga kuhamasisha utalii na kuongeza uelewa kuhusu uhifadhi wa wanyamapori.

"Simba ni mfalme wa nyika na mmoja wa wanyama maarufu barani Afrika na duniani. Katika Hifadhi ya Saanane, mnyama huyu amekuwa kivutio kikubwa na sehemu muhimu ya historia ya hifadhi. Tumetenga siku maalum kwa ajili yake ili kuenzi mchango wake katika utalii na elimu ya uhifadhi," amesema Dkt. Tutindaga.
Dkt. Tutindaga amefafanua kuwa, wageni watapata nafasi ya kumuona simba huyo akilishwa keki maalum iliyotengenezwa kwa umbo na malighafi salama kwa mnyama huyo, pamoja na kusimuliwa historia yake, mwenendo wa maisha yake, tabia zake, na nafasi yake katika kundi maarufu la The Big Five.

Dkt. Tutindaga ameeleza kuwa tukio hilo linalenga si tu kuwaburudisha watalii, bali pia kuongeza thamani ya utalii wa mijini (urban tourism) katika Mkoa wa Mwanza na kuonyesha kwamba vivutio vya kipekee havipo tu katika hifadhi kubwa, bali pia katika hifadhi ndogo zilizo karibu na miji.

"Watalii wengi wanaokuja Saanane hupenda kusikia simulizi za maisha ya simba, familia yake, uwezo wake wa kuwinda, na hata tabia zake wakati wa honeymoon. Hivyo tukio hili litatoa elimu kwa kina kuhusu maisha ya mnyama huyu," ameongeza.


Elimu, Zawadi na Maonesho kwa Wageni

Sherehe hiyo pia imelenga kuwanufaisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo pamoja na makundi mengine ya jamii. 

Wageni hasa wanafunzi watapata nafasi ya kuulizwa maswali kuhusu uhifadhi ambapo washindi watapewa zawadi mbalimbali ikiwemo mabegi yenye picha ya simba na nembo ya Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane.

Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka Kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Pellagy Marandu, amesema maandalizi yanaenda vizuri na kwamba siku hiyo itajumuisha maonesho ya uhifadhi, burudani, elimu kwa wageni na mawasilisho ya kihistoria kuhusu maisha ya simba huyo.
Pellagy Marandu

"Tumepanga siku ya burudani, elimu na ubunifu. Tunataka kila anayekanyaga Saanane tarehe hiyo ajue kuwa uhifadhi si nadharia tu, ni maisha halisi ya wanyama tunaoishi nao," amesema.


Mkutano wa kutangaza tukio hilo umehudhuriwa pia na Anifa John (Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza na Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Wanyamapori), Andrea Idrissa Mbwambo (Daktari Msaidizi wa Wanyamapori) na Mwalimu Gilbert Tindabatangile kutoka Shule ya Sekondari Mkolani, jijini Mwanza.

Kwa sasa, simba anaendelea kubaki miongoni mwa wanyamapori maarufu zaidi duniani, akivutia watalii kwa ujasiri, nguvu na hadhi yake kama mfalme wa pori. 

Tukio hili linatarajiwa kuongeza hamasa, ubunifu na upekee katika utalii wa ndani, huku likiipa Saanane nafasi ya kipekee katika ramani ya vivutio vya kipekee barani Afrika.

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni moja ya maeneo adimu yanayosimamiwa na TANAPA, ikiwa na hadhi ya pekee kama hifadhi ya kwanza Tanzania iliyopo katikati ya mji. Iko umbali wa dakika 10 tu kwa boti kutoka katikati ya jiji la Mwanza, jambo linaloifanya kuwa kivutio rahisi na cha kipekee kwa watalii wa ndani na nje.

Kisiwa hiki kina eneo la takriban 2.18 km², hivyo ni hifadhi ndogo kuliko zote nchini, lakini pamoja na ukubwa wake, kina utajiri mkubwa wa viumbe na mandhari. Historia yake inaanzia mwaka 1964 kilipoanzishwa kama bustani ya wanyamapori, baadaye kuwa game reserve mwaka 1991, na hatimaye kuwa Hifadhi ya Taifa mwaka 2013 chini ya TANAPA.

Saanane ina mandhari maridadi yenye miamba ya graniti, maporomoko madogo, mwambao wa ziwa, misitu midogo na uoto wa porini unaowavutia wapenzi wa bird watching na watalii wanaopenda utulivu. Wanyama kama impala, nyani, rock hyrax na ndege wa aina mbalimbali wanaonekana kwa urahisi.

TANAPA pia inaendeleza ubunifu wa utalii kupitia uanzishwaji wa mahema ya kulala (tented lodge) ndani ya hifadhi, hatua inayolenga kuifanya Saanane isiwe tu safari ya siku moja bali eneo la kukaa na kupata uzoefu kamili wa utalii wa mijini na pori kwa wakati mmoja.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Birthday ya Simba wa Saanane
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Birthday ya Simba wa Saanane
 Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza na Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Wanyamapori, Anifa John akielezea zaidi kuhusu Simba wa Saanane
 Daktari Msaidizi wa Wanyamapori, Andrea Idrissa Mbwambo akielezea zaidi kuhusu Simba wa Saanane
Mwalimu Gilbert Tindabatangile kutoka Shule ya Sekondari Mkolani, jijini Mwanza akielezea zaidi kuhusu Birthday ya Simba wa Saanane


Monday, November 10, 2025

BODABODA WENYE PIKIPIKI ZA MKATABA WALIA NA GHASIA ZA OKTOBA 29



Na Mwandishi wetu, Dodoma

Baadhi ya waendesha bodaboda jijini Dar es Salaam wameeleza kuathiriwa kiuchumi na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, zikisema matokeo ya tukio hilo yamewafanya wengi wao kuingia kwenye madeni makubwa kutokana na kusimama kwa shughuli zao za kila siku.

Akizungumza na Central, Bwana Issa Salala, dereva wa bodaboda anayefanya kazi kwa kutumia pikipiki ya mkataba, amesema vurugu hizo zilitokea wakati ambapo hakuwa na akiba yoyote, jambo lililosababisha kushindwa kulipa kodi ya pikipiki aliyokuwa akiitumia kwa kazi ya kila siku.

"Nililazimika kukaa ndani kwa zaidi ya siku tano bila kutoka kazini. Nilikosa fedha za kulipia pikipiki, na mwenye pikipiki aliendelea kudai hela zake. Ilikuwa kipindi kigumu sana," amesema Salala kwa uchungu.


Aidha, ameeleza kuwa hali hiyo ilichangia mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa, ambapo unga uliokuwa ukiuzwa shilingi 1,500 kwa kilo uliuzwa hadi shilingi 4,000, huku mchele ukipanda kutoka shilingi 2,000 hadi zaidi ya shilingi 5,000 kwa kilo moja.

Salala amesema changamoto hiyo imeonyesha namna vurugu na maandamano yasiyo na mpangilio mzuri yanavyoweza kuathiri maisha ya wananchi wa kipato cha chini, hasa vijana wanaojitafutia kipato kupitia sekta ya usafirishaji wa bodaboda.

"Ni muhimu vijana kufikiria mbele kabla ya kuchukua hatua. Wengi walioingia mitaani hawakujua madhara ya baadae. Tumeumia sisi na familia zetu. Tumepata hasara kubwa na hata hali zetu za kiafya zimebadilika," amesisitiza.

Wakati huo huo, wadau mbalimbali wa usafirishaji wameendelea kutoa wito kwa vijana nchini kujiepusha na matukio ya vurugu na badala yake kutumia muda na nguvu zao katika shughuli za kiuchumi zinazochangia ustawi wao binafsi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.




Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...