CHUO Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Kwa kushirikiana na Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na vyuo vya kati visivyo vya Serikali (TAMONGSCO) wametoa Mafunzo kuhusu namna bora ya uendeshaji wa shule za Msingi , Sekondari na vyuo vya kati kwa Wamiliki na Mameneja wa shule na vyuo vya kati visivyo vya Kiserikali nchini
Mafunzo hayo yatawapa fursa kujifunza masuala mbalimbali hususan fedha, uongozi pamoja kuwasilisha maoni na mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria ya elimu.
Akizungumza leo Desemba 16,2024 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo hayo ya Siku mbili, Kaimu Naibu Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba amesema mafunzo hayo yanakwenda kusaidia kuleta ufanisi na ubora mkubwa katika shule na vyuo vyao.
Amesema wataalamu ambao wanawapitisha kwenye mada mbalimbali ni wazoefu na watahakikisha washiriki kupata uelewa mkubwa na kwenda kuboresha maeneo yao .
"washiriki wote ninawasihi msikilize kwa makini mada zote ambazo zitawasilishwa, naamini mtapata uelewa mkubwa kwani wataalamu watakaowapitsha kwenye mada zilizoandaliwa ni wazoefu". Amesema Coretha.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Mafunzo hayo, CPA Charles Albert amesema mafunzo hayo yatasaidia kuboresha mifumo yao ya malipo na matumizi sahihi ya fedha pamoja na mipango ya kibajeti na maendeleo endelevu ya shule zao.
"Ambao wamepata taarifa na hawakuweza kufika kwenye mafunzo haya wamekosa uelewa wa namna ya upangaji wa bajeti zao kwasababu nimeangalia wamiliki wengi wa shule walikuwa hawajui kupanga bajeti zao vizuri lakini pia walikuwa hawajui viwango gani ambavyo vinatakiwa vikatwe kodi hasa katika kodi ya ongezeko la thamani inayotokana na mishahara ya wafanyakazi". Amesema
Naye mmoja wa washiriki, Mkurugenzi wa shule ya Morelight ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa shule na vyuo vya kati visivyo vya Kiserikali (TAMONGSCO) Wilaya ya Ubungo, Gervas Njoele amesema wamefundishwa namna ya kuendesha taasisi zao hasa kimapato na matumizi.
"Kwenye biashara unapopata mafunzo na semina mbalimbali za namna hii, zinatusaidia kujua namna za kuziendesha hizi taasisi ambazo zipo kwenye jamii". Amesema Gervas.
Mkuu wa Idara ya Kozi fupi na Shauri za kitaalamu Chuo Kikuu Mzumbe Dkt Darlene Mutalemwa na Mratibu wa mafunzo ambaye pia ni Katibu Mkuu TAMONGSCO Bw. Youstor Ntungi wamesema Mafunzo hayo yanashirikisha Wamiliki na Mameneja zaidi ya themanini(80) kutoka Shule za Msingi, Sekondari na vyuo vya kati kutoka Tanzania.
Kaimu Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt.Coretha Komba akifungua mafunzo.
Mratibu wa Mafunzo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TAMONGSCO Bw. Youstor Ntungi (kulia) akitambulisha washiriki kabla ya Mafunzo kuanza