Saturday, February 22, 2025

DAWASA WATANGAZA FURSA LUKUKI KWA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA


Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire ametangaza fursa lukuki kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Kigamboni zitakazotokana na ushirikiano bora uliitengenezwa baina yao na Mamlaka hiyo.

Mhandisi Bwire amebainisha fursa hizo katika kikao kazi na wenyeviti hao kilicholenga kuboresha mahusiano na kujenga ukaribu baina ya Serikali za Mitaa na DAWASA.

"Ukaribu huu unakuja na fursa nyingi ndugu wenyeviti ambazo zitanufaisha pande zote mbili , Serikali pamoja na wenyeviti kama mtu mmoja mmoja, kuanzia saa wwenyekiti atakaetusaidia kuhamasisha maunganisho na kutuletea wateja atapata kiasi cha Shilingi 10,000 kwa kila mteja mmoja anaemleta," amesema Mhandisi Bwire.

Bwire amesema sio hivyo tu lakini hata kwa wale ambao watasaidia kufichua wahujumu kwa Mamlaka mfano wezi wa maji hawataacha hivi hivi bali nao watanufaika kwa uzalendo watakaouonyesha.

"Ndugu zangu wenyeviti kwa kila mmoja wenu atakae saidia kubaini mwizi wa maji na tukamkamata na kumpiga faini basi Mwenyekiti uliesaidia kubaini hilo utapata asilimia 30 ya fedha zitakazolipwa kama faini," amesema Mhandisi Bwire

Bwire amesema motisha hii kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa itakua chachu ya wao kushirikiana na Mamlaka zaidi katika shughuli za kila siku kuwapatia huduma ya maji wananchi.

Mhandisi Bwire amesema hawataishia hapo tu bali watatoa motisha kwa kila Mwenyekiti atakaesaidia kushawishi mteja aliesitishiwa huduma Kulipa deni lake na kurudi kutumia huduma za DAWASA.

Hatua hii imepokelewa vyema na wenyeviti waliohudhuria kikao kazi hicho huku wakiahidi kufanya kazi bega kwa bega na DAWASA kuhakikisha wananchi wanapata huduma Bora ya Majisafi wakati wote.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...