Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (Kulia) akimweleza Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Katikati) kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Wizara hiyo muda mfupi baada ya Mhe. Dkt. Kijaji kuwasili makao Makuu ya Wizara hiyo yaliyopo kwenye mji wa Serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma Disemba 13, 2024.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akieleza mikakati ya Wizara hiyo inayolenga kuimarisha sekta za Mifugo na Uvuvi muda mfupi baada ya kuwasili makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo kwenye Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma Disemba 13, 2024.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili ofisini kwake makao Makuu ya Wizara hiyo yaliyopo kwenye Mji wa Serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma Disemba 13, 2024.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili ofisini kwake makao Makuu ya Wizara hiyo yaliyopo kwenye Mji wa Serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma Disemba 13, 2024.
****
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewataka wataalam wa Wizara hiyo kutumia taaluma walizonazo kuwatumikia wafugaji na Wavuvi kwa weledi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Dkt. Kijaji amesema hayo leo Disemba 13, 2024 mara baada ya kuwasili na kupokelewa kwenye Ofisi za makao makuu ya Wizara hiyo zilizopo Mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa Viongozi wengi na wataalam wamesoma kupitia kodi za Watanzania hivyo hawana budi kuwahudumia ipasavyo pindi wakifika uwandani.
"Kule uwandani wafugaji na wavuvi wetu wanajua zaidi kuliko sisi lakini sisi tumesoma ili tuweze kuwasaidia kile wafanye kwa usahihi zaidi kile wanachofanya" Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji ameongeza kuwa dhamira yake ni kuendeleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa mtangulizi wake Mhe. Abdallah Ulega ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wa sekta za Mifugo na Uvuvi kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2030.
Katika hatua nyingine Mhe. Kijaji ameelezea kusikitishwa kwake na mgogoro wa wakulima na wafugaji uliotokea Wilayani Kilosa hivi karibuni ambapo ameitangaza Wilaya hiyo kama kanda maalum na kuahidi kutumia kanda hiyo kama mfano wa kushughulikia migogoro ya aina hiyo kwenye maeneo mengine.
"Nimemjulisha mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuwa tutakuwa huko Wiki ijayo ambapo tutapanga kwa pamoja kati ya watu wa Ardhi, Kilimo na Mifugo ili tuondoe hii migogoro ambayo haina umuhimu kwa wafugaji na wakulima wetu kwa sababu sisi ni wamoja na wakati mwingine mfugaji huyo huyo ndo mkulima.
Mhe. Dkt. Kijaji amehitimisha maelekezo yake kwa kugusia sera ya uchumi wa buluu ambapo amewataka wataalam wa sekta ya Uvuvi kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi na utekelezaji wake unabadili maisha ya Wavuvi kwa ujumla.