Friday, April 4, 2025

TAFITI ZA KISAYANSI ZINACHOCHEA MABORESHO YA HUDUMA ZA AFYA NCHINI




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema imeendelea kushirikiana na taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika nchini zinagusa mahitaji halisi ya wananchi na kuchangia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe ameeleza kauli hiyo jijini Dodoma, Aprili 4, 2025 wakati wa Ufunguzi wa Mdahalo wa Kitaaluma (Symposium) katika Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa.

amesema kuwa tafiti katika sekta ya afya ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha huduma bora na zenye tija kwa wananchi, hasa kupitia tafiti za magonjwa ya binadamu ambazo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuboresha afya ya jamii.

"Tafiti mbalimbali, hasa katika maeneo ya magonjwa kama vile Malaria, Kifua kikuu na yale ya kuambukiza, zimekuwa chachu ya mabadiliko chanya kwenye sera na mbinu za utoaji huduma," amesema Dkt. Shekalaghe.


"Tafiti zimetuwezesha kuwa na ushahidi wa kisayansi unaoongoza matumizi ya dawa mpya, mbinu bora za kinga na pia kubaini maeneo yenye changamoto kubwa zaidi kiafya," amesema Dkt. Shekalaghe.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema mdahalo huo wa kitaaluma utasaidia katika kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya afya nchini.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa hakuna halmashauri nchini isiyokuwa na hospitali, jambo linalothibitisha mafanikio ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya.

Maadhimisho ya Wiki ya Afya kitaifa yenye Kauli mbiu isemayo " Tulipotoka, Tulipo, Tunapoelekea; Tunajenga Taifa Imara Lenye Afya" yanafayika kuanzia Machi 3 hadi 8 Aprili, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, yakihusisha utoaji wa huduma za afya bure, maonesho ya taasisi, vipimo, chanjo pamoja na mijadala ya kitaalam.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...