Saturday, September 5, 2026

BANDARI YA DAR ES ALAAM KUPANUA UWEZO KUPITIA MIRADI MIKUBWA




Na Sheila Ahmadi, Dar esalaam

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati katika Bandari ya Dar es Salaam, inayolenga kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo, kuimarisha ufanisi wa bandari na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali nchini na nje ya Tanzania.

Akizungumza Jijini Dar es salaam na Wanahabari Mara baada ya Kukagua miradi ya kimkakati kwenye bandari ya Dar esalaam Mkurugenzi wa huduma za uhandisi wa bandari Hiyo Mhandisi Erick Madinda, amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya bandari ili kuongeza uwezo wa kupokea na kuhudumia mizigo kwa wakati, pamoja na kuimarisha ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika ukanda wa Afrika Mashariki.

eneo la Malindi ni miongoni mwa maeneo yanayofanyiwa maboresho kupitia mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam ambao unajumuisha ujenzi na uboreshaji wa Gati, maeneo ya magari ambapo Mradi huo unagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 5.44.

Madinda alisema Kurasini Logistics Centre ni miongoni mwa miundombinu muhimu inayojengwa kwa ajili ya kupokea na kuhifadhi mizigo kabla ya kukamilishwa kwa taratibu za kisheria na baadaye kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Aidha kituo hicho chenye ukubwa wa takribani mita za mraba 200,000 kitakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya makontena 14,000, jambo litakalosaidia kupunguza muda wa mizigo kukaa katika yadi za bandari na kuongeza kasi ya utoaji wa mizigo.

“Kurasini Logistics Centre itaunganishwa na reli za Standard Gauge Railway (SGR) na Meter Gauge Railway (MGR), ili kuwezesha mizigo kusafirishwa moja kwa moja kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali kwa njia ya reli,” alisema Madinda"

Katika hatua nyingine Madinda Ameongeza kuwa Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa inapokea takribani tani milioni 33.7 za mizigo kwa mwaka, huku Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya barabara na reli pamoja na mifumo ya usafirishaji wa mizigo ili kuongeza ufanisi na kupunguza msongamano wa malori.

Hata hivyo ziara hiyo ilihusisha ukaguzi wa ujenzi wa Single Receiving Terminal (SRT), mradi unaolenga kuboresha upokeaji na usafirishaji wa mafuta kutoka bandarini.

Mradi huo unatarajiwa kurahisisha upokeaji wa mafuta kutoka kwenye meli na kupunguza gharama za uendeshaji. Unajumuisha matanki 15 kwa ajili ya kuhifadhi dizeli na petroli.

Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Jamal Mluma, alisema ujenzi wa SRT umefikia asilimia 52.8 na unagharimu Sh bilioni 678.6.

Vilevile mradi huo utakapokamilika utakuwa na mfumo wa kisasa wa kuhifadhi mafuta kwa muda mfupi na kutumia teknolojia za kisasa katika uendeshaji wake. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.

Naye Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM) Kareen Marry, alisema ziara hiyo imewapa fursa ya kujionea kwa vitendo utekelezaji wa miradi ya Serikali, akieleza kuwa hatua hizo zinaonyesha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za bandari na kupunguza changamoto ya foleni pamoja na muda wa meli na malori kukaa bandarini.








Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...