Saturday, November 7, 2026

WAENDESHA BODABODA 42 TANGA KUKABIDHIWA LESENI NOVEMBA 7

 


Na Rebeca Duwe Tanga


Waendesha pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda 42 jijini Tanga wanatarajiwa kukabidhiwa leseni zao za udereva Novemba 7, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza usalama barabarani na kupunguza ajali zinazotokana na ukosefu wa elimu ya udereva.


Hafla ya makabidhiano hayo inatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Police Mess jijini Tanga, kuanzia saa tano asubuhi, ambapo leseni hizo zitakabidhiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguz.


Polisi Tanga Kuimarisha Elimu ya Usalama Barabarani


Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Willy Mwamasika, amesema Jeshi la Polisi limejipanga kupunguza ajali za barabarani kwa kutoa elimu ya udereva na usalama barabarani kwa waendesha bodaboda.


Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya mafunzo yaliyotolewa kwa waendesha bodaboda katika kata 11 za Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mwamasika amesema mpango huo unalenga kuwafikia waendesha pikipiki wengi zaidi na kuwasaidia kupata leseni za udereva.


Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa baadhi ya waendesha bodaboda hawana uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni za usalama barabarani.


Vijana 42 Wakamilisha Mafunzo ya Udereva


Mwamasika amesema kuwa awali walilenga kuwapeleka vijana 100 kupata mafunzo ya udereva katika Chuo cha Udereva cha Bandiwe.


Hata hivyo, utekelezaji wa mpango huo ulikumbwa na changamoto mbalimbali. Kati ya vijana 100 waliolengwa, 78 waliweza kuanza mafunzo, lakini baadhi yao walishindwa kuendelea na kusababisha idadi kupungua hadi kufikia 57.


Aidha, vijana 42 wamefanikiwa kukamilisha mafunzo na wanatarajiwa kukabidhiwa leseni zao za udereva.


Baraza la Usalama Barabarani Kugharamia Mafunzo


Akielezea namna walivyosaidia vijana hao, Mwamasika amesema Baraza la Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, chini ya Mwenyekiti wake Mzee Rashid Liemba, liligharamia ada za mafunzo, mitihani ya udereva pamoja na gharama za uchakataji wa leseni.


"Mimi kama Katibu wa Baraza la Usalama Barabarani chini ya Mwenyekiti Mzee Rashid Liemba, tulifanikiwa kuwalipia ada za mafunzo, gharama za majaribio ya udereva (test fee) pamoja na gharama za kukata leseni ambazo ni shilingi 70,000," amesema Mwamasika.


Ameongeza kuwa ili kufikia lengo la vijana 100, walisajili wanafunzi wengine 43, lakini baadhi yao pia walishindwa kukamilisha mafunzo kutokana na changamoto mbalimbali.


Kati ya wanafunzi hao, vijana 15 waliaishia katikati ya mafunzo, huku juhudi zikiendelea kutafuta utaratibu wa kuwasaidia kupata leseni zao.


Bodaboda Wahimizwa Kutumia Fursa za Mafunzo


Mwamasika amewataka waendesha bodaboda kutumia fursa za mafunzo zinapotolewa, akieleza kuwa elimu ya udereva huwasaidia kubadili tabia, kufahamu sheria za barabarani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao pamoja na watumiaji wengine wa barabara.


Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kujenga kundi la waendesha bodaboda wenye uelewa wa kutosha kuhusu usalama barabarani na uwajibikaji katika shughuli zao za usafirishaji.


Hitimisho 


Makabidhiano ya leseni kwa waendesha bodaboda 42 jijini Tanga ni hatua inayolenga kuimarisha nidhamu ya barabarani na kuongeza uelewa wa sheria za usalama barabarani, huku juhudi za kuwafikia vijana wengine zikiendelea.


Mwisho

Wednesday, November 4, 2026

JIJI LA TANGA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA, WADAU WATAKIWA KUSHIRIKI

 


Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushiriki wa jamii nzima ili kukomesha vitendo hivyo haramu vinavyodhoofisha nguvu kazi na kuathiri maendeleo ya Halmashauri ya Jiji la Tanga.


Hayo yamesemwa na Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Khalid Rashid, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwanzange, wakati akifunga semina ya mafunzo ya siku tano iliyowashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo jijini humo.


Rashid alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, chini ya uongozi wa Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapher Selebos, hakuna kitakachoshindikana iwapo wadau watashirikiana kwa dhati.


Semina hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Red Cross jijini Tanga, chini ya uratibu wa asasi ya Gift of Hope, iliwashirikisha walimu, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa vijana, wakuu wa taasisi pamoja na waandishi wa habari.


Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwajengea uwezo washiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kuhakikisha Jiji la Tanga linakuwa eneo salama kwa wananchi.


Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Meya Rashid alisisitiza umuhimu wa kila mmoja kushiriki katika mapambano hayo, akisema ushirikiano huo utasaidia kukomesha vitendo vya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.


Alisema hali bado si nzuri katika Halmashauri ya Jiji la Tanga licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika, hivyo akasisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na wadau wote unahitajika zaidi.


"Naamini mafunzo haya ya siku tano mmeyapata kikamilifu. Msiyafungie kwenye makabati, bali mkayafanyie kazi kwa kuielimisha jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya," alisema Naibu Meya huyo.


Aidha, alisema jiografia ya Jiji la Tanga, ikiwemo ukaribu wake na nchi jirani ya Kenya pamoja na uwepo wa bandari, ni miongoni mwa sababu zinazoweza kutumiwa na wahalifu kama mianya ya kuingiza dawa za kulevya.


Hata hivyo, aliwataka wanaojihusisha na biashara hiyo haramu kuachana nayo mara moja, akieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.


Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la Jeshi la Polisi pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima, wakiwemo wananchi, viongozi wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali.


Pia aliipongeza asasi ya Gift of Hope kwa jitihada inazoendelea kuzifanya katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuiunga mkono ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.


Akifafanua umuhimu wa ushirikiano huo, Rashid alisema uwekezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati jijini Tanga unahitaji uwepo wa nguvu kazi yenye afya na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.


Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiletea nchi miradi mingi ya kimkakati inayohitaji vijana wenye afya njema na wasiokuwa katika matumizi ya dawa za kulevya ili waweze kunufaika na fursa za ajira zinazotokana na miradi hiyo.


Alionya kuwa vijana wasipojikinga na matumizi ya dawa za kulevya, wanaweza kupoteza fursa hizo na kuziacha zitumiwe na watu kutoka nje ya nchi.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Duga, Japhari Mohamed, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Uchumi na Afya, aliipongeza asasi ya Gift of Hope kwa jitihada zake za kupambana na dawa za kulevya.


Alisema amefurahishwa na mafunzo hayo na anaamini maarifa aliyoyapata yatasaidia katika kuelimisha jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.


Naye Mwalimu Yahaya Bakari alisema mafunzo hayo yamemuongezea maarifa yatakayomsaidia kusimamia nidhamu ya wanafunzi na kutambua viashiria vya awali vya tabia zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kujihusisha na dawa za kulevya.


Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii, Farida Adamjee, alisema semina hiyo imemwezesha kujifunza changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, akiahidi kutumia maarifa aliyoyapata katika kujenga jamii bora.


Naye Mwanasaikolojia Nancy Titus alisema mafunzo hayo yamemjengea uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya watu wa kada mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.


MWISHO.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...