Waziri Silaa ametoa maagizo hayo leo tarehe 16 Desemba, 2024 wakati akizindua Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa maagizo hayo yanakuja kufuatia maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 10 Desemba, 2024, Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar wakati wa hafla ya uapisho wa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Naibu Makatibu Wakuu na Mabalozi kuhusu usimamizi wa shirika hilo kujiendesha kibiashara.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa Bodi na menejimenti ya Shirika la TTCL, Waziri Silaa amesema, "Serikali ya Rais Dkt. Samia imewekeza fedha nyingi katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo mkongo wa taifa wa mawasiliano, minara ya mawasiliano, pamoja na kituo cha kuhifadhia data cha taifa (National Data Center).
"Nia ya Rais ni kuona uwekezaji huu mkubwa unaleta tija nchini." Amesema Waziri Silaa na kuongeza;
"Shirika hili likiendeshwa vyema lina uwezo wa kusaidia sekta nyingine, kwa sababu wizara yetu ni wezeshi katika mawasiliano, hivyo wizara nyingine na Taasisi zinaitegemea katika kukuza sekta zao za TEHAMA."
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TTCL Bw. David Nchimbi amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua kuongoza bodi hiyo na kuahidi kusimamia shirika ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Bw. Nchimbi amemshukuru Waziri Silaa kwa utayari alioonesha na kuahidi kuwa bodi itatoa ushirikiano kwa wizara wakati wote itakapokuwa inatekeleza majukumu yake.