Saturday, September 5, 2026

KABLA YA PENSHENI DAIMU SALUM MKWAWA ATOA SOMO LA KUWEKEZA MAPEMA KWA AJILI YA MAISHA BAADA YA KUSTAAFU

Hii ndio Royal Woodbridge Hotel iliyojengwa na kuwekezwa na mstaafu Daim Salum Mkwawa Hotel hii ipo  Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma mkabala na stendi ya Seedfarm njia inayokwenda Songea-Tunduru-LindiMuonekano wa ndani wa Hotel ya Royal Woodbridge iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma inayomilikiwa na Daimu Salum Mkwawa


Hapa ni eneo la kupatia chai na chakula katika Hotel ya Royal Woodbridge iliyopo Seedfarm Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Kustaafu kutoka kwenye ajira hakumaanishi mwisho wa uzalishaji au mchango wa mtu katika uchumi wa nchi, bali kunaweza kuwa mwanzo wa hatua nyingine ya maisha endapo mtumishi ataandaa mapema shughuli za kiuchumi zitakazomsaidia baada ya kuondoka kazini.

Hilo ni miongoni mwa masomo yanayoweza kupatikana katika safari ya Daimu  Salum Mkwawa, msomi na mwanazuoni aliyewahi kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za Serikali na baadaye kuhudumu katika Umoja wa Mataifa (UN) kwa miaka 18.

Mkwawa, ambaye sasa ni mstaafu, anasema umuhimu wa kujiandaa kwa maisha baada ya kustaafu haupaswi kuanza siku mtu anapomaliza ajira, bali unapaswa kuanza mapema wakati bado ana nguvu, kipato na uwezo wa kupanga maisha yake ya baadaye.

Anaeleza kuwa yeye mwenyewe alianza kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo tangu mwaka 1992, wakati bado akiwa katika ajira, ikiwa ni pamoja na miradi aliyoianzisha Dar es Salaam.

Safari yake ya kikazi ilimfikisha katika Wizara ya Kilimo na Kiwanda cha Sukari Kilombero, ambako anasema alipata pia uzoefu wa namna ya kutengeneza sukari.

Katika upande wa elimu, amesoma katika vyuo mbalimbali, vikiwemo Sokoine University of Agriculture (SUA) na Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza, kabla ya kuendelea na safari yake ya kitaaluma na kikazi.

Mwaka 1996, alifanya kazi na Umoja wa Mataifa hapa nchini kwa kipindi cha miaka 18, akihudumu kwa ukaribu zaidi na Serikali za Mitaa.

Baada ya mkataba wake nchini Tanzania kumalizika, Mkwawa anasema Umoja wa Mataifa ulimpa fursa ya kuendelea kufanya kazi nje ya nchi kutokana na uzoefu na umahiri aliokuwa ameonesha kazini.

Hata hivyo, aliamua kubaki Tanzania. Sababu mojawapo ilikuwa uwekezaji aliokuwa ameanza kuujenga nchini, pamoja na kuzingatia familia na umri ambao ulikuwa umeendelea kusogea.

Uamuzi huo ulimfanya aendelee na safari yake ya ujasiriamali, ikiwemo uwekezaji katika sekta ya hoteli.

Moja ya uwekezaji huo ni Royal Woodbridge Hotel, iliyopo Kata ya Seedfarm, Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma.

Kwa Mkwawa, uwekezaji huo siyo tu shughuli ya kibiashara, bali ni sehemu ya namna mstaafu anaweza kuendelea kutumia uzoefu, mtaji na maarifa aliyoyapata katika maisha ya ajira kwa ajili ya kujenga uchumi wake na kuchangia uchumi wa jamii inayomzunguka.

Hoteli hiyo kwa sasa ina vyumba 20, ikiwa na matarajio ya kufikia vyumba 30, pamoja na mpango wa kuwa na eneo la kuogelea na ukumbi wa mikutano.

Pamoja na kutoa huduma za malazi, uwekezaji huo umewezesha ajira kwa vijana wa kike na wa kiume, huku hoteli ikinunua bidhaa za chakula kutoka kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa sokoni.

Kwa namna hiyo, shughuli za hoteli zinakuwa sehemu ya mnyororo wa kiuchumi unaowaunganisha mmiliki wa biashara, wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara wa masoko, wasambazaji wa bidhaa na Serikali kupitia mapato mbalimbali.

Mkwawa pia anasisitiza umuhimu wa rasilimali watu katika sekta binafsi, akisema wafanyakazi wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza uwezo wao na kuhakikisha wageni wanapata huduma bora.

Huduma zinazopatikana katika hoteli hiyo ni pamoja na chakula, usalama ndani na nje ya eneo la hoteli, CCTV camera, Wi-Fi ya bure, parking ya magari, restaurant na kifungua kinywa cha bure kwa wageni wanaolala hotelini hapo.

Pia, hoteli hiyo ina mazingira yanayovutia kwa ajili ya kupiga picha, hali ya hewa inayovutia na vyumba vinavyolenga kutoa viwango vya huduma vinavyolingana na thamani ya fedha anayolipa mgeni.

Mkwawa anasema usalama, chakula bora, malazi yenye viwango na huduma zinazokidhi mahitaji ya wageni ni sehemu muhimu ya uwekezaji katika sekta ya utalii na ukarimu.

Kwa upande mwingine, anaitaja Serikali kama mshirika muhimu katika mafanikio ya wafanyabiashara, akipongeza ushirikiano uliopo baina ya Serikali na sekta binafsi.

Anaiomba Serikali kuendelea kuangalia mazingira ya wafanyabiashara, hususan biashara changa, wakati wa ukusanyaji wa kodi, ili kuwe na mazingira ambayo Serikali inapata mapato na mfanyabiashara anaendelea kufanya biashara yenye faida na endelevu.

Kwa maoni yake, Serikali inapaswa pia kuwa mshauri wa wafanyabiashara na kuwasaidia kufikia huduma za mikopo kwa urahisi zaidi.

Mchango wa uwekezaji huo unaonekana pia katika mapato ya Serikali kupitia Manispaa ya Songea na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku ajira na ununuzi wa bidhaa kutoka kwa wajasiriamali wa eneo hilo ukiendelea kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi wa Songea.

Mkwawa anasema uzoefu wake ni ushahidi kwamba maandalizi ya maisha baada ya kustaafu yanaweza kufanyika hatua kwa hatua, badala ya kusubiri mtu aondoke kazini ndipo aanze kutafuta shughuli ya kumuingizia kipato.

Kwa wastaafu na watumishi wanaokaribia kustaafu, simulizi hii inaweza kuwa ukumbusho wa umuhimu wa kuanza mapema kupanga maisha ya baada ya ajira, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika shughuli halali na endelevu kulingana na uwezo na utaalamu wa mtu.

Hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa pensheni pekee na kumwezesha mstaafu kuendelea kuwa mzalishaji, mwajiri na mshiriki wa shughuli za maendeleo katika jamii.

Kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, Mkwawa anasema uwekezaji katika huduma za malazi na biashara nyingine unaweza kusaidia kuongeza uwezo wa Songea kuhudumia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Royal Woodbridge Hotel, iliyopo katika Kata ya Seedfarm, Manispaa ya Songea, kando ya barabara kuu ya Songea–Tunduru–Lindi, ni miongoni mwa uwekezaji unaoonesha namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki katika kutoa huduma, ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Mkwawa anawakaribisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, mikoa jirani ya Tanzania pamoja na wageni kutoka nje ya nchi wanaofika Songea kutumia huduma zinazopatikana katika hoteli hiyo na kujionea wenyewe namna huduma zinavyotolewa.

Pia anasema hoteli hiyo inawezesha usafiri wa ndani ya Mkoa wa Ruvuma kwa wageni wanaohitaji huduma hiyo.

Ujumbe mkubwa unaotokana na safari yake ni kwamba maandalizi ya kustaafu yanapaswa kuanza kabla ya kustaafu. Kwa mtumishi mwenye uwezo na mpango, ajira inaweza kuwa chanzo cha mtaji wa kuanzisha uwekezaji wa baadaye, huku uzoefu wa kazi ukiwa rasilimali muhimu katika kusimamia biashara na kutoa mchango zaidi kwa jamii.

Kwa Taifa, simulizi kama hii inaendelea kuonesha umuhimu wa kuimarisha mazingira ya uwekezaji wa ndani ili wastaafu, wafanyakazi na wajasiriamali waweze kutumia maarifa, uzoefu na mitaji yao kujenga biashara, kutoa ajira na kuongeza shughuli za uzalishaji nchini.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...