
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya wazazi CCM wilaya Shinyanga Mjini wanaendelea na ziara ya kutembelea kata mbalimbali za Jimbo la Shinyanga Mjini.
Ziara hii inahusisha kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM, kufanya tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuangalia hali ya uhai wa chama, na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo hayo.
Ziara hiyo ilianza tarehe 18 Februari 2025 na hadi sasa, na leo Februari 20,2025 wajumbe wamefika katika kata ya Ndembezi, Chibe, na Ibinzamata.
Wakiwa katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, amesisitiza umuhimu wa wanachama wa CCM kudumisha mshikamano na umoja ili kuimarisha chama na kuendelea na utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
Mrindoko pia ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo, ikiwemo miradi ya barabara, elimu, maji, na afya, na kuhimiza jamii kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, Mrindoko ametoa wito kwa jamii kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya unyanyasaji, huku akionya kuhusu vitendo vya ulawiti na ubakaji, na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za haraka ili kukomesha vitendo hivi vinavyohatarisha usalama wa watoto.
Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mary Makamba, ametoa onyo kwa akina mama kuhusu madhara ya ulevi kwa familia.
Mary Makamba
Amesisitiza kwamba ulevi, hasa pombe, unachangia migogoro ya familia na hata kudhoofisha afya ya akili ya akina baba.
Ameeleza kwamba baadhi ya ndoa zimevunjika au kuingia matatizoni kwa sababu ya tabia ya wanawake kujiingiza katika ulevi.
Makamba pia amewahimiza akina mama kupunguza matumizi ya pombe na kuzingatia malezi bora ya familia.
"Mama zangu tupunguze pombe, tupunguze ulevi... kuna msemo tunasema 'kumwagilia moyo'. Ndoa nyingi zipo mahakamani kwa sababu ya sisi akina mama tumekuwa walevi, tunakunywa sana pombe, unakuta mama anaenda kulewa anarudi nyumbani usiku wa manane matokeo yake imekuwa chanzo migogoro katika familia, tunawatengenezea akina baba matatizo ya afya ya akili, wanashindwa kutafuta pesa",amesema Makamba.
Aidha ametahadharisha kuhusu mavazi yasiyofaa na athari zake katika jamii, na akatoa tahadhari kuhusu wanawake kujihusisha na mikopo umiza, ambayo pia imetajwa kuwa chanzo cha migogoro ndani ya familia.
Ziara hii inaendelea kuhamasisha umoja, maendeleo, na maadili mema katika jamii, huku wakazi wa Shinyanga Mjini wakiwa na nafasi ya kujadili masuala ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi kwa lengo la kujenga mustakabali bora kwa wote.

